Jumamosi, 24 Agosti, 2024
Leo ni Jumamosi 19 Mfunguo Tano Safar 1446 Hijria mwafaka na 24 Agosti 2024 Milaadia.
Katika siku kama ya leo miaka 1275 iliyopita yaani tarehe 19 Safar mwaka 171 Hijria alizaliwa Abu Ma'ashar Balkhi mmoja kati ya wanajimu na wasomi wakubwa wa elimu ya nujumu wa Kiirani. Kutokana na hamu yake kubwa ya elimu ya nyota, Abu Ma'ashar alielekea Baghdad na kuanza kusoma elimu ya nujumu. Abu Ma'ashar Balkhi alitumia vyanzo vya lugha za Kiarabu, Kihindi, Kigiriki na Kisiriani kwa ajili ya kupata elimu ya nujumu na kuwa miongoni mwa wanajimu wakubwa katika zama zake. Kazi zake katika taaluma hiyo zilitumiwa kwa karne kadhaa katika ulimwengu wa Kiislamu na Kimagharibi hata baada ya kufariki kwake dunia. Miongoni mwa vitabu mashuhuri vya msomi huyo wa Kiislamu ni al-Madkhal al-Kabir na al-Mawalidul al Saghirah. ***
Siku kama ya leo miaka 95 iliyopita, yalianza mapambano ya Ukuta wa Nudba huko Baitul Muqaddas. Ukuta wa Nudba huko magharibi mwa Masjidul Aqswa ni eneo alilotumia Mtume Muhammad (saw) wakati wa kupaa mbinguni katika safari ya Mi'iraj na kwa sababu hiyo eneo hilo likawa na umuhimu wa kidini na kihistoria kwa Waislamu. Tangu wiki moja kabla ya kuanza mapambano hayo ya Ukuta wa Nudba, Wazayuni ambao taratibu walikuwa wameanza kuikalia kwa mabavu Palestina kwa kuungwa mkono na Uingereza, walianzisha harakati dhidi ya Waislamu. Siku hiyo Wapalestina wenye hasira walianzisha mapambano makali dhidi ya Wazayuni hao maghasibu. Mapambano hayo yalienea kwa kasi kwenye miji mingine ya Palestina na Waingereza wakaamua kutangaza utawala wa kijeshi huko Palestina kwa kuhofia hasira za Wapalestina. ***
Katika siku kama ya leo miaka 83 iliyopita kwa mujibu wa kalenda ya Kiirani, ikiwa ni wakati wa Vita Vikuu vya Pili vya Dunia, majeshi ya nchi waitifaki yaliivamia na kuikalia kwa mabavu ardhi ya Iran. Wasiwasi ulikuwa umezikumba nchi za Marekani, Ufaransa na Uingereza kufuatia kusonga mbele vikosi vya Ujerumani katika ardhi ya Umoja wa Kisovieti. Kwani nchi hizo zilikuwa zikitambua kwamba, endapo Ujerumani itaushinda Umoja wa Kisovieti maslahi yao katika eneo la Mashariki ya Kati yangekuwa hatarini. Ni kwa sababu hiyo ndiyo maana madola hayo yakapeleka huko Urusi silaha na vifaa vingi vya kijeshi kupitia ardhi ya Iran. Licha ya Iran kutangaza kutounga mkono upande wowote katika vita hivyo, Umoja wa Sovieti ulianza kuishambulia Iran kutoka upande wa magharibi na mashariki, huku majeshi ya Uingereza yakifanya mashambulio kama hayo kwa upande wa kusini. ***
Na siku kama leo miaka 33 iliyopita, Ukraine ilipata uhuru toka kwa Umoja wa Kisovieti. Russia ilianza kuikalia kwa mabavu Ukraine ambayo wakati huo ilikuwa chini ya udhibiti na utawala wa Poland, katikati mwa karne ya 17 Miladia. Hata hivyo mwaka 1922, nchi hiyo iliunganishwa na mataifa yaliyokuwa yakiunda Umoja wa Sovieti. Hatimaye katika tarehe kama ya leo, Ukraine ikajipatia uhuru wake. ***