Sep 22, 2024 02:17 UTC
  • Jumapili, 22 Septemba 2024

Leo ni Jumapili 18 Mfunguo Sita Rabiul-Awwal 1446 Hijria mwafaaka na tarehe 22 Septemba 2024 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 1687 iliyopita, yaani sawa na tarehe 22 Septemba mwaka 337, vilianza vita vya miaka 13 kati ya Iran na Roma katika utawala wa Shapur II (Dhul Aktaf), wa silsila ya watawala wa Sasani na ambavyo katika historia vilifahamika kama vita vya duru ya kwanza. Vita vya duru ya pili vilianza mwaka 359, ambapo katika duru zote, Wairani waliibuka na ushindi. Katika duru ya kwanza ambapo vita hivyo vilidumu hadi mwaka 350, Waroma walipoteza kila kitu walichokuwa wakikidhibiti eneo la mashariki mwa Bahari ya Mediterranean, na mfalme wao aliuawa katika duru ya pili ya vita hivyo.

 

Siku kama ya leo miaka 1445 iliyopita kulingana na kalenda ya Hijria, ilianza kazi ya ujenzi wa Msikiti wa Mtume mjini Madina ambao ni msikiti wa pili kwa utukufu duniani baada ya Masjidul Haram. Mtume (SAW) alitoa amri ya kujengwa msikiti wa Madina baada tu ya kuhamia mjini humo na yeye mwenyewe alishiriki katika ujenzi wake. Kandokando ya msikiti huo kulijengwa vyumba vya Mtume na baadhi ya maswahaba zake. Mtume hakuutumia msikiti kwa ajili ya ibada tu, bali alitumia pia sehemu hiyo kwa ajili ya masuala kama kutoa hukumu baina ya watu, vikao vya mashauriano, mafunzo ya kivita na utatuzi wa masuala mbalimbali ya Waislamu. 

Muonekano wa msikiti wa Mtume mjini Madina

 

Katika siku kama ya leo miaka 122 iliyopita sawa na tarehe Mosi Mehr 1281 Hijria Shamsia, alizaliwa Ayatullahil Udhmaa Sayyid Ruhullah al Musawi Khomeini, mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Baba yake Imam Khomeini ambaye alikuwa miongoni mwa wanazuoni wa Kiislamu, aliuawa shahidi Imam akiwa bado mtoto na hivyo akalelewa na mama na shangazi yake. Baada ya kukamilisha masomo ya msingi, Ruhullah Khomeini alijiunga na masomo ya juu kwa walimu mashuhuri hususan Ayatullah Abdul Karim Hairi na Muhammad Ali Shahabadi. Imam Khomeini alianzisha harakati kubwa ya kupambana na utawala wa kidhalimu wa Shah baada ya kufariki dunia Ayatullah Borujerdi. Upinzani na mapambano yake yalimfanya mtawala kibaraka, Shah ampeleke uhamishoni katika nchi za Uturuki, Iraq na Ufaransa. Imam aliendeleza mapambano yake dhidi ya Shah akiwa uhamishoni alikobakia kwa kipindi cha miaka 15 na baadaye alirejea nchini na kuuondoa madarakani utawala wa kifalme wa Shah na kuasisi Jamhuri ya Kiislamu ya Iran hapo mwaka 1979.

 

Katika siku kama ya leo miaka 116 iliyopita, nchi ya Bulgaria ilijipatia uhuru kutoka kwa utawala wa Othmania. Bulgaria ilianza kutawaliwa na utawala huo mwishoni mwa karne ya 14. Wakati huo maudhi dhidi ya Wakristo yalianza na kuendelea kwa karibu miaka 500 ya udhibiti wa Othmania kwenye nchi hiyo na suala hilo liliibua uasi wa mara kwa mara wa raia wa Bulgaria. Hatimaye mwaka 1878 nchi hiyo ilipata uhuru na kujitangazia mamlaka ya ndani. Tarehe 22 Septemba mwaka 1908 mfalme wa wakati huo wa Bulgaria alitangaza uhuru kamili wa nch hiyo.

 

Siku kama ya leo miaka 64 iliyopita, nchi ya Mali iliyo kaskazini magharibi mwa Afrika ilipatia uhuru. Karibu miaka elfu mbili iliyopita nchi ya Mali ilikuwa na utamaduni mkubwa na uliong'ara. Hata hivyo nchi hiyo tangu karne ya 18 hadi ya 19 Miladia ilikuwa moja ya tawala za ufalme wa Sudan. Baada ya Morocco kutwaa baadhi ya maeneo yaliyokuwa chini ya tawala za ufalme wa Sudan ikiwemo Mali, tawala mbalimbali za kikabila nchini Mali zilifanikiwa kuingia madarakani. Satwa ya Wafaransa nchini Mali ilianza mnamo karne ya 19 na hadi kufikia mwaka 1898 nchi hiyo ilikuwa chini ya usimamizi wa Ufaransa. Hata hivyo Mali ambayo ilikuwa ikiitwa Sudan ya Ufaransa, mwaka 1958 ilianza kujitawala na mwaka 1960 ikajipatia uhuru wake kamili.