Mar 01, 2024 06:19 UTC
  • Hikma za Nahjul Balagha (45)

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum wasikilizaji wapenzi. Karibuni katika sehemu hii ya 45 ya mfululizo wa makala hizi fupifupi za Hikma za Nahjul Balagha. Leo pia tutaangalia kwa muhtasari hikma nyingine za Imam Ali bin Abi Talib AS kama ilivyonukuliwa kwenye kitabu cha Nahjul Balagha tukiwa na matumaini mtakuwa nasi hadi mwisho wa kipindi. Ingawa hii ni sehemu ya 45 ya mfululizo huu, lakini hikma tunayoendelea kuichambua ni ya 38.

وَأَکْرَمَ الْحَسَبِ حُسْنُ الْخُلُقِ

Na hadhi bora kabisa ya mtu ni maadili yake.

Katika hikma ya 38 ya kitabu cha Nahjul Balagha, Imam Ali AS anatupa hazina nane zenye thamani kubwa sana kwa kutumia maneno machache yenye balagha la ya hali ya juu. Leo tutaendelea kuichambua hikma hiyo ambapo hapa Imam anasema: Wa-akramal Hasabi, Husnul Khulqi, na hadhi bora kabisa ya mtu ni maadili yake mema. 

Neno hasab maana yake ni heshima na sharafu katika ukoo wa ubabani na umamani mwa mtu ambayo inamfanya mtu ajifakharishe nayo. Kwa hiyo, inaonekana maana aliyokusudia kuibanisha hapa Imam Ali AS katika hikma yake hii hii ni kwamba jambo la juu kabisa ambalo mtu anapaswa kujifakharisha nalo, heshima na sharafu ya kweli waliyojipamba nayo mababu na mabibi zake kupitia khulqa na tabia njema. Kwa maneno mengine ni kwamba; maadili ndiyo huamua heshima na sharafu ya mtu. Maadili yanayopendeza zaidi ni ya tabia njema ambazo hunyanyua jina na hadhi ya mtu milele na milele. Ni kama alivyosema Imam Ali AS katika hotuba nyingine yenye busara kubwa: "لَا قَرِینَ کَحُسْنِ الْخُلُقِ: Hakuna chochote cha kulandana cha na akhlaki njema." Yaani hakuna kitu chochote kinachoweza kuwa daraja sawa na tabia na maadili mema. Kwa sababu maadili mema na akhlaqi bora ni kitu cha asili na cha dhati ya ndani ya nafsi ya mtu, muda wote huwa pamoja naye kumsaidia na kumuokoa kwenye mambo mengi. 

Maadili mema ni katika sifa bora na nzuri katika milahaka na maingiliano ya watu kwenye jamii. Huvutia mapenzi na ushawishi kwa watu wengine na huathiri pia kwenye maneno na matamshi ya mtu. Ni kwa sababu hiyio ndio maana Mwenyezi Mungu Mtukufu amewaumba Mitume na manabii wake kwa sifa za ukamilifu wa kibinadamu kwenye maadili mema na kuwafanya kuwa vigezo vya milele kwa wanadamu wengine. Qur'ani Tukufu imemsifu hivyo pia Bwana Mtume Muhammad SAW kwamba yeye ni mja mtukufu ambaye yuko juu ya khulka njema na adhimu. Au katik aaya ya 159 ya sura ya tatu ya Aal Imran, Mwenyezi Mungu anasema: Basi ni kwa sababu ya rehema itokayo kwa Mwenyezi Mungu ndio umekuwa laini kwao. Na lau ungeli kuwa mkali, mwenye moyo mgumu, bila ya shaka wangelikukimbia. Aidha kumepokewa hadithi kutokwa kwa Bwana Mtume Muhammad SAW ambaye amesema: Maadili mema huimarisha mapenzi ya waja. 

Imesemwa katika riwaya kwamba, Imam Ali AS aliamrishwa na Mtume SAW kupigana na watu watatu waliokula njama za kumuua. Imam alimuua mmoja wa wale watu watatu na akawakamata wengine wawili na kuwapeleka mbele ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (SAW). Mtume aliwalingania Uislamu lakini walikataa katakata. Mtume alitoa amri ya kutekelezwa kisasi cha kuuawa kutokana na kushiriki katika njama za mauaji na kutokana na kuthibiti kwao kosa la muhaarib. Lakini hapo hapo Malaika Jibril AS alimshukia Mtume SAW na kumwambia: Mwenyezi Mungu Mtukufu anakuamrisha umsamehe mmoja wa watu hawa wawili, kutokana na maadili yake mema na ukarimu wake. Mtume alitii amri hiyo ya Mwenyezi Mungu na kuacha kutekeleza adhabu ya kifo kwa mtu huyo kutokana na maadili, ukaribu na tabia zake njema. Mtu yule hapo hapo alitamka shahada mbili na akawa Muislamu. Mtu akasema mtu huyo ameongozwa kwenye njia ya pepo kutokana na maadili na tabia zake njema.

Tags