Ijumaa, tarehe 25 Aprili, 2025
Leo ni Ijumaa tarehe 26 Shawwal 1446 Hijria sawa na Aprili 25 mwaka 2025.
Siku kama ya leo miaka 533 serikali ya mwisho ya Kiislamu barani Ulaya ilisambaratika huko Granada.
Baada ya kudhihiri dini ya Uislamu na kupanua mamlaka yake katika maeneo ya Asia na kaskazini mwa Afrika, jeshi la Waislamu liliingia kusini magharibi mwa Ulaya kupitia lango bahari la Jabal Tariq (Gibraltar) na kulitawala eneo hilo kwa kipindi cha karne 8. Eneo hilo ambao kwa sasa linaitwa Uhispania, wakati huo lilijulikana kwa jina la Andalusia.
Katika kipindi cha ustawi wa ustaarabu wa Kiislamu eneo la Granada lilikuwa kituo kikuu cha ustaarabu huo na makao makuu ya kueneza Uislamu hususan barani Ulaya.
Dola la Kiislamu la Andalusia liliangushwa kupitia njia ya kueneza ufuska na maovu baina ya watawala na makhalifa wa wakati huo.

Miaka 127 iliyopita katika siku kama ya leo, serikali ya Marekani ilitangaza vita dhidi ya Uhispania.
Kabla ya hapo, Marekani ilikuwa imeitaka Uhispania ilipatie ufumbuzi suala la Cuba kupitia njia za amani. Baadhi ya Wacuba kwa miaka mingi walikuwa wakipigania mamlaka ya kujitawala na mara kadhaa walifanya majaribio ya mapinduzi na kuendesha mapigano ya silaha. Kulipuka manowari ya kijeshi ya Marekani ya Maine katika maji ya Cuba, kilikuwa kisingizio kizuri kwa Marekani cha kuingia katika vita dhidi ya Uhispania.
Katika vita hivyo vilivyoanza tarehe 25 Aprili hadi Agosti 12 mwaka 1898 vilimalizika kwa kushindwa Uhispania; na kwa mujibu wa mkataba wa Paris ardhi za Ufilipino, Ouerto Rico, Guam na Cuba zipatiwa Marekani.

Miaka 54 iliyopita katika siku kama ya leo, Wamarekani laki mbili walifanya maandamano mjini Washington wakiendeleza upinzani wao dhidi ya mashambulizi ya nchi hiyo huko Vietnam.
Maandamano hayo yalikuwa miongoni mwa vielelezo vikubwa vya upinzani wa wananchi wa Marekani dhidi ya siasa za kichokozi za serikali ya nchi hiyo huko Vietnam.
Katika vita vya Vietnam vilivyoanza mwaka 1964 Marekani ilituma askari laki tano nchini humo ambako maelfu miongoni mwao waliuawa na wengine wengi kujeruhiwa.
Kwa sababu hiyo wananchi wa Marekani walizidisha upinzani dhidi ya vita hivyo na mwaka 1975 Marekani ililazimika kufunga virago na kuondoka Vietnam kutokana na mashinikizo ya ndani na ya kimataifa na kushindwa mara kwa mara jeshi la nchi hiyo katika medani za vita.

Na siku kama ya leo miaka 45 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 5 Ordibehesht mwaka 1359 Hijiria Shamsia, Marekani ilishambulia kijeshi ardhi ya Iran kwa kutumia helikopta na ndege kadhaa za kivita.
Serikali ya Marekani ilifanya mashambulizi hayo baada ya kushindwa njama zake za kutaka kuuangusha mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu wa Iran.
Lengo la mashambulio hayo lilikuwa ni kutaka kuwakomboa majasusi wake waliotiwa mbaroni wakati wa kutekwa ubalozi wa Marekani hapa nchini uliokuwa pango la kijasusi.
Licha ya kuweko mipango makini, kutumiwa vyombo vya kisasa kabisa na mazoezi mengi yaliyofanywa katika eneo linalofanana na hilo ili kuhakikisha operesheni hiyo inafanikiwa, lakini mashambulizi hayo yalikatishwa na tufani kubwa ya mchanga iliyotokea Tabas na kupelekea kuanguka baadhi ya ndege, kushika moto helikopta za Marekani na kufa baadhi ya askari wa nchi hiyo huku waliobakia wakiikimbia ardhi ya Iran.
