Jumatatu, Agosti 12, 2024
Leo ni Jumatatu tarehe 7 Mfunguo Tano Safar 1446 Hijria inayosadifiana na tarehe 12 Agosti 2024 Milaadia.
Katika siku kama ya leo miaka 1396 iliyopita, yaani tarehe 7 Safar mwaka 50 Hijiria kwa mujibu wa baadhi ya mapokezi, aliuawa shahidi Imam Hassan bin Ali bin Abi Twalib al Mujtaba (as), mjukuu wa Mtume Muhammad (saw).
Imam Hassan (as) ni mtoto wa Bibi Fatima al Zahra na Imam Ali bin Abi Talib (as), na alizaliwa mwaka wa 3 baada ya Mtume (saw) kuhamia Madina. Aliishi miaka saba ya mwanzo wa umri wake pamoja na babu yake, Mtume Muhammad (saw) ambapo alinufaika na mafunzo na maarifa ya dini tukufu ya Kiislamu. Imam Hassan alichukua jukumu zito la kuongoza Umma wa Kiislamu akiwa na umri wa miaka 37 baada ya kuuawa shahidi baba yake, Imam Ali (as).
Baada ya kuuliwa Imam Ali (as), Waislamu walimpa baia na mkono wa utiifu Imam Hassan kwa ajili ya kuwaongoza; hata hivyo baada tu ya kushika hatamu alikabiliwa na njama na uasi wa Muawiyah bin Abi Sufiyan. Hatimaye Imam Hassan aliandaa jeshi kwa ajili ya kukabilina na uasi wa Muawiya, ingawa muovu huyo (Muawiya) alitumia hila za kila namna kuwanunua wafuasi wa Imam Hassan ambao hatimaye walimkimbia na kumwacha peke yake mjukuu huyo wa Mtume wa Allah.
Imam Hassan al Mujtaba (as) alilazimika kufanya suluhu na Muawiyah bin Abi Sufiyan kwa ajili ya kulinda maslahi ya Uislamu na Waislamu. Mjukuu huyo kipenzi wa Mtume (saw) aliuawa shahidi siku kama ya leo kwa kupewa sumu katika njama iliyopangwa na Muawiya bin Abi Sufiyan.
Tarehe 12 Agosti mwaka 1949 hati ya makubaliano ya kimataifa ya kuwalinda majeruhi na mateka wa kivita ilipasishwa kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa huko Geneva, Uswisi.
Hati hiyo ilibuniwa kufuatia miamala isiyo ya kibinadamu na jinai zilizokuwa zikifanywa dhidi ya majeruhi na mateka wa kivita wakati wa Vita vya Pili vya Dunia.
Siku kama hii ya leo miaka 48 iliyopita sawa na tarehe 12 Agosti 1976, kambi ya wakimbizi wa Palestina ya Tel al Zaatar iliyoko karibu na Beirut mji mkuu wa Lebanon, ilitekwa baada ya kuzingirwa kwa muda mrefu na wanamgambo wa Kimaroni wa nchi hiyo na wakazi wake wakauawa kwa umati.
Kambi hiyo ilikuwa ikiwahifadhi maelfu ya wakimbizi wa Palestina na ilianza kuzingirwa mwanzoni mwa mwaka 1976 kwa uungaji mkono na uingiliaji wa utawala wa Kizayuni wa Israel. Utawala wa Kizayuni ulifanya hivyo kwa lengo la kushadidisha vita vya ndani huko Lebanon.
Tarehe 7 Safar miaka 35 iliyopita alifariki dunia Ayatullahil Udhma Sayyid Shahabuddin Mar'ashi Najafi, mmoja wa Marajii na viongozi wa juu wa Kiislamu hapa nchini, akiwa na umri wa miaka 96.
Alimu huyo alisoma elimu za fiqihi, usul fiqihi, hadithi, tafsiri ya Qur'ani, teolojia na misingi ya kimaadili katika vyuo vikuu vya kidini katika miji ya Kadhmein na Najaf, Iraq.
Miongoni mwa athari kubwa zilizoachwa na Ayatullah Mar'ashi Najafi ni maktaba kubwa ya vitabu iliyoko mjini Qum, ambayo inahesabiwa kuwa ya aina yake. Mwanazuoni huyo pia daima alikuwa muungaji mkono mkubwa wa Imam Ruhullah Khomeini na harakati ya Mapunduzi ya Kiislamu ya wananchi wa Iran.
Na miaka 25 iliyopita, Umoja wa Mataifa uliitangaza Agosti 12 kila mwaka, kuwa ‘Siku ya Vijana Duniani’ ili kueleza umuhimu wa vijana katika dunia ya sasa.
Tabaka hili lenye utanashati la jamii ndiyo sababu ya maendeleo ya kila nchi kwa msingi huo vijana katika kila nchi wanapaswa kupewa umuhimu mkubwa. Kutokana na umuhimu wao vijana wanapaswa kulindwa na kusaidiwa na serikali hususan katika masuala ya ajira, makazi na kujenga familia.
Katika upande mwingine kizazi cha leo cha vijana kinakabiliwa na changamoto nyingi za kimwili na kiroho ikiwa ni pamoja na ongezeko la matumizi ya dawa za kulevya, magonjwa ya kuambukiza kama Ukimwi na virusi vya HIV, intaneti na michezo ya computa ambayo inawatumbukiza vijana wengi katika ufuska na utovu wa maadili.
Kutangazwa Siku ya Vijana Duniani kunaweza kusaidia juhudi za kuwakumbusha vijana umuhimu wao na kuzuia changamoto mbalimbalizinazolikabili tabaka hilo muhimu.