Jumatatu, 29 Januari, 2024
Leo ni Jumatatu tarehe 17 Rajab, 1445 Hijria sawa na tarehe 29 Januari, 2024 Miladia
Miaka 324 iliyopita katika siku kama ya leo tarehe 17 Rajab mwaka 1121 Hijria, alifariki duani Allamah Fadhil Sheikh Sulaiman Bahrani, aliyekuwa miongoni mwa wasomi wakubwa wa Kiislamu.
Sheikh Abul-Hassan Sulaiman Ibn Abdillah Ibn Ali Ibn Hassan Bahrani Mahuzi, maarufu kwa jina la Muhaqqiq Bahrani, mmoja wa maulama wa Kiislamu wa madhehebu ya Shia mwanzoni mwa karne ya 12 Hijiria, alizaliwa katikati ya mwezi wa Ramadhani mwaka 1076 Hijiria. Alibobea katika elimu ya Hadithi, wapokezi wa Hadithi, historia na maisha ya mtukufu Mtume (saw) na Ahlu Baiti wake (as).

Sheikh Abdullah Samahiji na Sayyid Hashim Bahrani, mwandishi wa tafsiri ya Qur'ani ya Al-Burhan na Sheikh Ahmad Bahrani, ni miongoni mwa wanafunzi wa Allamah Fadhil Sheikh Sulaiman Bahrani. ***
Miaka 287 iliyopita, mnamo Januari 29, 1737 alizaliwa Thomas Paine, mwanasiasa na mwandishi mwanamapinduzi wa Uingereza. Baada ya kumaliza masomo yake ya elimu ya kati Paine aliamua kujishughulisha na kazi mbalimbali lakini hakufanikiwa katika yoyote kati ya hizo.
Hatimaye mnamo mwaka 1774, yaani mwaka mmoja kabla ya kuanza vita vya uhuru wa Marekani aliwasili nchini humo na kuanza kazi ya uandishi. Tasnifu yake iliyoitwa "Akili Timamu" iliwaathiri mno wananchi na viongozi wa Marekani na kuimarisha azma yao ya kujikomboa kutoka kwenye makucha ya Uingereza. Baada ya uhuru wa Marekani, Thomas Paine alirejea kwao Uingereza ambako aliandika kitabu "Haki za Mtu" kutetea Mapinduzi ya Ufaransa. Kwa sababu huko Uingereza alitambuliwa kama haini, Paine alilazimika kuelekea Ufaransa ambako alichaguliwa kuwa mjumbe wa Baraza la Taifa. Alifia Marekani mwaka 1809 katika hali ya simanzi na ufakiri.
Miaka 98 iliyopita, mnamo tarehe 29 Januari 1926, alizaliwa Profesa Muhammad Abdussalam, mwanafizikia mbobezi wa Pakistan katika mji wa Punjab mashariki ya nchi hiyo.
Abdussalam, ambaye alizaliwa katika familia ya kidini alianza kudhihirisha mapema kipawa kikubwa alichokuwa nacho kwa kufanikiwa kuingia chuo kikuu cha Punjab akiwa na umri wa miaka 14. Na baada ya kuhitimu shahada ya pili ya Uzamili akiwa na umri wa miaka 20 alielekea chuo kikuu cha Cambridge nchini Uingereza. Baada ya kuhitimu shahada ya kwanza ya Hisabati na Fizikia, mwaka 1951, Abdussalam alihitimu shahada yake ya Uzamivu au PhD ya Fizikia na kutunukiwa tuzo ya Adams.
Mwaka 1979, Profesa Muhammad Abdussalam pamoja na watafiti wengine wawili, alitunikiwa tuzo ya amani ya Nobeli na kuwa mwanasayansi wa kwanza katika Ulimwengu wa Kiislamu kushinda tuzo hiyo. Mwanasayansi huyo aliteuliwa kuwa mshauri wa masuala ya sayansi na elimu wa rais wa Pakistan kuanzia mwaka 1961 hadi 1974. Katika uhai wake, Muhammad Abdussalam alivumbua vitu kadhaa wa kadhaa na aliaga dunia mwaka 1996. *
Miaka 82 iliyopita katika siku kama ya leo, yaani tarehe 29 Januari 1942, baada ya majeshi ya Uingereza na Urusi kuivamia ardhi ya Iran na kukiuka msimamo wa Iran wa kutopendelea upande wowote katika Vita vya Pili vya Dunia, makubaliano baina ya pande hizo tatu yalisainiwa.
Kwa makubaliano hayo, serikali ya wakati huo ya Iran ililazimika kufungua njia na nyenzo za mawasiliano ya nchi kavu, angani na baharini kwa ajili ya kambi ya Waitifaki, yaani Allies katika vita hivyo, ili kwa kuitumia njia ya Iran kupitishia silaha na zana za kivita, iweze kuimarisha vikosi vyake vya upande wa Urusi dhidi ya Ujerumani ya Manazi.
Kwa upande wao, Urusi na Uingereza ziliyatambua mamlaka kamili ya kujitawala na umoja wa ardhi yote ya Iran na kuahidi kwamba, katika muda usiozidi miezi sita baada ya kumalizika vita, zitaondoa majeshi yao katika ardhi ya Iran. Lakini mbali na kuisababishia nchi hii hasara zisizofidika wakati yalipokuwepo majeshi yao, pale vita vilipomalizika, sio tu Urusi haikuwa tayari kuwaondoa askari wake, lakini pia ilijaribu kufanya kila mbinu kuunda serikali kibaraka kaskazini magharibi ya Iran kwa ajili ya kuandaa mazingira ya eneo hilo kujitenga.
Hata hivyo njama hiyo iligonga mwamba na jeshi la Urusi likalazimika kuondoka katika ardhi ya Iran.

Na miaka 45 iliyopita, yaani tarehe 29 Januari 1979, wakati wanazuoni mashuhuri wa Iran walipofanya mgomo wa kuketi ndani ya msikiti wa Chuo Kikuu cha Tehran kupinga na kulalamikia hatua ya utawala wa Shah kumzuia Imam Khomeni (MA) asiingie nchini, umati mkubwa wa wananchi ulimiminika mabarabarani kuelekea msikiti huko.
Katika miji mingine ya Iran pia waandamanaji waliokuwa wakitoa nara na kaulimbiu za “Allahu Akbar, Khomeini ni Kiongozi”, walitaka utawala wa kidikteta wa Shah uangushwe na Imam Khomeini arejee nchini.
Askari wa utawala wa Shah waliingilia kati tena kuwatawanya wananchi mjini Tehran ambapo katika makabiliano hayo, Waislamu wanamapambano wengi wa Iran waliuliwa shahidi na kujeruhiwa.
