May 05, 2025 02:21 UTC
  • Jumatatu, 5 Mei, 2025

Leo ni Jumatatu 7 Dhulqaadah 1446 Hijria mwafaka na 5 Mei 2025.

Leo tarehe 15 Ordebehesht Hijiria Shamsia ni siku ya kumuenzi Sheikh Swaduq, msomi mashuhuri wa Kiislamu.

Abu Ja'far Muhammad Ibn Ali ibn Babawayh maarufu kwa jina la Sheikh Swaduq alizaliwa katika eneo la Qum nchini Iran yapata mwaka 306 Hijiria katika familia ya wasomi. Akiwa kijana mdogo alianza kujifunza elimu za dini ya Kiislamu na kufanikiwa kukwea daraja za elimu kutoka kwa baba yake na maulama wengine wa zama zake. Baada ya hapo alifikia daraja za juu katika elimu, na kufanya safari katika maeneo tofauti kwa ajili ya kutafuta elimu zaidi na kukusanya Hadithi. Inaelezwa kuwa alipata kusoma kwa wasomi zaidi ya 200 wa zama zake. 

Miongoni mwa wanafunzi wake ni pamoja na Sheikh Al-Mufid, Hassan Bin Muhammad Qumi, Alamul-Huda, Sayyid Murtadha, na wengine wengi. Sheikh Swaduq ameacha athari nyingi ambazo miongoni mwazo ni 'Man laa Yahdhuruhul Faqihi chenye juzuu nne ambacho ni kati ya vitabu mashuhuri vya hadithi kwa Waislamu wa madhehebu ya Shia. Kitabu hicho kina Hadithi 6000. Vitabu vyake vingine mashuhuri ni 'Madinatul-Ilm' chenye juzuu 10, 'Al Aamaali, al Khiswaal', 'Uyunu Akhbaar al-Ridha (as)' na 'Ilalu al Sharai'.  

Miaka 730 iliyopita katika siku kama ya leo alifariki dunia Ibn Baswis mtaalamu wa kaligrafia maarufu kwa jina la Damashqi. 

Alizaliwa mwaka 651 Hijiria katika mji wa Damascus na kwa muda wa miaka 50 alijishughulisha kufundisha hati na wakaazi wa mji huo walistafidi kwa elimu na sanaa kutoka kwake.

Ibn Baswis aliandika hati kwa mitindo tofauti ya kupendeza na katika umri wake wa uzeeni aliandika nakala ya Qur'ani Tukufu kwa kutumia maji ya dhahabu na kwa hati nzuri na za kuvutia. Qur'ani hiyo pamoja na athari nyingine za Ibn Basis bado ziko hadi leo. 

Siku kama ya leo miaka 207 iliyopita, alizaliwa Karl Heinrich Marx mwanafalsafa wa Kijerumani na mwasisi wa nadharia ya Umaksi.

Karl Marx awali alianza kusomea taaluma ya sheria na baadaye historia na falsafa. Mwanafalsafa huyo wa Kijerumani kwa muda fulani alikuwa mkuu wa jarida moja na mwaka 1848 alishirikiana na mwanafalsafa mwenzake wa Kijerumani na kubainisha imani, maoni na mitazamo yake katika kitabu alichokipa jina la "Manifesto ya Ukomonisti."

Miaka miwili baadaye Marx alibaidishwa kutokana na kujishughulisha na harakati za kisiasa na hadi mwishoni mwa maisha yake makazi yake yalikuwa nchini Uingereza.  

Karl Marx

Siku kama ya leo miaka 204 iliyopita, alifariki dunia Napoleon Bonaparte mfalme aliyekuwa na nguvu wa Ufaransa, akiwa uhamishoni.

Napoleon alizaliwa mwaka 1769 na kuchukua madaraka makubwa ya uongozi baada ya mapinduzi ya Ufaransa mwaka 1789, ambapo aliifanya nchi hiyo ishinde vita na nchi nyingi za Ulaya.

Baada ya kuwa mfalme wa Ufaransa, Napeleon alibadilika na kuwa mtawala aliyependa kujitanua na kuzivamia nchi nyingine katika maeneo mbalimbali duniani. Kwa ajili hiyo katika kipindi cha utawala wake alipigana vita kadhaa na nchi nyingine na kukalia kwa mabavu maeneo mengi ya bara Ulaya. 

Napoleon Bonaparte

Miaka 44 iliyopita katika siku kama ya leo alifariki dunia Bobby Sands mwanamapambano maarufu wa Ireland baada ya kukaa katika jela ya Uingereza kwa wiki kadhaa na kugoma kula chakula kwa muda wa siku 66 katika kupigania uhuru wa Ireland ya Kaskazini.

Serikali ya kikoloni ya Uingereza ilikabiliwa na wimbi kubwa la malalamiko kutoka ndani na nje ya nchi hiyo kufuatia kifo cha Bobby Sands na wanaharakati wenzake wa Ireland ambao waligoma kula chakula wakiwa katika jela za nchi hiyo. ***

Katika siku kama ya leo miaka 81 iliyopita, hayati Imam Ruhullah Khomeini akiwa na umri wa miaka 42, alitoa taarifa yake ya kwanza ya kisiasa akiwataka wananchi kusimama na kuanza harakati kwa ajili ya Mwenyezi Mungu.

Katika taarifa hiyo Imam Khomeini alichunguza hali ya miaka ya nyuma, ya kipindi hicho na mustakbali wa wananchi wa Iran na Waislamu kwa ujumla na kusema: "Kuanza harakati na mapambano kwa ajili ya Mwenyezi Mungu ndiyo njia pekee ya kurekebisha hali ya dunia." Alisema suala hilo ndiyo falsafa ya kutumwa Manabii wote wa Mwenyezi Mungu.

Imam pia alieleza sababu za hali mbaya ya Waislamu na wananchi wa Iran na kukumbusha majukumu mazito ya wanazuoni wa dini na athari mbaya za tabaka hilo kughafilika na masuala ya kisiasa. Katika taarifa hiyo Imam Khomeini alipiga kengele ya hatari na kuwaamsha Waislamu husuan wanafunzi wa vyuo vya kidini kuhusu umuhimu wa kusimama na kuanza mapambano ya kurekebisha umma.   

Na tarehe 5 Mei imetangazwa na Shirika la Afya Duniani (WHO) na Shirikisho la Kimataifa la Wakunga kuwa ni ya Siku ya Kimataifa ya Wakunga.

Siku hiyo ilipendekezwa kwa mara ya kwanza kuwa Siku ya Kimataifa ya Wakunga mwaka 1980 na kutangazwa rasmi mwaka 1992.

Lengo la kuainishwa siku hii ni kuwaenzi wakunga na kazi ya ukunga, kuzidisha uelewa na kubadilishana maarifa na taarifa zinazohusiana na afya ya akina mama na watoto wachanga na vilevile kuonyesha umuhimu wa kazi za wakunga.