Apr 20, 2025 02:25 UTC
  • Jumapili, Aprili 20, 2025

Jumapili tarehe 21 Mfunguo Mosi Shawwal 1446 Hijria inayosadifiana na tarehe 20 Aprili 2025.

 Miaka 1354 iliyopita katika siku inayosadifiana na ya leo, ardhi ya Andalusia huko Uhispania ya leo ilidhibitiwa na jeshi la Kiislamu lililoongozwa na Tariq bin Ziyad.

Tariq ambaye alikuwa na wapiganaji karibu ya elfu 12, alivuka kwa boti mlango bahari ulioko kati ya Morocco na Uhispania ambao umepewa jina lake Tariq bin Ziad au "Gibraltar". Tariq bin Ziyad aliamuru kochomwa moto boti zote zilizotumiwa na wapiganaji wake kuvukia lango bahari na Gibralta ili kuwahamasisha zaidi kupigana na maadui.

Katika kipindi cha karne 8 za utawala wao huko Andalusia, Waislamu walianzisha vituo mbalimbali vya utamaduni na taasisi za kiuchumi na kwa kipindi kirefu ardhi hiyo ilikuwa kituo kikuu cha ustaarabu wa Kiislamu barani Ulaya.   *

Katika siku kama hii ya leo miaka 1092 iliyopita, alifariki dunia Ibn Habban, mtaalamu wa hadithi, elimu ya fiq'hi na mwanahistoria mashuhuri wa karne ya 14 Hijiria.

Alipata elimu ya msingi kwa walimu mashuhuri wa zama zake na kisha akaelekea Neishabur kaskazini mwa mashariki mwa Iran, ambao katika kipindi hicho ulikuwa ni moja ya vituo muhimu vya kielimu. Ibn Habban anahesabika kuwa mtu mwenye nadharia muhimu katika elimu ya hadithi.

Miongoni mwa athari muhimu za msomi huyu mkubwa ni pamoja na kitabu cha"At-Thuqat" na Rawdhatul-Uqalaai wa Nazahatul-fudhalaai."   

Siku kama ya leo tarehe 20 Aprili miaka 223 iliyopita Mawahabi wa Hijaz (Saudi Arabia) walishambulia mji mtakatifu wa Karbala nchini Iraq na kuua mamia ya Waislamu wa madhehebu ya Shia.

Baada ya mawahabi kushika hatamu za uongozi huko Hijaz mwanzoni mwa karne ya 19 walianzisha mashambulizi ya mara kwa mara ya kundi hilo lenye misimamo na fikra za kuchupa mipaka dhidi ya Waislamu wengine hususan wafuasi wa Watu wa Nyumba ya Mtume wetu Muhammad (saw) na miongoni mwa mashambulizi ya mawahabi hao ni yale ya kushambulia miji mitakatifu ya Karbala na Najaf nchini Iraq tarehe 20 Aprili mwaka 1802. Miji hiyo ambayo ni mitakatifu hususan kwa Waislamu wa madhehebu ya Shia kutokana na kuwa na makaburi ya watu wa kizazi cha Mtume wetu Muhammad (saw), imekuwa ikilengwa na mawahabi.

Katika mashambulizi hayo mawahabi walishambulia haram ya mjukuu wa Mtume, Imam Hussein bin Ali mwana wa Bibi Fatima (as) huko Karbala na kuvunja quba na kaburi na mtukufu huyo na kisha wakapora mali iliyokuwa hapo. Waislamu zaidi ya elfu mbili waliuawa katika shambulizi hilo la mawahabi. Mashambulizi hayo yaliwakasirisha sana Waislamu katika maeneo mbalimbali ya dunia na kuzidisha chuki yao dhidi ya mawahabi na mafundisho ya kundi hilo potofu. Mawahabi waliendeleza mauaji ya Waislamu wa madhehebu ya Shia na madhehebu nyinginezo baada ya kuanzishwa dola la watawala  wa kizazi cha Aal Saud huko Saudi Arabia na walishambulia na kuharibu Haram ya wajukuu wa Mtume Muhammad (saw) na za masahaba zake wakubwa katika makaburi ya Baqii mjini Madina.   

Miaka 26 iliyopita, katika siku kama ya leo, kulitokea maafa makubwa ya mashambulizi yaliyofanywa na wanafunzi wawili wa Kimarekani kwenye shule moja ya sekondari.

Wanafunzi hao waliwamiminia risasi na kuwaua wanafunzi wenzao 12 na mwalimu wao na kuwajeruhi wengine 21. Wanafunzi hao waliovamia shule ya Columbine High School iliyoko Denver, katika jimbo la Colorado, walijiua wenyewe baada ya kufanya mauaji hayo.

Mauaji kama hayo ya kutisha yamekuwa yakitokea mara kwa mara katika maeneo ya umma nchini Marekani. Wataalamu wanasema kuuwa, uhuru wa kununua na kumiliki silaha ni miongoni mwa sababu za maafa hayo yanayotokea kila mwaka nchini Marekani.