Apr 19, 2024 23:11 UTC
  • Jumamosi, Aprili 20, 2024

Jumamosi tarehe 11 Mfunguo Mosi Shawwal 1445 Hijria inayosadifiana na tarehe 20 Aprili 2024 Milaadia.

Siku kama ya leo miaka 1448 iliyopita, Mtume Muhammad (saw) alikwenda eneo la “Taif” kwa ajili ya kueneza dini ya Uislamu. Safari ya hiyo na kulingania dini katika eneo la Taif, karibu na Makka, ilifanyika muda mfupii baada ya kuaga dunia Abu Twalib aliyekuwa msaidizi mkuu na mlinzi wa Mtume, na kwa sababu hii, waabudu masanamu wa Kiquraishi walikuwa wamezidisha mateso yao dhidi ya mtukufu huyo na masahaba zake.

Kwa msingi huo, kama watu wa Taif wangesilimu, mji huu ungekuwa kituo na mahali salama kwa Waislamu waliokuwa wakikandamizwa na kudhulumwia huko Makka. Hata hivyo viongozi wa kabila la Thaqif huko Taif, sio tu kwamba hawakumwamini Mungu Mmoja na Mtume wake, Muhammad (SAW), bali pia waliwachochea baadhi ya wajinga waliomuudhi  Mtume (saw) na kumjeruhi.

Siku kama ya leo tarehe 20 Aprili miaka 222 iliyopita Mawahabi wa Hijaz (Saudi Arabia) walishambulia mji mtakatifu wa Karbala nchini Iraq na kuua mamia ya Waislamu wa madhehebu ya Shia.

Baada ya mawahabi kushika hatamu za uongozi huko Hijaz mwanzoni mwa karne ya 19 walianzisha mashambulizi ya mara kwa mara ya kundi hilo lenye misimamo na fikra za kuchupa mipaka dhidi ya Waislamu wengine hususan wafuasi wa Watu wa Nyumba ya Mtume wetu Muhammad (saw) na miongoni mwa mashambulizi ya mawahabi hao ni yale ya kushambulia miji mitakatifu ya Karbala na Najaf nchini Iraq tarehe 20 Aprili mwaka 1802. Miji hiyo ambayo ni mitakatifu hususan kwa Waislamu wa madhehebu ya Shia kutokana na kuwa na makaburi ya watu wa kizazi cha Mtume wetu Muhammad (saw), imekuwa ikilengwa na mawahabi.

Katika mashambulizi hayo mawahabi walishambulia haram ya mjukuu wa Mtume, Imam Hussein bin Ali mwana wa Bibi Fatima (as) huko Karbala na kuvunja quba na kaburi na mtukufu huyo na kisha wakapora mali iliyokuwa hapo. Waislamu zaidi ya elfu mbili waliuawa katika shambulizi hilo la mawahabi. Mashambulizi hayo yaliwakasirisha sana Waislamu katika maeneo mbalimbali ya dunia na kuzidisha chuki yao dhidi ya mawahabi na mafundisho ya kundi hilo potofu. Mawahabi waliendeleza mauaji ya Waislamu wa madhehebu ya Shia na madhehebu nyinginezo baada ya kuanzishwa dola la watawala  wa kizazi cha Aal Saud huko Saudi Arabia na walishambulia na kuharibu Haram ya wajukuu wa Mtume Muhammad (saw) na za masahaba zake wakubwa katika makaburi ya Baqii mjini Madina.

Haram ya mjukuu wa Mtume, Imam Hussein na Abul Fadhl (as), Karbala

Miaka 25 iliyopita, katika siku kama ya leo, kulitokea maafa makubwa ya mashambulizi yaliyofanywa na wanafunzi wawili wa Kimarekani kwenye shule moja ya sekondari.

Wanafunzi hao waliwamiminia risasi na kuwaua wanafunzi wenzao 12 na mwalimu wao na kuwajeruhi wengine 21. Wanafunzi hao waliovamia shule ya Columbine High School iliyoko Denver, katika jimbo la Colorado, walijiua wenyewe baada ya kufanya mauaji hayo.

Mauaji kama hayo ya kutisha yamekuwa yakitokea mara kwa mara katika maeneo ya umma nchini Marekani. Wataalamu wanasema kuuwa, uhuru wa kununua na kumiliki silaha ni miongoni mwa sababu za maafa hayo yanayotokea kila mwaka nchini Marekani. 

Mauajii ya Shule ya Sekondarii ya Columbine  

Katika siku kama ya leo tarehe 20 Aprili miaka 14 iliyopita, mlipuko uliotokea kwenye mtambo wa kuchimba mafuta wa Deepwater Horizon na kuzamisha mtambo huo mali ya Shirika la Mafuta la Uingereza (British Petroleum) kulikosababisha kuvuja mafuta katika Ghuba ya Mexico.

Wafanyakazi 11 wa mtambo huo waliuawa na mafuta mengi yaliyokuwa yakivuja kutoka katika kisima hicho yalisababisha uchafuzi mkubwa wa mazingira kuwahi kutokea katika karne moja ya hivi karibuni huko Marekani.  **