Feb 25, 2024 02:25 UTC
  • Jumapili, 25 Februari, 2024

Leo ni Jumapili 15 Shaaban 1445 Hijria sawa na 25 Februari 2024 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 1190 iliyopita alizaliwa Imam Mahdi (as) mwokozi wa ulimwengu katika mji wa Samarra Kaskazini mwa Baghdad mji mkuu wa Iraq. Yeye ni mwana mpendwa wa Imam Hassan Askari (as) ambaye ni mmoja wa wajukuu wa Mtume Muhammad (saw). Miongoni mwa lakabu mashuhuri za Imam huyo wa Zama ni Mahdi, ambayo ina maana ya mtu aliyepewa hidaya na kuongozwa, na al Qaim, kwa maana ya atakayeanzisha mapambano. Imam Mahdi alipitisha miaka mitano ya kwanza ya uhai wake akiwa na baba yake mpendwa, Imam Askari (as). Alichukua jukumu la kuongoza Umma wa Kiislamu kama Imam baada ya kuuawa shahidi baba yake mtukufu na kisha akatoweka na kwenda ghaiba kutokana na amri ya Mwenyezi Mungu. Kwa muda wa miaka 69 mtukufu huyo alikuwa akiwasiliana na kuwaongoza Waislamu kupitia wawakilishi wake maalumu. Baada ya hapo na kwa amri ya Mwenyezi Mungu, Imam Mahdi alienda kwenye ghaiba kubwa na ya muda mrefu na atadhihiri tena ulimwenguni wakati mwafaka ambao Mwenyezi Mungu ataona unafaa. Atakapodhihiri duniani, ataujaza ulimwengu kwa uadilifu na usawa baada ya kujaa dhulma na uonevu. Siku ya kuzaliwa mtukufu huyo huadhimishwa nchini Iran kama Siku ya Waliodhulumiwa Duniani. ***

 

Katika siku kama hii ya leo miaka 40 iliyopita ndege za kivita za utawala wa dikteta wa zamani wa Iraq, Saddam Hussein zilishambulia miji ya Saqz, Pol-e Dokhtar na Mahabad. Utawala wa Saddam Hussein uliamua kushambulia makazi ya raia katika miji mbalimbali ya Iran sambamba na ushindi mkubwa wa wapiganaji wa Kiislamu hususan katika operesheni ya jeshi la Iran iliyopewa jina la Khaibar na kipigo cha jeshi la Iraq katika visiwa vya Majnun. Makumi ya raia waliuawa na wengine wengi kujeruhiwa katika mashambulizi hayo. ***

 

Tarehe 25 Februari miaka 38 iliyopita dikteta wa zamani wa Ufilipino aliyekuwa amejitangaza rais wa maisha, Ferdinand Marcos, alikimbia nchi hiyo akiwa pamoja na familia yake. Marcos alichukua hatamu za uongozi mwaka 1965. Alidumisha utawala wake wa kidikteta na ukandamizaji nchini Ufilipino kwa himaya na uungaji mkono wa nchi za Magharibi hususan Marekani. Mwaka 1973 Ferdinand Marcos alijitangaza kuwa rais wa maisha wa Ufilipino. Wakati huo wananchi katika maeneo mbalimbali walikuwa tayari wameanzisha harakati za mapambano ya kisiasa na kijeshi dhidi ya dikteta huyo. Mapambano hayo yalishika kasi zaidi katikati ya mwongo wa 1980, na Februari 25 1986 Marcos alilazimika kukimbia Ufilipino.  ***

Ferdinand Marcos

 

Siku kama ya leo miaka 30 iliyopita Mzayuni mmoja aliyekuwa na misimamo ya kufurutu ada aliwashambulia na kuwamiminia risasi Waislamu waliokuwa wakitekeleza ibada ya Swala katika Msikiti wa Haram ya Nabii Ibrahim mjini al Khalil, Palestina inayokaliwa kwa mabavu na kuua shahidi 29 miongoni mwao. Mauaji hayo yalitokea wakati Waislamu hao walipokuwa katika ibada ya funga ya mwezi mtukufu wa Ramadhani. Waislamu wengine wengi walijeruhiwa katika shambulizi hilo la kikatili. Mauaji hayo ambayo yalidhihirisha tena uhasama na chuki za Wazayuni wa Israel dhidi ya Waislamu, yalilaaniwa na Waislamu kote duniani. Ukatili huo ulizusha wimbi kubwa la machafuko katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu za Palestina ambapo wananchi walizidisha mapambano dhidi ya maghasibu wa Tel Aviv. Israel ilimshika kwa muda na kumuachia huru mhalifu huyo katili kwa kisingizio kwamba alikuwa punguani! ***

Mji wa al-Khalil