Oct 01, 2024 06:47 UTC
  • Jumanne tarehe Mosi Oktoba 2024

Leo ni Jumanne tarehe 27 Mfunguo Sita Rabiul-Awwal 1446 Hijria sawa na tarehe Mosi Oktoba 2024.

Katika siku kama ya leo miaka 2346 iliyopita aliaga dunia mwanafalsafa mashuhuri wa Ugiriki ya kale, Aristotle.

Aristotle alizaliwa mwaka 384 kabla ya kuzaliwa Nabi Isa Masih, katika mji wa Stagira ambao sasa ni sehemu ya jimbo la Ugiriki la Macedonia ya Kati. Baba yake alikuwa daktari wa mfalme wa Macedonia na alipata mali nyingi kwa njia hii.

Aristotle alifariki dunia Oktoba 1, mwaka 322 kabla ya kuzaliwa Isa Masih akiwa na umri wa miaka 62. 

Tarehe 27 Rabiul Awwal miaka 1083 iliyopita alizaliwa mshairi na mwandishi mashuhuri wa Kiarabu, Abul Alaa al Ma'arri katika eneo la Maarratun Nu'man karibu na mji wa Halab (Aleppo) nchini Syria.

Baadaye alielekea Baghdad huko Iraq kwa ajili ya kukamilisha elimu ya juu. Licha ya kuwa kipofu tangu utotoni, lakini Abul Alaa alitokea kuwa mshairi mashuhuri na hodari wa zama zake.

Miongoni mwa vitabu vyake mashuhuri la "Risalatul Ghufran" na "al Aamali." 

Abul Alaa al Ma'arri

Miaka 75 iliyopita katika siku kama ya leo, ilitangazwa rasmi Jamhuri ya Watu wa China chini ya uongozi wa Mao Tse Tung.

Nchi ya China yenye ustaarabu mkongwe, ilikuwa chini ya udhibiti wa madola ya Ulaya kuanzia mwishoni mwa karne ya 16. Mara kadhaa Wachina walianzisha vita dhidi ya mkoloni hasa Muingereza ili kuikomboa nchi yao lakini hawakufanikiwa.

Mwaka 1912 mapinduzi yaliyoongozwa na Sun Yat-Sen dhidi ya mfumo wa utawala wa Kifalme yalizaa matunda na kiongozi huyo akachaguliwa kuwa rais wa China.

Katika siku kama ya leo miaka 65 iliyopita, nchi ya Nigeria ilipata uhuru.

Wareno waliwasili Nigeria katika karne ya 15 na mkoloni Mwingereza naye akawasili katika nchi hiyo katika karne ya 16. Katika karne ya 17 ardhi ya Nigeria iligeuzwa na kuwa moja kati ya vituo muhimu vya biashara ya utumwa. Mwishoni mwa karne ya 19 vikosi vya majeshi ya Uingereza, viliidhibiti kikamilifu ardhi ya Nigeria.

Mwaka 1914 Uingereza uliziunganisha nchi mbili za Nigeria ya Kaskazini na Kusini zilizokuwa chini ya udhibiti wake na kuunda koloni moja la Nigeria. Miaka 40 baadaye nchi hiyo ikajitangazia kuwa na utawala wa ndani. Hatimaye baada ya kupitia misukosuko mingi, Nigeria ikajipatia uhuru katika siku kama ya leo.

Siku kama ya leo Miaka 56 iliyopita, Ayatullah Sayyid Muhsin Hakim, mkuu wa kituo cha kidini cha Najaf aliaga dunia akiwa na umri wa miaka 92.

Alipambana vikali na kila kundi au watu waliojaribu kuharibu jina la Uislamu. Fatua yake mashuhuri ya kupinga fikra ya ukomunisti dhidi ya mafundisho ya dini ilileta mabadiliko makubwa nchin Iraq. Fatua hiyo pia ilimpelekea kutoa amri ya kupigana jihadi dhidi ya utawala haramu wa Israel.

Ujenzi wa maktaba, shule na vituo vya kidini na kiutamaduni pamoja na uandishi wa vitabu kama vile Mustamsak Urwat al-Wuthqah na Nahjul Faqaha ni miongoni mwa vitabu mashuhuri vilivyoandikwa na mwanazuoni huyo mashuhuri wa Kiislamu.

Ayatullah Sayyid Muhsin Hakim

Na tarehe Mosi Oktoba ni siku ya Wazee Duniani.

Siku hii ilitengwa kwa ajili ya kuwakirimu na kuwaenzi watu wa tabaka hilo.

Ni vyema kukumbusha hapa kuwa hapa nchini Iran na kutokana na mabadiliko yaliyotokea baada ya Mapinduzi ya Kiislamu na utamaduni wa Kiislamu unaotawala hapa nchini wazee na watu wazima wanapewa nafasi ya juu ndani ya familia na katika jamii.

 

Tags