Jumatano, Agosti 3, 2016
Leo ni Jumatano tarehe 29 Shawwal 1436 Hijria sawa na Agosti 3, 2016
.Miaka 38 iliyopita katika siku kama ya leo, katika hatua yake nyingine ya kigaidi utawala wa Kizayuni wa Israel uliwauwa Izzuddin Qalq mjumbe wa Harakati ya Ukombozi wa Palestina (PLO) na naibu wake huko Paris, Ufaransa. Shirika la ujasusi la utawala wa Kizayuni wa Israel MOSSAD katika miongo miwili ya 70 na 80 liliwauwa kigaidi viongozi wengi wa PLO ili kuidhoofisha harakati hiyo na kuilazimisha kuanzisha mazungumzo eti ya mapatano kati ya Wapalestina na Israel.
Katika siku kama ya leo miaka 102 iliyopita, meli ya kwanza ilipita katika Kanali ya Panama na kwa utaratibu huo, kanali hiyo ikawa imefunguliwa. Wahandisi wa Kifaransa ndio walioanza kujenga mfereji huo wa Panama na baadaye Wamarekani walikamilisha kazi hiyo. Kujengwa mfereji huo wenye urefu wa kilomita 68, kuliunganisha bahari mbili za Pacifi na Atlantic.
Siku kama ya leo miaka 524 iliyopita, ilianza safari kubwa zaidi ya uvumbuzi ya baharia wa Kiitalia Christopher Columbus. Christopher Columbus alipewa jukumu la kuvumbua njia mpya ya kuelekea India katika makubaliano yaliyofikiwa kati yake na mfalme na malkia wa Uhispania wa wakati huo. Kwa sababu hiyo Christopher Columbus aliondoka katika bandari ya Paulus huko Uhispania akiwa na meli tatu na mabaharia 120 na hatimaye walifika katika nchi kavu baada ya kuwa baharini kwa siku 33. Wakati huo Columbus na wenzake walidhani kuwa wamewasili India lakini walikuwa wamevumbua bara America bila ya wao kujua.
Na tarehe 13 Mordad miaka 86 alizaliwa Sayyid Ali Sistani, faqihi, mwanazuoni na marejeo ya Waislamu wa Kishia. Sayyid Sistani alizaliwa katika mji mtakatifu wa Mash'had huko kaskazini mwa Iran na alianza kusoma Qur'ani tukufu akiwa na umri wa miaka mitano. Baada ya kupata elimu ya msingi ya masomo ya kidini, Ayatullah Ali Sistan alielekea kwenye mji mtakatifu wa Qum kwa ajili ya elimu zaidi na kujifunza kwa maulama wakubwa wa mji huo. Mwaka 1331 Hijria Shamsia alielekea katika mji mtakatifu wa Najaf huko Iraq kwa ajili ya elimu ya juu zaidi na kupata elimu kwa maulama wa mji huo hususan Ayatullahil Udhma Sayyid Abul Qaim al Khui. Kwa sasa Ayatullah Sistan anahesabiwa kuwa miongoni mwa marjai na wanazuoni wakubwa nchini Iraq na amekuwa na mchango muhimu katika kuimarisha umoja na mshikamano wa Waislamu hususan katika mapambano dhidi ya uvamizi wa Marekani na mashambulizi ya kundi la kigaidi la Daesh nchini humo.