Jumatano, tarehe 22 Mei, 2024
Leo ni Jumatano tarehe 13 Mfunguo Pili Dhulqaada 1445 Hijria sawa na Mei 22 mwaka 2024.
Siku kama ya leo miaka 165 iliyopita, alizaliwa Arthur Conan Doyle mwandishi wa Scotland.
Awali Doyle alisomea elimu ya tiba, hata hivyo kutokana na kwamba hakufaulu katika uga huo ndipo akaamua kujiunga na taaluma ya uandishi. Licha ya kwamba Doyle aliandika visa vingi lakini kilichompa umashuhuri ni majmui ya visa vya polisi vilivyoitwa Sherlock Holmes. Arthur Conan Doyle alifariki dunia mwaka 1930. **
Siku kama ya leo miaka 139 iliyopita aliaga dunia Victor Hugo mwandishi na malenga mashuhuri wa Kifaransa akiwa na umri wa miaka 83. Hugo alikuwa muungaji mkono mkuu wa mabadiliko kwa maslahi ya matabaka ya wanyonge na masikini nchini humo.
Victor Hugo alijitosa kwenye uwanja wa kisiasa akiwa na umri wa miaka 25 na kufanikiwa kuchaguliwa kuwa mbunge. Lakini ulipofika wakati wa utawala wa Napoleon wa Tatu alijiengua kwenye uwanja huo na kubaidishwa kwa muda wa miaka 20 baada ya kupinga siasa za dikteta Napoleon wa Tatu.
Miongoni mwa kazi maarufu za mwandishi huyu wa Kifaransa, tunaweza kutaja riwaya "Les Miserables", "Hunchback of Notre Dame", "The Man Who Laughs" na "Workers of the Sea". ****
Siku kama ya leo miaka 112 iliyopita yaani mwaka 1912 alizaliwa Herbert Charles Brown mwanakemia wa Uingereza.
Brown alizaliwa mwaka 1912 mjini London na familia yake ikahamia Marekani kabla ya hata kutimiza miaka miwili. Alijiunga na chuo kikuu cha Chicago mwaka 1935 na kusomea kozi ya Kemia na kuendelea na masomo hadi alipofanikiwa kuwa mhazili wa chuo kikuu. Mwaka 1979 alitunukiwa tunzo ya Nobel katika taaluma ya kemia kutokana na jitihada alizofanya katika ugunduzi wa michanganyiko mipya ya kemia kaboni au Organic Chemistry. Herbert Charles Brown alifariki dunia mwaka 2004. ***
Siku kama hii ya leo miaka 38 iliyopita Omar Tilmisani mmoja wa viongozi wa Harakati ya Ikhwanul Muslimin ya Misri aliaga dunia.
Alizaliwa mwaka 1904 katika eneo la Tilmisan nchini Algeria. Tilmisani alihitimu masomo yake ya shahada katika taaluma ya sheria na mwaka 1928 akawa mwanachama wa Ikhwanul Muslimin baada ya kuasisiwa harakati hiyo. Tilmisani ambaye alimpita kwa miaka miwili Hassan al Banna kiongozi wa harakati hiyo anahesabiwa kuwa mmoja wa makada wakongwe wa harakati hiyo. Hatimaye Omar Tilmisani aliaga dunia tarehe 22 Mei 1986 akiwa na umri wa miaka 82 baada ya kupatwa na maradhi ya ini na figo.