Aug 12, 2024 08:35 UTC
  • Hikma za Nahjul Balagha (61)

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum wasikilizaji wapenzi. Karibuni katika sehemu hii ya 61 ya mfululizo wa makala hizi fupifupi za Hikma za Nahjul Balagha. Leo pia tutaangalia kwa muhtasari hikma nyingine za Imam Ali bin Abi Talib AS kama ilivyonukuliwa kwenye kitabu cha Nahjul Balagha tukiwa na matumaini mtakuwa nasi hadi mwisho wa kipindi hiki. Ingawa hii ni sehemu ya 61 ya mfululizo huu, lakini hikma tunayoendelea kuichambua ni ya 54.

لَا غِنَى کَالْعَقْلِ، وَ لَا فَقْرَ کَالْجَهْلِ، وَ لَا مِیرَاثَ کَالْأَدَبِ، وَ لَا ظَهِیرَ کَالْمُشَاوَرَةِ

Hakuna utajiri kama akilii, wala ufakiri kama ujinga, wala urithi bora kama adabu na wala ngao bora kama kushauriana na watu.

Katika hikma hii ya 54, Imam Ali anatufundisha masuala mengine manne muhimu sana katika kujenga nafsi na jamii iliyobora. Tutatupia jicho kwa muhtasari moja baada ya nyingine kulingana na muda utakavyotuhusu.

Kitu cha kwanza kabisa kilichogusiwa na Imam Ali AS katika hikma hii yenye thamani kubwa ni pale aliposema: لَا غِنَى کَالْعَقْلِ، وَ لَا فَقْرَ کَالْجَهْلِ Hakuna utajiri kama akilii, wala ufakiri kama ujinga. Hapa Imam anatufafanulia kwa balagha ya juu maana hasa ya utajiri na maana hasa ya umaskini na ufakiri. Kwa mujibu wa Imam, utajiri si mtu kumiliki mali nyingi na kuwa na utajiri mkubwa wala umaskini si kuwa na mali kidogo na kipato cha chini, bali vielelezo vya mambo hayo mawili ni kitu kiingiine kabisa. 

Amma kuhusu akili na ujinga, kuna aya nyingi tu za Qur'ani Tukufu zinazozungumzia mambo hayo na kuyatolea maana yake. Kwa mfano katika aya ya 10 ya sura ya 67 ya al Mulk tunasoma: 

وَقَالُوا لَوْ کُنَّا نَسْمَعُ أَوْ نَعْقِلُ مَا کُنَّا فِی أَصْحَابِ السَّعِیرِ

Na (watu wa motoni) watasema: Lau kuwa tungeli sikia, au tungeli kuwa na akili, tusingeli kuwa katika watu wa Motoni!

Naam watalalamika wakisema lau kama tungetumia vizuri akili zetu na tusingelifanya ujinga, basi leo hii tusingekuwa tunateketea kwenye moto mkali.

Aya za namna hiyo ni nyingi sana ndani ya Qur'ani Tukufu. Hapa tunukuu aya nyingine inayopatikana katika sura ya 6 ya al An'am aya ya 32 inasema:

وَمَا الْحَیَاةُ الدُّنْیَا إِلاَّ لَعِبٌ وَلَهْوٌ وَلَلدَّارُ الآخِرَةُ خَیْرٌ لِّلَّذِینَ یَتَّقُونَ أَفَلاَ تَعْقِلُونَ

Na maisha ya dunia si chochte ila ni mchezo na pumbao tu. Na hakika nyumba ya Akhera ni bora zaidi kwa wanaomcha Mungu. Basi, je, hamtii akilini?

Hivyo kwa kielelezo cha kutumia vizuri akili ndivyo mwanadamu anavyotakiwa kufanya katika kumwabudu Mola wake. Kama anatakiwa apate mafanikio ya duniani na Akhera, basi lazima atumie vizuri akili yake. Mwanadamu hatakiwi kuipa likizo akili yake katika jambo lolote lile. Moja ya sifa za kipekee za akili ni kwamba inamwokoa mwanadamu kwenye mazingira magumu na mbele ya wajinga na wapumbavu. Na hilo ndilo linalompambanua mwenye akili na punguani. Wakati wowote mwenye akili anakupambana na fitna, hufanya haraka kurejea kwa Mola wake, huupiga kufuli ulimi na mkono wake usitumbukie kwenye firna hiyo. Na wakati wowote mwenye akili anapoona jambo jema hulipokea kwa heshima na kwa hikma na busara kubwa na hayuko tayari hata kidogo kuja kufedheheka mbele ya Muumba wake.  

Hivyo ni sawasawa kabisa maneno ya Imam Ali AS aliposema: Hakuna utajiri kama akili na hakuna ufakiri kushinda ujinga.

Amma katika sehemu ya tatu na nne ya hikma yake hii Imam Ali AS anasema:

لَا مِیرَاثَ کَالْأَدَبِ، وَ لَا ظَهِیرَ کَالْمُشَاوَرَةِ

Hakuna urithi bora kama adabu na wala ngao bora kama kushauriana na watu.

Maana ya adab katika hikma hii si ufasaha wa lugha, bali adab maana yake ni adabu, ni kuwa na miamala na tabia nzuri na kila mtu. Imepokewa katika historia kwamba wakati Imam Ali AS alipolazimishwa na Muawiya kuingia vitani na liwali huyo wa Sham, aliwasikia wafuasi wake wawili Imam wanatamka maneno mabaya kuhusu watu wa Sham. Imam Ali AS alituma mtu wake ili kuwakataza wasitoe maneno hayo. Watu hao walikuja kwa Imam na kumwambia Yaa Amiral Muuminin, kwani sisi hatuko kwenye haki katika hili? Imam aliwajibu, bila ya shaka muko kwenye haki lakini siridhiki ninapokuoneni mnakuwa kama wao katika kulaani na kutoa maneno mabaya. Ninachopenda mimi ni kukuoneni mnatumia hikma kukabiliana nao msikariri maneno yao mabaya. Wale watu wawili walisema: Yaa Amiral Muuminin, tumesikia na tutatekeleza nasaha zako.

Aidha imepokewa hadithi kutoka kwa Bwana Mtume Muhammad SAW akisema:

من لا أدب له لا عقل له

Asiye na adabu hana akili.

Amma katika sehemu ya nne na ya mwisho ya hikma hii, Imam Ali AS anazungumzia ngao bora katika maisha ya mwanadamu akisema: Hakuna ngao bora kama kushauriana na watu (wema).

Dini tukufu ya Kiislamu inalipa umuhimu mkubwa suala la kushauriana mambo. Pamoja na kwamba Bwana Mtume Muhammad SAW ni mja bora kabisa wa Allah aliyekuwa anapokea wahyi moja kwa moja kutoka kwa Allah na pamoja na kuwa Qur’ani imeshushwa kwenye kifua chake, na licha ya kwamba alikuwa na hikma kubwa na muono wa mbali kabisa kuliko kiumbe yeyote yule, na wala hakuhitajia ushauri wa mtu mwingine, ilimtosha miongozo aliyokuwa akipokea moja kwa moja kutoka kwa Mwenyezi Mungu, lakini pamoja na hayo na kwa ajili ya kutufundisha akhlaki na tabia njema na kutuonesha umuhimu wa mashauriano, alikuwa akiwapa nafasi Masahaba wake watoe ushauri wao kuhusu mambo mbalimbali. Kwa njia hiyo Bwana Mtume aliwalea masahaba wake katika hali ya kupenda kushauriana na kwa upande mwingine aliziwezesha fikra na akili zao kuchanua kama ambavyo aliwapa nguvu ya kujiamini na kuona kuwa ni watu wenye hadhi na wanaothaminiwa na Kiongozi wao.

Kimsingi, wale wanaofanya kazi zao muhimu kwa kushauriana na watu wenye busara, uwezekano wa kwenda kombo unakuwa mdogo ikilinganishwa na wale wasiopenda ushauri wa wengine. Tab’an kama inavyosemwa mara kwa mara si kila mtu ana hadhi na ustahiki wa kuombwa ushauri. Mtu anayefaa kuombwa ushauri ni mcha-Mungu, mkweli, mtunza siri, jasiri, mwenye welewa wa jambo analoshauriwa na ambaye ushauri wake unaweza kumfaidisha anayemuomba ushauri.

Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.