Jun 23, 2024 02:43 UTC
  • Jumapili, 23 Juni, 2024

Leo nii Jumapili 16 Mfunguo Tatu Dhul-Hiija 1445 Hijria sawa na 23 Juni 2024 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 1104 iliyopita lilindwa bunge la kwanza dunia huko Island. Bunge hilo ambalo wawakilishi wake walikuwa wakichaguliwa na wananchi kupitia masanduku ya kura, lilikuwa na kazi ya kuisaidia serikali kifikra. Bunge la zamani zaidi duniani baada ya lile la Iceland, lilianza kazi zake nchini Uingereza katikati ya karne ya 13. 

Katika siku ya leo miaka 488 iliyopita, ilianza harakati ya kiongozi wa kidini na mpenda mageuzi wa Ufaransa, Calvin John, huko Geneva mji mkuu wa Uswisi. Alizaliwa mwaka 1509 na kujifunza sheria na masomo ya kidini. Katika zama za ujana wake, Calvin John alijiunga na harakati ya Kiprotestanti ilioasisiwa na Martin Luther. Aliivamia Geneva, Uswisi kwa kusaidiwa na wafuasi wa Kiprotestanti na kujaribu kuasisi mfumo wa uongozi wa kidini katika jamii ya nchi hiyo kwa mujibu wa dhehebu la Protestanti. Calvin John pia alianzisha mfumo wa ideolojia ya Kikristo iliyojulikana kama Calvinism na kubainisha itikadi zake katika kitabu chake alichokiita" Institutes of Christian Religion."  ***

 

Miaka 268 iliyopita katika siku muwafaka na leo, vilijiri vita vya kwanza kati ya vikosi vya Uingereza na India huko katika eneo la Bengali, Kaskazini Mashariki mwa India. Waingereza walishinda vita hivyo na kulidhibiti eneo hilo ambalo katika zama hizo lilikuwa sehemu ya ardhi ya India. Waingereza ambao walianza kuingia nchini India miaka kadhaa nyuma kupitia East Indian Company, mbali na kuyarejesha nyuma majeshi ya India, katika vita vilivyofuata walimshinda pia hasimu wao mkubwa Ufaransa na kufanikiwa kuyatoa kabisa majeshi hayo katika ardhi ya India.  ***

 

Tarehe 23 Juni miaka 85 iliyopita, Wafaransa waliikabidhi Uturuki bandari muhimu ya Iskenderun, eneo ambalo katika zama hizo lilikuwa sehemu ya ardhi ya Syria. Kwa miaka kadhaa kabla ya tukio hilo, Uturuki ilikuwa ikidai umiliki wa bandari hiyo. Baada ya Vita vya Kwanza vya Dunia, eneo hilo lilikabidhiwa Syria kwa mujibu wa makubaliano yaliyokuwa yamefikiwa baina ya Uingereza na Ufaransa. Hata hivyo baada ya kuangushwa utawala wa Othmania na kuchukua hatamu za uongozi nchini Uturuki Mustafa Kamal Ataturk aliyekuwa na mielekeo ya Kimagharibi, Ufaransa ambayo wakati huo ilikuwa ikiikalia kwa mabavu Syria, iliikabidhi Bandari ya Iskenderun kwa Uturuki. Hatua hiyo ilipelekea kuongezeka hisia za chuki dhidi ya Ufaransa nchini Syria na kuzidisha mapambano dhidi ya mkoloni huyo. Hadi leo hii serikali ya Syria ingali inasisitiza kwamba, Bandari ya Iskenderun ni mali yake. ***

Bandari ya Iskenderun,

 

Siku kama ya leo miaka 13 iliyopita aliaga dunia qari mkubwa wa Qur'ani wa Misri, Abul Ainain Shu'aisha. Alizaliwa mwaka 1922 katika mji wa Bila mkoa wa Kafr El-Shaikh na akafanikiwa kuhifadhi Qur'ani nzima akiwa bado mtoto. Alipata umashuhuri mkubwa katika kusoma Qur'ani mwaka 1938 katika mji wa Mansurah. Mwaka 1939 alianza kusoma Qur'ani katika Redio ya Cairo na kuunda mfumo wake makhsusi wa qiraa. Alikuwa qari wa kwanza kusoma Qur'ani ndani ya Msikiti wa Al Aqsa huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu. Abul Ainain Shu'aisha alipata umashuhuri mkubwa kwa kutembelea nchi nyingi duniani kwa ajili ya kusoma Qurani. Katika muongo 1970 aliasisi Jumuiya ya Wasomaji wa Qur'ani nchini Misri akishirikiana na magwiji wengine wa qiraa ya Qurani kama Ustadh Abdul Basit Abdul Swamad. Sheikh Abul Ainain Shu'aisha alikuwa miongoni mwa watu wanaowapenda na kuwaashiki Ahlul Baiti na Watu wa Nyumba tukufu ya Mtume wetu Muhammad (saw). Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran, Ayatullah Ali Khamenei, amemsifu na kompongeza kwa kumpa laqabu ya Sheikh na Mzee wa Qurani. *** 

Abul Ainain Shu'aisha