Jumamosi, 27 Januari, 2024
Leo ni Jumamosi 15 ya mwezi Rajab 1445 Hijria mwafaka na 27 Januari 2024 Miladia.
Tarehe 15 Rajab miaka 1450 iliyopita, kundi la kwanza la Waislamu lilianza safari ya kuondoka Makka na kuhamia Uhabeshi barani Afrika. Hijra hiyo iliyokuwa na taathira kubwa katika harakati za Uislamu, ilifanyika miaka 8 kabla ya Mtume (saw) kuhamia Madina. Baada ya kushadidi mashaka ya Waislamu waliokuwa wakiteswa na kusumbuliwa na washirikina wa Makka, Mtume Muhammad (saw) aliwaamuru baadhi ya maswahaba zake waelekee katika ardhi ya Uhabeshi barani Afrika kwa ajili ya kujilinda na adha na mateso ya washirikina. Kundi hilo la Waislamu lililojumuisha wanaume 11 na wanawake 4 likiongozwa na Uthman bin Madh'un, lilihamia Uhabeshi na kutayarisha uwanja na mazingira mazuri ya Hijra ya pili ya Waislamu kuelekea katika ardhi hiyo ya Afrika. Kundi hilo la pili liliongozwa na binamu wa Mtume wetu Muhammad (saw), Ja'far bin Abi Twalib. Hijra hizo mbili zilikuwa na mchango mkubwa wa kueneza zaidi dini ya Uislamu barani Afrika. ***
Miaka 1443 iliyopita katika siku kama ya leo, mnamo tarehe 15 Rajab mwaka wa Pili Hijria, Kibla cha Waislamu kilibadilishwa kutoka Baitul Muqaddas na kuelekea Makka kwa amri ya Mwenyezi Mungu. Mayahudi daima walikuwa wakiwakebehi Waislamu kwa vile walikuwa nao wakielekea kwenye kibla hicho hicho cha Baitul Muqaddas. Hali hiyo iliwatia unyonge Waislamu na hasa Mtume Mtukufu SAW, na kwa minajili hiyo, katika siku kama ya leo Mwenyezi Mungu aliteremsha wahyi kwa Mtume SAW kupitia Malaika Jibrail AS akimtaka aelekee Makka wakati wa ibada ya Swala, badala ya Baitul Muqaddas. ***
Siku kama ya leo miaka 1385 iliyopita mwafaka na tarehe 15 Rajab mwaka 60 Hijria, alifariki dunia Muawiyah bin Abu Sufiyan, adui mkubwa wa Ahlibaiti wa Mtume Muhammad (saw) na mwasisi wa utawala muovu wa Bani Umayyah. Muawiyah alizaliwa miaka 15 kabla ya kuhama Mtume SAW kutoka Makka na kuelekea Madina, na alisilimu wakati jeshi la Kiislamu lilipoukomboa mji wa Makka mwaka wa 8 Hijria. Muawiyah alishika ugavana wa Sham wakati wa Ukhalifa wa Omar bin Khattab. Wakati wa uongozi wa Imam Ali bin Abi Twalib (A.S) alianzisha vita vya Siffin kwa kisingizio cha kulipiza kisasi cha kuuawa Othman bin A'ffan. Alibadilisha uongozi wa Kiislamu ni kuufanya sawa na usultani na ufalme wa Warumi. Mbali na kufanya mauaji ya mjuu mkubwa wa Mtume Muhammad (saw), Imam Hassan bin Ali (as), Muawiyah bin Abi Sufiani pia alimrithisha utawala mwanaye fasiki, mlevi na katili Yazid, ambaye pia alimuua kikatili mjukuu wa pili wa Mtume (saw), Imam Hussein bin Ali (as). ***

Siku kama ya leo miaka 1383 iliyopita kulingana na kalenda ya Hijria, alifariki dunia Bibi Zaynab (as) mjukuu wa Mtume Mtukufu (saw) baada ya kuvumilia mateso na machungu mengi. Bibi Zaynab (as) alizaliwa mwaka wa 6 Hijria na alipata malezi bora kutoka kwa baba yake, Imam Ali na mama yake, Bibi Fatimat Zahra (as). Mwaka 61 Hijria, Bibi Zaynab (as) alishiriki katika mapambano ya Karbala pamoja na kaka yake, Imam Hussein (as) na watu wengine wa familia ya Mtume (saw). Baada ya kuuawa shahidi Imam Hussein (as) na wafuasi wake, Bibi Zaynab alikuwa mfikisha ujumbe wa hamasa ya kudumu ya Imam Hussein na wafuasi wake. ***

Miaka 133 iliyopita katika siku kama hii ya leo alizaliwa Ilya Ehrenburg mwandishi wa Umoja wa Kisovieti yaani Urusi ya zamani. Ilya alifanya kazi ya uandishi habari kwa miaka kadhaa huko Uhispania na kuanza kujishughulisha na utunzi wa mashairi pia. Ehrenburg alifahamika vyema nchini humo kama mwandishi wa hadithi na mwanahabari, khususan pale alipokuwa akiripoti matukio katika Vita vya Kwanza vya Dunia, vya Pili na vile vya ndani vya Uhispania. Mwandishi huyo wa Kirusi aliandika vitabu visivyopungua 100 vikiwemo vya "Tufani" na "Kuanguka Paris". Ilya alifariki dunia mwaka 1967. ***

Siku kama ya leo miaka 51 iliyopita, makubaliano ya kusitisha vita kati ya Marekani na Vietnam Kaskazini yalitiwa saini mjini Paris, Ufaransa baada ya mazungumzo yaliyodumu kwa kipindi cha miaka minne. Kwa mujibu wa makubaliano hayo ya Paris, Marekani ilikubali kuondoa majeshi yake huko Vietnam Kusini. Japokuwa baada ya kutiwa saini makubaliano hayo vita kati ya Marekani na Vietnam Kaskazini havikusitishwa, lakini serikali ya Washington ililazimika kuondoa majeshi yake huko Vietnam Kusini baada ya kupata hasara kubwa za hali na mali. Makubaliano ya Paris yalikuwa pigo kubwa kwa siasa za uingiliaji kati na za kibeberu za Marekani nchini Vietnam ambazo zilianza kutekelezwa mwaka 1964. ***