Jul 01, 2024 06:05 UTC
  • Hikma za Nahjul Balagha (58)

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum wasikilizaji wapenzi. Karibuni katika sehemu hii ya 58 ya mfululizo wa makala hizi fupifupi za Hikma za Nahjul Balagha. Leo pia tutaangalia kwa muhtasari hikma nyingine za Imam Ali bin Abi Talib AS kama ilivyonukuliwa kwenye kitabu cha Nahjul Balagha tukiwa na matumaini mtakuwa nasi hadi mwisho wa kipindi. Ingawa hii ni sehemu ya 58 ya mfululizo huu, lakini hikma tunayoichambua ni ya 51.

عَیْبُکَ مَسْتُورٌ، مَا أَسْعَدَکَ جَدُّک

Aibu yako ni yenye kusitirika madhali hadhi ungalinayo.

Katika hikma hii ya 51 ya Nahjul Balagha, Imam Ali AS anaashiria nukta nyingine muhimu sana iliyojaa hikma kwa maneno mafupi lakini yenye maana pana. Anasema madhali dunia haijakupa mgongo, madamu hadhi bado unayo, maadamu dunia iko na wewe, aibu zako nazo hufichika. 

Hapa Imam Ali, anatufundisha sote uhakika wa kanuni hii muhimu iliyopo kwenye jamii za wanadamu ambayo makosa yetu huwa yanafunikwa maadamu nyakati za maisha ni kwa faida na hadhi yetu, madhali tuna nguvu na ushawishi. Kwa sababu watu wengi hupenda kunufaika nasi kwa namna mbalimbali hivyo hufumbia macho aibu, kasoro na mapungufu yetu ili wapate mradi wao. Bali kuna wakati kasoro zetu hizo hutangazwa na huangaliwa kwa sura nzuri na kuchukuliwa kama fursa na faida kwetu. Lakini dunia inapotupa kisogo, tukawa tumepoteza ushawishi na hadhi, cheo na nafasi yetu kwenye jamii, makosa yetu hata madogo hufichuka na baadhi ya wakati hata mema yetu huonekana ni aibu mbele ya walimwengu. Na hilo kwa kweli ni kosa linalofanywa na wanadamu. Sasa hapa Imam Ali AS anatutanabahisha kwamba, tusitegemee maneno ya watu bali pale tunapoona tuna kasoro tufanye haraka kurekebisha kasoro hizo kwani hatujui hadhi na heshima yetu itabaki hadi lini na wala hatujui ni lini dunia itatupa kisogo. Tukumbuke pia kwamba, katika hikma ya 9 ya Nahjul Balagha tulichambua hikma kama hiyo ya Imam Ali AS aliposema: Ulimwengu ukimpa mtu uso humkopesha mazuri ya wengine na ukimpa kisogo humpoka mazuri hayo. Nakuomba tembelea tovuti yetu ya parstoday.ir/sw upate uchambuzi wa kina wa hikma hiyo ya 9 na nyinginezo za Nahjul Balagha.

Naam, lililo muhimu kwa mtu mwenye hikma ni kurekebisha mwenyewe kasoro na aibu zake asisubiri kunyookewa au kupewa mgongo na dunia. Katika Qur’ani Tukufu, Siku ya Kiyama ni siku ya kufichuliwa mambo ya ndani na yaliyofichika na hata siri kubwa za viumbe. Aya ya 9 ya Sura ya 86 ya at Tariq inasema: Siku zitakapodhihirishwa siri. Aya ya 18 ya sura ya 69 ya al Haaqah inasema: Siku hiyo mtahudhurishwa - haitafichika siri yenu yoyote. Aya hizo zinaonesha wajibu wa kila mtu kutambua kwamba hakuna siri inayoweza kubakia kuwa siri milele. Huenda wanadamu wasijue lakini hakuna chochote kinachofichika mbele Muumba wa mbingu na ardhi. Ni wajibu wa kila mmoja wetu kujirekebisha mwenyewe kabla ya kufedheheka kwa kufichuka siri yake. Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.

Tags