Apr 21, 2024 13:56 UTC
  • Hikma za Nahjul Balagha (47)

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum wasikilizaji wapenzi. Karibuni katika sehemu hii ya 47 ya mfululizo wa makala hizi fupifupi za Hikma za Nahjul Balagha. Leo pia tutaangalia kwa muhtasari hikma nyingine za Imam Ali bin Abi Talib AS kama ilivyonukuliwa kwenye kitabu cha Nahjul Balagha tukiwa na matumaini mtakuwa nasi hadi mwisho wa kipindi. Ingawa hii ni sehemu ya 47 ya mfululizo huu, lakini hikma tunayoichambua ni ya 39.

لَا قُرْبَةَ بِالنَّوَافِلِ، إِذَا أَضَرَّتْ بِالْفَرَائِضِ

Hakuna kujikurubisha kwa suna, kama zitadhuru faradhi.

Naam, katika hikma hii ya 39, Imam Ali AS anatufundisha jambo jingine muhimu na la dharura sana akisema, "Hakuna kujikurubisha kwa Allah kwa kufanya mambo ya sunna ambayo yanadhuru mambo ya faradhi na ya wajibu kwa mtu. 

Uislamu wa mtu hukamilika pale mtu huyo anapochunga na kuheshimu mafundisho yote ya dini Tukufu ya Kiislamu na kuyatekeleza kivitendo na kwa njia sahihi. Tab'an, jambo la chini kabisa ambalo Uislamu umelitaka kwa Waislamu walitekeleze ni kuchunga mambo ya wajibu na kuacha mambo ya haramu. Mambo ya wajibu ni yale ambayo Mwenyezi Mungu ameyafaradhisha na humlipa mja Wake thawabu anapoyafanya na amemuandalia adhabu kwa kutoyafanya. Amma neno "Mustahab" maana yake halisi ni kitu cha kupendeza kinachohimizwa kufanywa lakini si wajibu. Wanachuoni wa fiqhi wanasema kuwa, hayo ni matendo mengi zaidi mazuri ambayo Waislamu wanahimizwa na kuraghibishwa wayatende. Wakiyatenda hupata thawabu, lakini wasipoyatenda hawapati madhambi na wala Allah hatowaadhibu kwa hilo.

Vitendo vya mustahabu ni katika njia na vielelezo vya kujikurubisha kwa Mwenyezi Mungu. Lakini kama tulivyosema, iwapo mtu hatovitenda, hatoadhibiwa na Muumba. Kwa hiyo, lililo muhimu na ambalo ni wajibu litangulizwe mbele ya jingine, ni lile jambo la faradhi na si mustahabu na sunna. Tab'an inavyotakiwa hasa ni mtu kujipanga vizuri na kuhakikisha anatekeleza vilivyo yote mawili, mambo ya faradhi na mambo ya sunna na akifanya hivyo bila ya shaka yoyote atapata ujira mkubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Lakini ikiwa haiwezekani kufanya yote mawili, anachopaswa kukitanguliza mtu ni jambo la wajibu mbele ya la mustahabu.  Kwa mfano, itakapotokezea wakati wa Sala ya faradhi kuwa dhiki, mtu hapaswi kusali kwanza sunna na kuja kuisali Sala ya faradhi nje ya wakati wake. Vile vile kama mtu ana deni, anachopaswa ni kuhakikisha analipa kwanza deni lake ndipo aende kwenye mambo ya sadaka na kuwasaidia masikini. Sababu ya jambo hilo iko wazi na haihitaji hata kushereheshwa kwani, iwapo utaacha faradhi, utaadhibiwa, lakini unapoacha sunna hutoadhibiwa na Muumba. 

Tunachopaswa kukitilia maanani zaidi hapa ni kwamba, Imam anasema, iwapo jambo la sunna litaleta madhara kwa jambo la wajibu, naam, iwapo litaleta madhara, basi sunna hiyo haina maana na hakuna ukaribu wowote kwa Allah iwapo mtu ataacha alilowajibishwa na kufanya lisilowajibishwa. Katika sehemu nyingine Imam Ali AS amenukuliwa akisema:

إنّک إنِ اشتَغَلتَ بفَضائلِ النَّوافِلِ عَن أداءِ الفَرائضِ، فلَن یَقومَ فَضلٌ تَکسِبُهُ بِفَرضٍ تُضَیِّعُهُ

"Iwapo utakaa na kujishughulisha tu thawabu za sunna na ukaacha kutekeleza ya faradhi, thawabu unazozipata kwenye sunna hazitofidia faradhi ulizozipoteza.

Ni kwa kuzingatia umuhimu mkubwa wa jambo hilo pia ndio maana Bwana Mtume Muhammad SAW akahimiza sana kwa kusema, mcha Mungu mkubwa zaidi ni yule anayetekeleza vizuri mambo ya faradhi. Amenukuliwa akisema:

اِعمَلْ بفَرائضِ اللَّهِ تَکُن أتقَى الناسِ

Tekeleza faradhi za Allah, utakuwa mcha Mungu mkubwa kuliko wote.

Naye Imam Sajjad, Ali bnil Husain, Zaynul Abidin AS anasema: 

مَن عَمِلَ بما افتَرَضَ اللَّهُ علَیهِ فهُو مِن خَیرِ الناسِ

Mtu bora zaidi ni yule anayetekeleza aliyofaradhishiwa na Allah.

Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.

Tags