Jun 29, 2024 02:21 UTC
  • Jumamosi, 29 Juni, 2024

Leo ni Jumamosi 22 Mfunguo Tatu Dhul-Hija 1445 Hijria mwafaka na 29 Juni 2024 Miladia.

Katika siku kama ya leo miaka 1385 iliyopita kulingana na kalenda ya Hijria, Maytham al-Tammar mmoja wa Masahaba na wafuasi wa Mtume Muhammad (saw) aliuawa shahidi. Awali Maytham al-Tammar alikuwa mtumwa na alinunuliwa na kuachiwa huru na Imam Ali bin Abi Talib (as). Imam Ali alikuwa akimpenda na kumthamini sana Maytham al-Tammar kama ambavyo Maytham pia alikuwa na mapenzi makubwa kwa Imam Ali. Hatimaye katika siku kama ya leo, sahaba huyo mwema wa Mtume (saw) aliuawa kinyama na watawala wa Bani Umayyah kwa kosa la kuwapenda na kuwaunga mkono Ahlul Bait (as). 

Kaburi la Maytham al-Tamar

 

Miaka 964 iliyopita katika kama ya leo alifariki dunia Khaja Abdullah Ansari malenga na arif mkubwa wa Kiislamu na wa Iran wa karne ya tano Hijria.  Alizaliwa katika mji wa Herat ulioko Afghanistan ya leo ambao wakati huo ulikuwa sehemu ya ardhi ya Iran. Alipewa lakabu ya Mzee wa Herat. Khaja Abdullah Ansari ameandika vitabu vingi vya elimu ya irfani kwa lugha za Kiarabu na Kifarsi kwa sura ya mashairi, mashuhuri zaidi vikiwa ni "Munajat Nameh", "Mohabbat Nameh" na "Zadul Arifin". Vilevile ameandika tafsiri ya Qur'ani Tukufu aliyoipa jina la "Kashful Asrar."

Khaja Abdullah Ansari

 

Siku kama ya leo miaka 111 iliyopita vilianza Vita vya Pili vya Balkan kati ya Bulgaria na umoja wa nchi za Serbia, Ugiriki, Montenegro, Romania na utawala wa Othmania. Karibu mwaka mmoja kabla ya hapo katika Vita vya Kwanza vya Balkan, Bulgaria, Serbia, Ugiriki na Montenegro zilizokuwa sehemu ya utawala wa Othmania, zilianzisha uasi dhidi ya ufalme huo, na kutokana na kudhoofika utawala huo nchi hizo zilifanikiwa kupata uhuru. Kwa msingi huo karibu asilimia 80 ya nchi zilizokuwa chini ya himaya ya Othmania huko Ulaya zikatoka chini ya udhibiti wa dola hilo. Hata hivyo nchi zilizoshinda katika Vita vya Kwanza vya Balkan hazikuweza kufikia makubaliano ya kugawana ardhi zilizokombolewa sababu iliyopelekea kuanza Vita vya Pili vya Balkan. Vita vya Balkan viliandaa mazingira ya kuanza kwa Vita vya Kwanza vya Dunia. 

Picha ya vita vya pili vya Balkan

 

Siku kama ya leo miaka 48 iliyopita yaani tarehe 29 Juni mwaka 1976, muungano wa visiwa vya Ushelisheli ulipata uhuru na kila siku kama hii huadhimishwa katika visiwa hivyo kama siku ya taifa. Hadi kufikia katikati ya karne ya 18, wakati ambao Wareno walikuwa wakiikalia kwa mabavu ardhi hiyo, sehemu kubwa ya visiwa vya Ushelisheli ilikuwa bado haijagunduliwa na haikuwa na wakazi. Mwishoni mwa karne ya 18 wakati ulipopamba moto wa mapinduzi ya Ufaransa, wanajeshi wa Uingereza waliokuwa katika eneo la Afrika waliivamia Ushelisheli. Mapambano ya kuikomboa nchi hiyo yalipamba moto mwaka 1960 na kuendelea, na miaka 16 iliyofuata visiwa vya Ushelisheli vikawa huru na kuasisi mfumo wa Jamhuri. Ushelisheli inaundwa na visiwa kadhaa vilivyoko katika bahari ya Hindi ikipakana na Madagascar.

 

Katika siku kama ya leo miaka 38 iliyopita, sawa na tarehe 9 Tir 1365 Hijria Shamsia, ilianza operesheni ya kijeshi ya Karbala -1 kwa ajili ya kukomboa mji wa Mehran huko magharibi mwa Iran uliokuwa umetwaliwa na jeshi vamizi la Saddam Hussein wa Iraq. Mji huo ulikaliwa kwa mabavu muda mfupi baada ya jeshi la Baath la Iraq kuvamia ardhi ya Iran Septemba 1981 na ulikombolewa na wapiganaji shupavu wa Iran katika operesheni makini ya Karbala-1.

Picha inayowaonyesha wapiganaji wa Kiirani katika Operesneni ya kijeshi ya Karbala-5

 

Tarehe 29 Juni miaka 32 iliyopita aliuawa Mohamed Boudiaf aliyekuwa Mkuu wa Baraza la Serikali ya Algeria. Mohamed Boudiaf alikuwa rais wa nne wa Algeria tangu nchi hiyo ilipopata uhuru. Alijiunga na harakati za siri za kupinga ukoloni wa Ufaransa akiwa bado kijana na kupanda ngazi katika harakati ya wananchi wa Algeria iliyokuwa ikiendesha harakati za siri dhidi ya wakoloni wa Kifaransa. Baada ya ushindi wa mapinduzi ya wananchi wa Algeria hapo mwaka 1962 Mohamed Boudiaf aliunda serikali ya kisoshalisti akishirikiana na Ahmed Ben Bella. Alikimbilia nje ya nchi kufuatia mapinduzi ya Houari Boumediene dhidi ya serikali Ben Bella na kurejea Algeria baada ya kujiuzulu Chadli Bendjedid na kuunda baraza la uongozi. Kama walivyokuwa viongozi wengi wa baada ya uhuru wa Algeria, Mohamed Boudiaf alikuwa mpinzani mkubwa wa fikra za Kiislamu na baada ya kushika madaraka alivunja harakati ya Kiislamu ya nchi hiyo iliyokuwa imeshinda uchaguzi wa Bunge na kubatilisha matokeo ya uchaguzi huo. Hatua hiyo ilisababisha machafuko ya ndani nchini Algeria na tarehe 29 Juni 1992 alipigwa risasi na kuuawa na mmoja wa walinzi wake. 

Tags