May 15, 2025 03:06 UTC
  • Alkhamisi, tarehe 15 Mei, 2025

Leo ni Alkhamisi tarehe 17 Dhilqaada 1446 Hijria sawa na tarehe 15 Mei mwaka 2025.

Siku kama ya leo miaka 1267 iliyopita Imam Mussa al Kadhim (as) ambaye ni miongoni mwa Ahlubait wa Mtume wetu Muhammad (saw) alibaidishwa kutoka Madina na kupelekwa Iraq kwa amri ya mtawala dhalimu, Haroun Rashid.

Mtukufu huyo aliwasili Iraq tarehe 7 Dhilhijja 179 Hijria na kufungwa katika jela mji huo. Kwa muda, Imam aliwekwa katika jela ya Issa bin Ja'far aliyekuwa mtawala wa Basra, lakini mtawala huyo alimwandikia barua Haroun Rashid akimuomba amkabidhi Imam kwa mtu mwingine kwa sababu hakupata ushahidi wowote dhidi ya mtukufu huyo.

Haroun Rashid alimpeleka tena uhamishoni Imam mjini Baghdad na akamtaka waziri wake, Fadhl bin Rabii amuue mjukuu huyo wa Mtume. Waziri huyo alikataa na hivyo Haroun alimtaka mtu aliyejulikana kwa jina la Yahya bin Khalid Barmaki atekeleze amri hiyo.

Hatimaye Imam Kadhim (as) aliuuliwa shahidi na muovu huyo kwa amri ya mtawala Haroun Rashid.   ***

Tarehe 15 Mei miaka 249 iliyopita katika siku kama hii ya leo ilitengenezwa meli ya kwanza yenye kutumia mvuke.

Meli inayotumia nishati ya mvuke ilitengenezwa miaka 70 baada ya kuvumbuliwa nishati ya mvuke na mhandisi wa Kifaransa Denis Papin.

Utumiaji wa nishati ya mvuke katika meli ulileta mabadiliko makubwa katika sekta ya usafiri wa baharini.    ****

Miaka 166 iliyopita katika siku kama hii ya leo alizaliwa Pierre Curie msomi na mwanafizikia wa Ufaransa.

Kipaji cha masomo ya hesabati na fizikia alichokuwa nacho kilianza kuonekana tokea ujana wake, na hatimaye kuibuka kuwa mtafiti mkubwa katika nyanja hizo. Mwaka 1898 mwanafizikia huyo wa Kifaransa alifanikiwa kugundua Radium akisaidiana na mkewe Bi. Marie Pierre.

Pierre Curie aliaga dunia mwaka 1906.   ***

Siku kama ya leo tarehe 15 Mei 1919, Izmir moja kati ya miji ya kihistoria na muhimu nchini Uturuki, ulitekwa na wanajeshi wa Mustafa Kamal Pasha, mwasisi wa Jamhuri ya Uturuki, baada ya kujiri mapigano yaliyopelekea kuuawa watu wengi.

Mji wa Izmir uko magharibi mwa Uturuki, na harakati ya Warepublican ya Uturuki ilianziwa katika mji huo wa kihistoria.   ***

 

Vita Vikuu vya Pili vya Dunia

Miaka 85 iliyopita katika siku kama ya leo, yaani tarehe 15 Mei mwaka 1940, jeshi la Ujerumani liliivamia na kuikalia kwa mabavu nchi ya Uholanzi baada ya shambulio kubwa lililodumu kwa siku 5 katika Vita Vikuu vya Pili vya Dunia.

Wanajeshi wa Kinazi wa Ujerumani walianza kuzishambulia nchi za Ufaransa, Ubelgiji, Uholanzi na Luxemburg huko magharibi mwa Ujerumani tarehe 10 Mei na kufanikiwa kuzidhibiti nchi zote hizo. Uholanzi ilijipatia uhuru wake mwaka 1945.     ***

Siku kama ya leo miaka 91 iliyopita alifariki dunia Ayatullahil Udhma Sheikh Abdulkarim Hairi Yazdi fakihi na mwanazuoni mkubwa wa Kiislamu ambaye aliasisi Hauza na taasisi ya kielimu ya vyuo vikuu vya kidini yya Qum.

Alimu huyo alizaliwa katika mji wa Yazd katikati mwa Iran na baada ya kupata elimu ya mwanzo alielekea nchini Iraq ili kuendelea na masomo ambako alipata elimu na maarifa kutoka kwa maulamaa maarufu wa zama hizo na kufikia daraja ya juu ya ijitihad.

Ayatullahil Udhma Sheikh Abdulkarim Hairi Yazdi

 

Ayatullah Hairi Yazdi aliporejea Iran alihisi haja ya kuwepo taasisi yenye nguvu ya elimu ya dini na kwa minajili hiyo mwaka 1340 Hijiria Shamsia alinzisha Hauza ya Qum ambayo katika mji mtakatifu wa Qum. Hauza ya Qum ilipanuka kwa kasi na hivi sasa ni miongoni mwa vituo muhimu vya elimu katika ulimwengu wa Kiislamu.  **

Siku kama ya leo miaka 32 iliyopita, Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa liliitangaza Mei 15 kuwa Siku ya Kimataifa ya Familia.

Uamuzi huo ulichukuliwa kutokana na umuhimu wa familia na asasi hii tukufu ambayo inahesabiwa kuwa msingi mkuu wa jamii na lengo ni kuilinda familia na madhara ya nje na ya ndani na kuifanya iwe na mchango na nafasi bora zaidi. Asasi ya familia ilikuweko tangu wakati wa kudhihiri mwanadamu na imeendelea kuwa nguzo kuu ya jamii. Mke na mume na watoto na wakati mwingine bibi na babu ni watu wanaounda familia hii.

Familia ni mahala tulivu kwa wenza, sehemu ya kulea na kukuza watoto na ni mazingira yenye amani kwa ajili ya wanafamilia kuwa na mawasiliano salama.  ****