Jumatatu, tarehe 21 Aprili, 2025
Leo ni Jumatatu tarehe 22 Shawwal 1446 Hijria sawa na Aprili 21 mwaka 2025.
Leo tarehe Mosi Ordibehesht katika kalenda ya mwaka wa Hijria Shamsia ni siku ya kumuenzi Sheikh Muslihuddeen Saadi Shirazi malenga, mshairi na mwalimu stadi wa tungo za mashairi na nathari wa Kifarsi.
Saadi Shirazi alizaliwa karibu mwaka 606 Hijria Qamariya katika familia ya kielimu kwenye mji wa Shiraz ulioko kusini mwa Iran, na baada ya kukipitisha kipindi cha utoto na kuinukia kwake katika mji alikozaliwa wa Shiraz, akiwa kijana, Saadi aliamua kwenda katika mji wa Baghdad huko Iraq.
Akiwa huko alisoma katika shule ya Nidhamiya na baadaye kufanya safari katika maeneo ya Sham, Hijaz, Roma na maeneo mengine ya dunia. Katika safari zake hizo, malenga huyo mashuhuri alifanikiwa kufahamiana na jamii mbalimbali na kuona mengi yaliyoimarisha kipawa chake cha kutunga mashairi.
Saadi Shirazi ni miongoni mwa malenga na washairi wakubwa katika ulimwengu wa Kiislamu. Saadi Shirazi ameandika vitabu kadhaa, muhimu zaidi ni kile cha tungo cha Bustan na kitabu chake cha nathari cha Golestan.

Siku kama ya leo miaka 1196 iliyopita, Egbert Mfalme wa Kwanza wa Uingereza alichukua madaraka baada ya vita vya muda mrefu.
Kabla ya hapo Uingereza ilikuwa ikiongozwa na wafalme wa kiukoo ikiwa imegawika katika sehemu kadhaa za kijiografia, na kila mtawala akitawala eneo lake maalumu.
Egbert aliyekuwa mfalme wa Wessex, eneo lililokuwa Kusini mwa Uingereza ya sasa, baada ya kupambana na watawala wa kitabaka na kuwashinda, mwaka 829 alifanikiwa kuingia madarakani akiwa Mfalme wa Kwanza wa Uingereza na kuasisi silsila ya utawala wa Wasaxoni wa Magharibi.

Katika siku kama ya leo miaka 87 iliyopita, Allamah Muhammad Iqbal Lahori mwanafikra, mwanafalsafa na malenga wa Kiislamu aliaga dunia huko Bara Hindi.
Alizaliwa mwaka 1873 katika mji wa Sialkot kwenye jimbo la Punjab. Baada ya kumaliza masomo ya awali na ya juu na kupata shahada ya uzamili, Allamah Muhammad Iqbal Lahori alielekea nchini Ujerumani na baadaye Uingereza kwa lengo la kujiendeleza katika elimu ya falsafa na kubaki huko kwa kipindi cha miaka minne.
Malenga huyo alianza kutunga mashairi akiwa katika masomo yake ya sekondari. Baada ya kurejea India, Iqbal Lahori alianza kuwaamsha Waislamu wa nchi hiyo na kufanya jitihada za kuwaunganisha pamoja huku akibainisha fikra na mitazamo yake kupitia beti za mashairi.
Mwanafalsafa huyo anahesabiwa kuwa mmoja wa waanzilishi na waasisi wa Pakistan huru.

Na siku kama ya leo miaka 45 iliyopita aliaga dunia Sohrab Sepehri malenga na mchoraji mashuhuri wa Kiirani.
Sohrab alizaliwa mwaka 1307 Hijria Shamsiya katika mji wa Kashan katikati mwa Iran. Awali malenga huyo wa Kiirani alianza kufundisha na baada ya hapo alijiunga na taaluma ya sanaa. Vilevile alikuwa na kipaji kikubwa katika masuala ya uchoraji.
Kazi za malenga na mchoraji huyo wa Kiirani zilimpatia tuzo na zawadi nyingi katika maonyesho mbalimbali yaliyofanyika ndani na nje ya Iran. Diwani ya kwanza ya mashairi ya Sepehri ilichapishwa mwaka 1330 Hijria Shamsiya kwa jina la "Kifo cha Rangi" (The Death of Colour).
