Hikma za Nahjul Balagha (44)
Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum wasikilizaji wapenzi. Karibuni katika sehemu hii ya 44 ya mfululizo wa makala hizi fupifupi za Hikma za Nahjul Balagha. Leo pia tutaangalia kwa muhtasari sehemu nyingine ya hikma za Imam Ali bin Abi Talib AS kama zilivyonukuliwa kwenye kitabu cha Nahjul Balagha tukiwa na matumaini mtakuwa nasi hadi mwisho wa kipindi. Ingawa hii ni sehemu ya 44 ya mfululizo huu, lakini hikma tunayoichambua ni ya 38.
وَأَوْحَشَ الْوَحْشَةِ الْعُجْبُ
Upweke wa kutisha zaidi ni wa majivuno.
Wasikilizaji wapenzi tunaendelea na kutoa uchambuzi kuhusu hikma ya 38 ya Nahjul Balagha. Kama ambavyo tumekuwa tukirudia mara kwa mara kwamba katika hikma hii, Imam Ali bin Abi Talib AS anatupa johari na hazina nane zenye thamani kubwa ndani ya maneno machache yenye maana pana na yaliyojaa hikma na busara. Baada ya kuzungumzia thamani za akili na ubaya wa uzuzu na upumbavu, hapa sasa Imam anazungumzia majivuno na ubinafsi akisema: Upweke wa kutisha zaidi ni wa majivuno.
Ghururi na majivuno ni miongoni mwa tabia mbaya sana katika maisha ya mtu binafsi na ya kijamii hasa katika imani na maadili. Mtu mwenye kiburi na kujiona bora kuliko wengine, haoni kuwa anastahiki kuzungumza kwa heshima na watu wengine na kuwatendea vile wanavyostahiki kutendewa bali muda wote hujiweka daraja ya juu zaidi kuliko wengine. Matokeo yake ni kwamba mtu huyo hupoteza marafiki, kwa sababu hakuna mtu aliye tayari kushirikiana na mtu huyo mwenye ubinafsi na majivuno, na hivyo anabaki peke yake na kutawaliwa na upweke katika maisha yake.
Ubinafsi na ghururi humfanya mtu asiendelee kupevuka. Madhali hatoachana na majivuno, mtu huyo hatoweza kamwe kufikia ukamilifu wake wa kibinadamu. Imenukuliwa katika kisa kimoja kwamba siku moja mtu mmoja aliyekuwa amepanda farasi, alifika kwenye ufukwe wa maji kwa ajili ya kuvuka na kwenda ng’ambo ya pili. Lakini kadiri alivyojitahidi kumlazimisha farasi wake avuke, farasi alikataa katakata. Akaja mtu mwenye busara na kusema: Yakoroge maji ya hiki kijito yawe tope. Baada ya kufanya kama alivyoelekezwa na yule mtu mwenye hikma, farasi alivuka kwa urahisi kabisa. Yule bwana alipoulizwa kuhusu wapi amekuja na fikra ile alisema: Maji yalipokuwa safi, farasi aliona sura na mwili wake ndani ya maji na aliona kwamba kama ataweka mguu wake, atakuwa anajikanyaga mwenyewe hivyo hakuwa tayari kujikanyaga, lakini mara tu baada ya maji yalipochafuliwa, amesahau sura yake ndani ya maji yale na amepita kirahisi.
Ghururi na majivuno humnyima mtu fursa na nguvu za kuona mambo katika uhalisia wake na humjengea hali ya kughururisha inayomfanya afikiri kuwa mambo yote yapo chini ya udhibiti wake. Hujiona kuwa yeye peke yake ndiye mwenye ufanisi katika matendo yake.
Imesimuliwa pia kwamba, mtu mmoja alikuwa safirini na Nabii Isa AS. Walipofika kwenye ufukwe wa bahari, Nabii Isa AS alisema “Basmillah” kwa yakini ya moyo wake na akaanza kutembea juu ya maji kana kwamba anatembea juu ya ardhi. Yule mtu alipomuona Masih Isa yaani Yesu AS anatembea juu ya maji, naye pia alisema Bismillah yaani Kwa jina la Allah kwa Yakini ya moyo wake. Yeye pia alikanyaga juu ya maji na akaanza kutembea kama yuko nchi kavu, sawa kabisa na alivyofanya Nabii Isa AS.
Baada ya kuona na yeye ameweza kutembea juu ya maji kama Nabii Isa AS ghururi ilimpitikia moyoni na kusema, Nabii Isa ni neno la Mungu na anaweza kutembea kiurahisi hivi juu ya maji, lakini na mimi pia naweza kutembea juu ya maji. Alipofikiri hiyo tu maji yalimgharikisha na akaanza kuomba msaada kutoka kwa Nabii Isa AS. Nabii Isa alimuokoa na kumuuliza imekuwaje. Yule mtu alisema: Nilijiambia moyoni, wewe ni neno la Mungu unatembea juu ya maji, lakini na mimi pia naweza kutembea juu ya maji. Mungu hakucherewa kunishushia adhabu Yake. Nabii Isa AS alimwambia: Majivuno na kiburi chako kimekufanya ujiweke daraja ambayo si yako. Hukupaswa kufanya hivyo. Tubu kwa Mola wako. Yule mja mtiifu alitubu na Mwenyezi Mungu akamrejesha kwenye daraja anayostahiki ambayo alikuwa amemuweka.