Jumamosi, tarehe 15 Machi, 2025
Leo ni Jumamosi tarehe 14 Ramadhani 1446 Hijria, sawa na tarehe 15 Machi, 2025.
Siku kama ya leo miaka 1379 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 14 Ramadhani mwaka 67 Hijria, aliuawa shahidi Mukhtar bin Abu Ubaida al Thaqafi, kiongozi wa harakati ya kulipiza kisasi cha damu ya Imam Hussein bin Ali AS, mjukuu wa Mtume Mtukufu Muhammad SAW.
Imam Hussein AS akiwa pamoja na wafuasi wake na watu wa familia yake, aliuawa shahidi na wafuasi wa Yazid bin Muawiya, akilinda dini tukufu ya Kiislamu. Mukhtar alianzisha harakati zake katika mji wa Kufa. Kabla yake, kulijitokeza kundi la 'Tawwabiin' ambalo lilianzisha mapambano dhidi ya utawala wa Bani Umayya, kwa lengo la kulipiza kisasi cha damu ya Imam Hussein AS.
Mukhtar al Thaqafi alitawala Kufa kwa muda wa mwaka mmoja hivi, na hatimaye alishindwa na jeshi la Mus'ab bin Zubair na kuuawa shahidi katika siku kama hii ya leo.

Siku kama ya leo miaka 171 iliyopita alizaliwa tabibu maarufu wa Kijerumani kwa jina la Emil Adolf von Behring.
Behring aliendeleza utafiti wa Louis Pastor, mwanakemia wa Kifaransa wa zama hizo katika uwanja wa kutambua na kuzuia maradhi yanayoambukiza na kupata mafanikio makubwa katika suala hilo.
Mwaka 1901 Emil Adolf von Behring alitunukiwa tuzo ya Nobel katika taaluma ya fizikia.

Katika siku kama ya leo miaka 118 iliyopita, Parvin I’tisami mwandishi na malenga mahiri wa Kiirani aliyekuwa na kipaji kikubwa alizaliwa katika mji wa Tabriz ulioko kaskazini magharibi mwa Iran. Mshairi huyu alizaliwa katika familia iliyosifika kwa fadhila na heshima. Baba yake ni Yusuf I’tisam al-Mulk aliyekuwa mmoja wa watarjumi na waandishi watajika katika zama zake. Parvin alijifunza fasihi ya Iran na ya Kiarabu kwa baba yake na alionyesha kipaji cha hali ya juu cha mashairi tangu akiwa mdogo.
Katika kipindi chote cha masomo, Parvin I’tisami alikuwa mwanafunzi bora shuleni. Safari zote alizifanya akiwa pamoja na baba yake na kujifunza mambo mengi katika safari hizo.

Katika siku kama ya leo miaka 40 iliyopita Mahdi Bakeri mmoja wa makamanda mashujaa na wenye tadibiri katika kipindi cha kujihami kutakatifu wanananchi wa Iran mbele ya hujuma na mashambulio ya kichokozi ya jeshi la dikteta wa wakati huo wa Iraq Saddam Hussein alikufa shahidi.
Alizaliwa katika mji wa Miandoab kaskazini magharibi mwa Iran na mama yake alifariki dunia wakati yeye akiwa mtoto mdogo. Kaka yake naye kutokana na kuonyesha upinzani dhidi ya utawala dhalimu wa Shah aliuawa na makachero wa utawala huo.

Katika siku kama ya leo miaka 36 iliyopita, utawala wa Baath nchini Iraq uliushambulia bila huruma na kwa mabomu ya kemikali za sumu mji wa Halabja wa wakazi wa Kikurdi huko kaskazini mashariki mwa nchi hiyo kwa kutumia makumi ya ndege za kivita.
Hujuma hiyo ilianza baada ya kushindwa kupambana na wapiganaji Waislamu wa Iran na wa Kikurdi wa huko Iraq, na katika upande wa pili wananchi Waislamu wa Halabja waliwakaribisha wapiganaji wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kutokana na dhulma na ukandamizaji usio na kipimo wa Saddam Hussein dhidi yao.
Raia elfu tano wasio na hatia waliuawa kutokana na kuvuta gesi ya sumu huko Halabja. Hata hivyo nchi za Magharibi hazikuchukua hatua yoyote kwa jinai hiyo kubwa na ya kutisha.

Katika siku kama hii ya leo miaka 36 iliyopita ardhi ya Taba huko kaskazini mashariki mwa Misri ilikombolewa baada ya kukaliwa kwa mabavu kwa miaka kadhaa na utawala ghasibu wa Israel.
Utawala wa Kizayuni ulilikalia kwa mabavu jangwa la Sinai katika vita vya mwaka 1967, ambalo upande wa mashariki mwake linapatikana eneo la Taba. Utawala wa Tel Aviv ulikubali kuirejeshea Misri jangwa la Sinai baada ya kusaini mkataba wa Camp David mwaka 1987.
Israel iliendelea kulikalia kijeshi eneo muhimu la Taba huko kaskazini mwa Ghuba ya Aqaba, licha ya utawala huo wa Kizayuni kuondoka katika baadhi ya sehemu za jangwa hilo.
