Apr 12, 2024 03:29 UTC
  • Ijumaa, 12 Aprili, 2024

Leo ni Ijumaa tarehe 3 Shawwal 1445 Hijria sawa na tarehe 12 Aprili 2024.

Siku kama ya leo miaka 204 iliyopita sawa na tarehe 12 Aprili 1820, dawa ya kutibu ugonjwa wa malaria iligundulika kutoka kwenye magamba ya mti wa Cinchona.

Asili ya mti huu wenye majani ya kijani kibichi ni maeneo ya Amerika ya Kusini lakini hii leo unapandwa katika ameneo mengine ya dunia. Utomvu wa mti huu hutumika kutengeneza dawa chungu sana ya Quinine.

Tarehe 12 Aprili mwaka 1820 kwa mara ya kwanza kabisa madaktari Pierre Joseph Pelletier na Joseph Bienaimé Caventou wa Ufaransa walifanyia majaribio dawa hiyo ya malaria katika Maabara ya Paris na kukaanza jitihada za kuzalisha dawa ya Quinine. 

Siku kama ya leo miaka 201 iliyopita, sawa na tarehe 12 Aprili 1823, alizaliwa Alexandr Ostrovsky mwandishi wa tamthilia wa nchini Russia.

Alihitimu masomo ya sheria katika chuo kikuu ingawa aliamua kujiunga na tasnia ya uandishi wa tamthilia na uigizaji. Karibu kila mwaka Alexandr Ostrovsky alikuwa akifanya uigizaji wa kihistoria au kuandika vichekesho ambapo alikuwa akiakisi hali halisi ya jamii. Alikuwa na taathira kubwa katika senema ya Russia. Miongoni mwa athari za mwanasanaa huyo ni pamoja na 'Binti wa Barafu', 'Msitu' 'Tufani' na 'Muhanga Mwingine.' Mwandishi huyo alifariki dunia mwaka 1886.   

Alexandr Ostrovsky

Siku kama ya leo miaka 157 iliyopita, sawa na tarehe 12 Aprili 1867, Mutsuhito, mfalme maarufu na mwanamageuzi wa Japan aliingia madarakani nchini humo.

Mfalme huyo aliingia madarakani wakati ambapo Japan ilikuwa inakabiliwa na changamoto nyingi za udhaifu katika nyuga tofauti. Ni kwa ajili hiyo ndio maana Mutsuhito baada ya mwaka mmoja kuingia madarakani akabuni mapinduzi ya kijamii na kuanzisha mageuzi nchini Japan. Katika uwanja huo alihamisha mji mkuu kutoka Kyoto kwenya Tokyo sambamba na kubadili katiba ya nchi hiyo.

Hata kama utawala wa Mutsuhito ulifikia tamati mwaka 1912, lakini Japan iliweza kupata maendeleo licha ya kuliibuka vita baina yake na China na Russia.   

Mutsuhito

Tarehe 12 Aprili miaka 63 iliyopita, kwa mara ya kwanza mwanadamu alifika katika anga za mbali na kuizunguka dunia.

Siku hiyo Yuri Gagarin mwanaanga wa Urusi ya zamani aliyekuwa na umri wa miaka 27 aliizunguka dunia kwa dakika 89 kwa kutumia chombo cha anga za mbali kwa jina la Vastok 1 na kwa msingi huo kukapatikana mafanikio makubwa katika sekta ya masuala ya anga.

Gagarin alifariki dunia akiwa pamoja na mmoja wa viongozi wa ngazi za juu wa sekta ya masuala ya anga wa Urusi ya zamani katika ajali ya ndege hapo mwaka 1968.   

Yuri Gagarin

Siku kama ya leo miaka 38 iliyopita kulingana na kalenda ya Hijria Shamsia, alifariki dunia msomi mkubwa wa Kiislamu, Ayatullah Mujtaba Hatami Lankarani. Ayatullah Lankarani alizaliwa katika mji wa Isfahan hapa nchini Iran na katika kipindi cha ujanani alielekea katika mji wa Najaf huko Iraq kwa ajili ya kupata masomo. Akiwa huko Najaf, Ayatullah Mujtaba Hatami Lankarani aliweza kusoma chini ya maulama wakubwa wa zama zake kama vile Dhiyaudin Iraqi, Ayatullah Mirzai Naayini na Sayyid Abul-Hassan Isfahani. Baada ya kumaliza masomo yake na kufikia daraja ya juu ya elimu alirudi katika mji alikozaliwa wa Isfahan na kutumia umri wake wote katika kutoa mafunzo ya dini tukufu ya Kiislamu. Ayatullah Lankarani alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 75.

Ayatullah Mujtaba Hatami Lankarani

Na katika siku kama ya leo miaka 16 iliyopita, wananchi kadhaa wa Iran waliuawa shahidi kufuatia shambulio la kigaidi na utegaji bomu. Bomu hilo lilitegwa katika Husseiniya ya Shuhadaa katika mji wa Shiraz. Jinai hiyo ilifanyika kwa uongozi na usimamizi wa mashirika ya kijasusi ya kigeni. Baadhi ya watekelezaji wa shambulio hilo la bomu walitiwa mbaroni katika moja ya hoteli za Tehran ambapo baada ya kufunguliwa mashtaka walilipwa ujira wa amali yao hiyo.

 

Tags