Feb 06, 2024 02:55 UTC
  • Jumanne, tarehe 6 Februari, 2024

Leo ni Jumanne tarehe 25 Rajab 1445 Hijria, sawa na Februari 6 mwaka 2024.

Siku kama ya leo miaka 1262 iliyopita, Imam Musa Kadhim (as) mmoja wa wajukuu watoharifu wa Mtume Mtukufu (saw) aliuawa shahidi.

Imam Kadhim (as) alizaliwa mwaka 128 Hijiria huko katika eneo la Ab'waa lililoko baina ya miji mitakatifu ya Madina na Makka. Mtukufu huyo kwa miaka 20 alipata malezi na elimu muhimu kutoka kwa baba yake ambaye ni Imam Jaafar as-Swadiq (as). Baada ya kuuawa baba yake huyo, Imam Kadhim (as) alipata fursa ya kuuongoza Umma wa Kiislamu kwa muda wa miaka 35, ambapo alipata mateso na mashaka mengi katika njia hiyo. Katika zama zake ambazo zilisadifiana na ustawi mkubwa wa utamaduni na elimu ya Kiislamu pamoja na kuimarishwa uhusiano na mataifa ya kigeni, Imam alifanya juhudi kubwa za kueneza mafunzo ya Kiislamu katika mataifa hayo kupitia wanafunzi wake.

Mbali na hayo, Imam pia aliendesha mapambano makali dhidi ya watawala dhalimu wa Bani Abbas. Hatimaye Haroun ar-Rashid kutoka ukoo wa Bani Abbas aliyehofia sana kuporomoka kwa utawala wake, alimfunga jela Imam Kadhim (as). Licha ya kufungwa jela lakini Imam (as) hakusimamisha shughuli zake za kulingania dini na na mafundisho sahihi ya Uislamu.

Hatimaye Haroun Rashid alifanya njama ya kumuua Imam kwa kumpa sumu. Huku tukitoa mkono wa pole kwa Waislamu wote duniani kwa mnasaba huu mchungu wa kuuawa shahidi Imam Kadhim (as), tunakunukulieni hapa moja ya semi zake zenye mafunzo na busara kubwa. Imam anasema: 'Njia bora zaidi ya kumkurubia Mwenyezi Mungu baada ya kumjua ni kusimamisha swala, kuwatendea wema wazazi wawili na kuachana na husuda na majivuno.'   

Siku kama ya leo miaka 407 iliyopita alifariki dunia daktari na mtaalamu wa mimea wa Italia, Prospero Alpini.

Alizaliwa mwaka 1553 na baada ya kuhitimu masomo ya tiba alitunukiwa shahada ya udaktari. Katika uchunguzi na utafiti wake, Prospero Alpini aligundua kwamba, mimea kama walivyo wanyama, ina jinsia mbili za kike na kiume japokuwa hakuweza kujua kama kanuni hiyo inahusu kila kitu.

Miongoni mwa hatua nyingine muhimu za Prospero Alpini ni kuarifisha kahawa na ndizi kwa watu wa Ulaya. Biashara ya kahawa ya Mocha au al Mukha ambalo ni jina la bandari iliyoko kusini mwa Yemen, ilikuwa mikononi mwa Waislamu tangu karne ya 15, na mtaalamu huyo wa mimea wa Italia ndiye aliwajulisha watu wa Ulaya aina hiyo ya kahawa (Arabica) iliyokuwa ikioteshwa katika maeneo ya milimani nchini Yemen. 

Prospero Alpini

Siku kama ya leo miaka 102 iliyopita mkutano wa kimataifa wa kuzuia matumizi ya silaha za sumu ulimaliza kazi zake mjini Washington, Marekani kwa kutiwa saini mkataba uliopewa jina la mkataba wa pande tano kati ya nchi zilizoshiriki mkutano huo.

Nchi zilizotia saini mkataba huo ni Marekani, Ufaransa, Uingereza, Italia na Japan. Mkataba huo ulipiga marufuku utumiaji wa aina yoyote ya gesi za sumu na za kemikali katika vita. Miaka kadhaa baadaye nchi nyingine zilijiunga na mkataba huo wa kuzuia utumiaji wa gesi za sumu vitani.

Miaka 88 iliyopita mwafaka na tarehe 6 mwezi Februari mwaka 1936 eneo lenye baridi zaidi duniani lilitambuliwa na jopo moja la kielimu baada ya kufanya juhudi za miaka minne na hatimaye kugundua eneo hilo.

Kundi hilo la wataalamu hatimaye liligundua kuwa, mji wa Verkhoyansk huko Siberia, kaskazini mwa Russia, ndiyo eneo lenye baridi zaidi duniani baada ya kufanya utafiti wa muda mrefu. Mji wa Verkhoyansk ulikuwa ukitumika kama makazi ya uhamishoni ya wahalifu wa kisiasa wa Russia kabla ya kusambaratika Umoja wa Kisovieti.

Mji huo una jamii ndogo ya watu ambao kazi yao kuu ni biashara ya ngozi na kuchimba madini. Kiwango cha joto la eneo hilo majira ya baridi hufikia daraja 70 chini ya sifuri. 

Tarehe 6 Februari miaka 61 iliyopita aliaga dunia mwanaharakati mashuhuri na mpigania uhuru wa Morocco, Abd-el Karim Al-Khattabi.

lianzisha harakati za kupambana na wakoloni wa Kihispania na Kifaransa akiwa bado kijana na kuunda kundi la mapambano katika maeneo ya milimani nchini humo.

Ni vyema kukumbusha hapa kuwa wakati wa Vita vya Kwanza vya Dunia Uhispania ilifanya mauaji mengi ya halaiki huko Morocco kwa ajili ya kupanua mamlaka na ushawishi wake.

Baada ya Vita vya Kwanza vya Dunia na wakati wa kupamba moto mapambano ya wanamapinduzi wa Morocco, Ufaransa nayo ilifanya mauaji dhidi ya maelfu ya wananchi wa nchi hiyo.     

Abd-el Karim Al-Khattabi

Na siku kama hii ya leo miaka 45 iliyopita mamilioni ya wananchi Waislamu na wanamapinduzi wa Iran waliandamana katika miji mbalimbali hapa nchini baada ya kutangazwa serikali ya muda ya Mapinduzi.

Wananchi Waislamu wa Iran walifanya maandamano ili kuunga mkono uamuzi huo uliotolewa na Imam Khomeini Mwenyezi Mungu amrehemu.

Katika siku hiyo pia wananchi wa Iran na kwa sauti moja walitaka kuondoka madarakani serikali ya Bakhtiyar ambayo ilikuwa kibaraka wa madola ya kibeberu.

Siku hiyo pia Jenerali Robert Ernest Huyser, mjumbe maalumu wa Marekani aliyekuwa Tehran kwa ajili ya kusaidia juhudi za kuubakisha madarakani utawala wa Shah Pahlavi na kutangaza uungaji mkono wa Washington kwa makamanda wa jeshi la Shah, alifunga virago na kurejea Marekani baada ya kushindwa kusitisha wimbi la Mapinduzi ya Kiislamu.

Jenerali Robert Huyser