Jul 27, 2025 02:32 UTC
  • Jumamosi, 26 Julai, 2025

Leo ni Jumamosi Mosi Mfunguo Tano Safar 1447 Hijria mwafaka na 26 Julai 2025 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 1410 iliyopita, awamu ya mwisho ya vita kati ya jeshi la Imam Ali bin Abi Twalib (as) na Muawiya bin Abi Sufiyan ilianza katika eneo la Siffin kandokando ya Mto Furati (Euphrates) nchini Iraq. Baada ya Imam Ali bin Abi Twalib (as) kushika hatamu za uongozi Muawiya alikataa kumpa mkono wa utiifu na akaamua kuanzisha vita dhidi ya serikali yake.  

 

Tarehe Mosi Safar miaka 1386 iliyopita, msafara wa familia ya Mtume Muhammad (SAW) ambayo ilichukuliwa mateka katika vita vya Karbala, uliwasili katika mji wa Damascus huko Sham ambao ulikuwa makao makuu ya utawala wa Yazid bin Muawiya. Wakiwa Sham, Ahlul Bait wa Mtume (SAW) hususan Bibi Zainab (as) na Imam Sajjad (as) walitoa hutuba katika msikiti wa Sham wakifichua maovu ya Yazidi, kiongozi dhalimu wa Bani Umayyah. Vilevile Ahlul Bait wa Mtume (SAW) walifikisha kwa watu ujumbe wa harakati ya mashahidi wa Karbala kwa njia nzuri kiasi kwamba watu wa Sham walielewa ukweli kuhusu jinai za jeshi la Yazid na kuzua hasira dhidi ya mtawala huyo. Hali hiyo ilimfanya Yazidi aliyetoa amri ya kuuawa Imam Hussein (as) na wafuasi wake, akane uhakika huo na kumtwisha lawama hizo Ubaidullah bin Ziyad, aliyekuwa gavana wa mji wa Kufa, Iraq. 

 

Siku kama ya leo miaka 178 iliyopita nchi ya Kiafrika ya Liberia ilipata uhuru. Liberia iko katika mwambao wa bahari ya Atlantic na inapakana na nchi za Guinea, Sierra Leone na Ivory Coast. Idadi kubwa ya raia wa nchi hiyo yenye jumla ya watu milioni tatu wanafuata dini za kijadi na kimila na asilimia 16 ya raia wake inaundwa na Waislamu. Lugha rasmi ya raia wa Liberia ni Kingereza. Liberia iliundwa mwaka 1822 kwa ajili ya Waafrika waliokuwa watumwa huko Marekani. Mwaka 1841 nchi hiyo iliandika katiba na kupewa jina la Liberia lenye maana ya ardhi ya watu huru.   

 

 Miaka 169 iliyopita katika siku kama ya leo George Bernard Shaw mwandishi, muigizaji wa michezo ya kuchekesha na mkosoaji wa Ki-Ireland alizaliwa katika mji wa Dublin. Baba yake alikuwa mtumishi wa serikali. Akiwa katika rika la kuinukia George Bernard alianza kuandika visa na tamthiliya. Alijitihidi kutoa taswira ya matatizo ya kijamii katika visa vyake. 1925 Shaw alitunukiwa tuzo ya nobel ya fasihi. 

George Bernard Shaw

 

Miaka 81 iliyopita katika siku kama ya leo, Reza Pahlavi, anayejulikana kama Reza Khan, mwanzilishi wa silsila Pahlavi nchini Iran, alikufa nchini Afrika Kusini baada ya kutawala wa miaka 16 na miaka mitatu ya uhamishoni. Alizaliwa mwaka 1257 Hijria  Shamsia katika kijiji kimoja kaskazini mwa Iran. Mnamo mwaka wa 1299 Hijria Shamsia, wakati akiwa afisa wa vikosi vya Kazakh, Reza Khan alipewa jukumu na Waingereza kufanya mapinduzi nchini Iran ili kulinda maslahi ya serikali ya London. Baada ya mapinduzi haya, Reza Khan akawa Waziri wa Ulinzi na kisha Waziri Mkuu. Hatimaye, kwa kuungwa mkono na Waingereza mwaka 1304 Hijria Shamsia, aliupindua utawala wa ukoo wa Qajar na kukalia kiti cha ufalme licha ya upinzani wa wanazuoni na wanasiasa wapenda uhuru. Baada yah apo aliitawala kimabavu Iran kwa muuda wa miaka 16 na kufanya njama za kufuta nembo za utamaduuni wa Kiislamu nchini Iran naa baadala yake kuweka nembo za Kimagharibi.

Maiti ya Reza Shah

 

Siku kama ya leo miaka 69 iliyopita, Gamal Abdul-Nasser rais wa wakati huo wa Misri alitangaza kuutaifisha Mfereji wa Suez. Mfereji huo ulianzishwa mwaka 1896 baada ya Misri kukaliwa kwa mabavu na Uingereza na kwa utaratibu huo, njia ya baharini baina ya Ulaya na Asia ikawa imefupishwa. Udhibiti wa Uingereza na Ufaransa kwa Mfereji wa Suez uliendelea hadi serikali ya Abdu l-Nasser ilipokuja kuutaifisha na kuutangaza kuwa mali ya taifa. Hatua hiyo ilifuatiwa na mashambulio ya kijeshi ya Uingereza, Ufaransa na utawala dhalimu wa Israel. Hata hivyo mashinikizo ya kimataifa dhidi ya madola vamizi na mapambano ya wananchi Waislamu wa Misri, yalivifanya vikosi vamizi viondoke katika mfereji huo muhimu na ukawa katika miliki ya serikali na taifa la Misri. 

 

Katika siku kama ya leo miaka 60 iliyopita visiwa vya Maldives huko kusini mwa bara Asia vilipata uhuru. Visiwa vya Maldives vilivamiwa na kukaliwa kwa mabavu na Wareno mwanzoni mwa karne ya 16. Visiwa hivyo baadaye vilidhibitiwa na Waholanzi na Wafaransa na hatimaye mwishoni mwa karne ya 19, vikakaliwa na Waingereza.

 

Siku kama ya leo miaka 46 iliyopita, yaani tarehe 26 Julai mwaka 1979,  Zuheir Mohsen, Katibu Mkuu wa wakati huo wa Harakati ya as-Sa'iqa tawi la Harakati ya Ukombozi ya Palestina (PLO) aliuawa kigaidi na maajenti wa shirika la ujasusi la utawala wa Kizayuni (Mossad) huko katika mji wa Cannes nchini Ufaransa. Magaidi wa Kizayuni walikimbia na kutoweka baada ya kufanya mauaji hayo na polisi wa Ufaransa walidai kuwa hawakupata uthibitisho kwamba Mossad ilihusika na mauaji hayo. 

Zuheir Mohsen