Hikma za Nahjul Balagha (43)
Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum wasikilizaji wapenzi. Karibuni katika sehemu hii ya 43 ya mfululizo wa makala hizi fupifupi za Hikma za Nahjul Balagha. Leo pia tutaangalia kwa muhtasari hikma nyingine za Imam Ali bin Abi Talib AS kama ilivyonukuliwa kwenye kitabu cha Nahjul Balagha tukiwa na matumaini mtakuwa nasi hadi mwisho wa kipindi. Ingawa hii ni sehemu ya 43 ya mfululizo huu, lakini hikma tunayoendelea kuichambua ni ya 38.
وَأَکْبَرَ الْفَقْرِ الْحُمْقُ
Na upumbavu ndio umaskini mkubwa zaidi.
Wasikilizaji wapenzi, tunaendelea kuichambua hikma ya 38 ya Nahjul Balagha ambayo inahusiana na hazina nane zenye thamani kubwa zilizomo kwenye usia wa Imam Ali kwa mwanawe Imam Hasan al Mujtaba AS. Imam Ali AS anatufundisha sote hikma hii yenye vito vinane muhimu na vyenye thamani kubwa. Sehemu iliyopita ilihusu akili na hapa anasema: Na upumbavu ndio umaskini mkubwa zaidi.
Neno "ahmaq" ambalo lina maana ya mpumbavu, zuzu na juha yaani mtu asiyetumia vizuri akili yake, hata akieleweshwa hataki kuelewa, zumburukuku asiyejua maana hata akielimishwa. Hili neno "ahmaq" linatumiwa kwa mtu ambaye maneno yake huitangulia akili yake. Kwa maana ya kwamba, hafikiri kabla ya kusema. Haiulizi akili yake kwamba je alichoamua kusema ni sawa au si sawa. Tab'an inabidi ifahamike hapa kwamba maana ya “watu wapumbavu” katika hikma hii si watu waliozaliwa na akili ndogo bali maana yake ni kama tulivyosema, ni watu wapuuzi, majuha na mazuzu mazumburukuku ambao hata kama huenda katika baadhi ya mambo wakaonekana kuwa na akili kubwa za kile kinachoitwa wasomi na maprofesa, lakini katika baadhi ya mambo hasa ya imani na itikadi za kidini wanakuwa mazuzu na majuha ambao wanakubali imani za kipumbavu na kuacha kuzitumia vyema akili zao kufuata mambo ya haki. Imam Ali hapa anawazungumzia watu wapumbavu wa aina hiyo kwamba ndio maskini zaidi kuliko mtu mwingine yoyote hata kama wataonekana kidhahiri kuwa na utajiri mkubwa, ushawishi na vyeo vikubwa katika jamii zao.
Kimsingi mtu ahmaq na mpumbavu, hupoteza dunia na Akhera yake! Mtu zuzu hufadhilisha raha za kupumbaza za duniani na kuhatarisha manufaa makubwa ya Akhera kwa ladha za kizumburukuku na za muda mfupi sana za hapa ulimwengu. Ni wazi kuwa mtu wa namna hiyo hatokuwa na chochote huko Akhera na hapa duniani pia hupoteza kiurahisi marafiki wazuri na wa maana kutokana na ujuha wake na anashindwa kuwa na tadibiri ya kutosha ya kuamiliana ipasavyo mambo yake hapa ulimwenguni. Siku zote huishi na hofu na jambo dogo kwake huwa kubwa, na hiyo ni adhabu isiyo na kifani anayojisababishia kwa sababu ya upumbavu na uahmaki wake.
Katika moja ya nasaha za Imam Sajjad AS wakati mwanawe yaani Imam Muhammad Baqir AS alipokuwa ameazimia kwenda katika moja ya safari zake, alimuuzia mwanawe huyo akimwambia: Mwanangu, epuka kufanya urafiki na zuzu na mpumbavu na kaa mbali naye na epuka kufanya mijadala na mazungumzo naye. Kisha, katika kueleza viwango vya kutoona mbali na ufinyu wa mawazo wa watu mazuzu na majuha, Imam Sajjad AS alisema: Mpumbavu akinena, upumbavu wake na uzuzu wake humfedhehesha, akinyamaza mapungufu na udhalili wake hudhihirika kwa matendo yake. Akipewa siri humfedhehesha aliyempa siri na ujuzi wake haumfaidishi elimu ya wengine haimnufaishi. Hamsikilizi anayempa ushauri na hamwachi salama rafiki yake. Jirani yake anatamani kuwa mbali na nyumba yake na anayeketi karibu naye huogopa kusema chochote kwa kuhofia nafsi yake. Mtu ahmaki na mpumbavu anaposhiriki katika mikutano ya watu wengine, ikiwa watu waliopo kwenye mkutano ni wakubwa kuliko yeye, atawalemaza kwa upumbavu wake na ikiwa ni wadogo kuliko yeye, atapotoa kwa tabia zake ya kijuha na kipumbavu.
Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.