Jumatatu, 16 Juni, 2025
Leo ni Jumatatu 20 Mfunguo Tatu Dhulhija 1446 Hijria mwafaka na 16 Juni 2025 Milaadia.
Miaka 1318 iliyopita katika siku kama ya leo alizaliwa Imam Musa Kadhim AS, mmoja wa wajukuu vipenzi wa Bwana Mtume Muhammad SAW.
Mpaka anatimiza umri wa miaka 20, mtukufu huyo alikuwa pamoja na baba yake mpenzi Imam Jaafar Sadiq AS akichota maalumati kwenye bahari yake ya elimu na maarifa.
Baada ya kuuliwa shahidi baba yake, Imam Musa Kadhim AS alibeba jukumu la Uimamu na uongozi wa Waislamu kwa muda wa miaka 35, ambapo katika kipindi chote hicho alihimili na kuvumilia tabu na misukosuko mingi. Miaka ya mwanzoni ya Uimamu wa Imam Musa Kadhim, ilisadifiana na kuporomoka kwa utawala wa Bani Umayyah na kushikwa hatamu za utawala na Bani Abbas.
Hadi mwisho wa uhai wake akiwa na umri wa miaka 55, mtukufu huyo alishuhudia tawala za makhalifa watano wa Bani Abbas, ambao kila mmoja wao hakusita kuchukua kila hatua ya kuwapiga vita wapinzani wake na kuwakandamiza watetezi wa haki waliokuwa wafuasi wa watu wa Nyumba ya Bwana Mtume SAW. Imam Musa Kadhim AS alitumia sehemu kubwa ya maisha yake kuwasomesha na kuwalea watu kimaadili na kuwaelimisha juu ya utamaduni na mafundisho sahihi ya Uislamu.
Alipambika kwa tabia njema, huruma na ukarimu usio na kifani na alikuwa maarufu mbele ya watu wote kwa utukufu wa nafsi, ukarimu, moyo wa kutoa sadaka kwa siri na kwa dhahiri na kuwasamehe waliomkosea. Mbali na kutoa mkono wa heri na baraka kwa mnasaba wa kuzaliwa Imamu huyu muadhamu, nakunukulieni maneno mazuri na ya hekima ya mtukufu huyo aliyesema: “Njia bora inayomkurubisha mtu kwa Mwenyezi Mungu baada ya kumjua Yeye Mola ni Swala, kuwatendea wema baba na mama na kujiepusha na uhasidi na kujiona”.

Katika siku kama ya leo miaka 81 iliyopita, yaani sawa na tarehe 16 Juni mwaka 1944, wanajeshi wa majini wa Marekani waliaza kushambulia kwa mabomu miji ya Japan sambamba na kuulenga mji wa Fokula ulioko kusini mwa nchi hiyo.
Hayo yalijiri wakati wa Vita vya Pili vya Dunia. Mashambulizi hayo yalifanyika kwa lengo la kuilazimisha Tokyo isalimu amri.
Katika mashambulizi hayo makumi ya maelfu ya raia wa Japan waliuawa na kujeruhiwa, sambamba na kuangamizwa viwanda na mashamba ya nchi hiyo. Vita hivyo vilipelekea Marekani kushambulia kwa mabomu ya nyuklia miji miwili ya Japan ya Hiroshima na Nagasaki mwezi Oktoba mwaka 1945.

Siku kama ya leo miaka 62 iliyopita sawa na tarehe 16 Juni 1963, Valentina Tereshkova mwanamke wa kwanza duniani mwanaanga kutoka Russia, alianza safari yake ya angani kwa kutumia safina ya anga iliyoitwa Vostok-6.
Mwanake huyo alitua katika orbiti ya ardhi wakati ambao Valery Bykovsky mwanaanga mwingine wa Russia alipokuwa akijishughulisha pia kuzunguka dunia.
Safari ya Tereshkova katika anga za juu ilifanyika miaka miwili baada ya safari ya Yuri Gagarin ambayo ilikuwa ya kwanza kufanywa na mwanadamu katika anga hizo.
Katika muda wa masaa 70 na dakika 50 aliyokuwa katika anga za juu, Tereshkova alizunguka dunia mara 48.

Siku kama ya leo miaka 49 iliyopita wananchi wa Soweto huko Afrika Kusini walianza harakati za mapambano dhidi ya utawala wa ubaguzi wa rangi wa makuburu.
Katika kipindi hicho Afrika Kusini ilikuwa ikitawaliwa na wazungu wachache waliodhibiti kila kitu na sheria zilizokuwa dhidi ya binadamu.
Juni 16 mwaka 1976 maelfu ya wanafunzi wazalendo walifanya maandamano makubwa kupinga sera za kibaguzi katika sekta ya elimu ambayo yalikabiliwa na ukandamizaji mkubwa wa utawala wa kibaguzi. Mamia ya raia waliuawa na wengine kujeruhiwa.
