Iran yaonya vyombo vya habari vya India kwa habari za uongo
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i128872-iran_yaonya_vyombo_vya_habari_vya_india_kwa_habari_za_uongo
Ubalozi wa Iran mjini New Delhi, umekosoa uchapishaji wa ripoti zisizo na msingi katika baadhi ya vyombo vya habari vya India, na kusema katika taarifa yake kwamba: "Vyombo vya habari vya India havipaswi kuhatarisha imani ya umma na sifa ya kitaaluma kwa kuchapisha habari za uongo."
(last modified 2026-02-21T22:51:18+00:00 )
Jul 28, 2025 23:02 UTC
  • Iran yaonya vyombo vya habari vya India kwa habari za uongo

Ubalozi wa Iran mjini New Delhi, umekosoa uchapishaji wa ripoti zisizo na msingi katika baadhi ya vyombo vya habari vya India, na kusema katika taarifa yake kwamba: "Vyombo vya habari vya India havipaswi kuhatarisha imani ya umma na sifa ya kitaaluma kwa kuchapisha habari za uongo."

Katika siku za hivi karibuni, baadhi ya vyombo vya habari vya India vimechapisha ripoti zisizo na msingi ambazo haziheshimu Iran na kiongozi wake mkuu.

Ubalozi wa Iran mjini New Delhi umekosoa vikali hatua hiyo na kueleza kwamba, inakinzana na maadili ya taaluma ya habari.

"Ripoti kama hizo za kutowajibika sio tu kwamba hudhoofisha imani ya umma lakini pia huharibu sana sifa ya kitaaluma ya taasisi hizi za vyombo vya habari miongoni mwa watazamaji wao", imeeleza taarifa hiyo.

Sehemu nyingine ya taarifa ya ubalozi wa Iran mjini New Delhi imesema, vyombo vya habari vya India vinapaswa kutegemea vyanzo vya kuaminika na visivyo na upendeleo na kuepuka kuchapisha maudhui yenye utata na yasiyo sahihi kuhusu Iran.

Aidha taarifa hiyo imesema, vyombo vya habari vinapaswa kufanya kazi ili kuimarisha uhusiano wa kihistoria wa urafiki na kuheshimiana kati ya watu wa mataifa haya mawili makubwa na yaliyo na ustaarabu mkongwe.

Uhusiano mzuri kati ya Tehran na New Delhi ulianza miongo kadhaa iliyopita. Nchi hizo mbili ni wanachama wakuu wa Jumuiya ya Nchi Zisizofungamana na Siasa za Upande Wowote (NAM). Hata hivyo, katika kipindi cha muongo mmoja uliopita, hali imeibuka katika duru za kisiasa, hasa miongoni mwa vyombo vya habari, ambayo inaonekana kutaka kuzorotesha mahusiano haya kupitia uchapishaji wa habari za uongo.