May 19, 2025 04:56 UTC
  • Jumatatu, 19 Mei, 2025

Leo ni Jumatatu 21 Dhul-Qaadah 1446 Hijria mwafaka na 19 Mei 2025.

Siku kama ya leo miaka Miaka 504 iliyopita, majeshi ya utawala wa kifalme wa Othmania yaliuteka mji muhimu wa Belgrade, uliokuwa mji mkuu wa Yugoslavia ya zamani.  

Mwishoni mwa karne ya 14 Utawala wa Othmania ulianza kusonga mbele katika eneo la Balkan na kuweza kulitawala karibu eneo lote hilo.

Miaka 20 baadaye yaani mwaka 1541 utawala huo uliweza pia kuyadhibiti maeneo ya Hungary.

Siku kama ya leo miaka 263 iliyopita, alizaliwa katika familia masikini Johann Gottlieb Fichte mwanafalsafa wa Kijerumani.

Johann alikuwa mmoja wa waasisi wakuu wa harakati ya kifalsafa iliyojulikana kama "German Idealism", harakati ambayo ilitokana na maandiko ya kinadharia na kimaadili ya rafiki yake Immanuel Kant.

Johann Gottlieb Fitche aliathiriwa sana kinadharia na mwanafalsafa mwenzake huyo na kumkabidhi baadhi ya kazi zake. Johann Fitche ameandika vitabu vingi muhimu ambapo baadhi ni vile alivyovipa majina  ya Foundations of Nature Right, Mustakabali wa Binadamu na makala ya The Way Towards the Blessed Life.

Johann Gottlieb Fichte

Siku kama ya leo miaka 100 iliyopita, alizaliwa Malcolm X, kiongozi wa harakati za kupigania uhuru Wamarekani wenye asili ya Afrika.

Malcolm X alizaliwa katika familia masikitini na akiwa na umri wa miaka minne, alishuhudia kijiji chao kikiteketezwa kwa moto na watu wa jamii ya Ku Klux Klan kutokana na mashambulizi ya kibaguzi. Baadaye alienda kujiunga na shule ya kutwa. Hata hivyo hakuweza kukamilisha masomo kutokana na umasikini, hivyo alilazimika kufanya kazi katika mgahawa mmoja ambapo alijikuta akitumbukia katika utumiaji wa dawa za kulevya na unyang’anyi.

Kufuatia hali hiyo akiwa na umri wa miaka 21 alihukumiwa kifungo cha miaka mitano jela kutokana na hali hiyo. Akiwa jela alifahamiana na wafungwa wengi wenye asili ya Kiafrika waliotokana na familia za Kiislamu kama ambavyo pia alikuwa na mahusiano na Elijah Muhammad, kiongozi wa harakati ya siri ya Wamarekani weusi. Mahusiano na kiongozi huyo yaliendelea hata baada ya Malcolm X kutoka jela.

Baada ya hapo alianza kusoma na kufanya utafiti mwingi kuhusiana na Uislamu ambapo kwa msaada wa Waislamu alifanikiwa kujenga misikiti miwili katika mji wa Detroit, Philadelphia nchini Marekani.

Malcolm X

Siku kama ya leo miaka 90 iliyopita, Thomas Edward Lawrence mwanasiasa na afisa wa ujasusi wa Uingereza alifariki dunia katika ajali ya gari.

Lawrence alizaliwa mwaka 1888 Miladia. Katika kipindi cha miaka kati ya 1910 na 1914, mwanasiasa huyo wa Uingereza aliwakilisha kamati ya masuala ya akiolojia (elimu kale) na pia kuhudumu huko Iraq, Syria na Palestina.

Aidha alikuwa mfanyakazi wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Uingereza na mwaka 1916 aliteuliwa kuwa mkuu wa idara ya ujasusi ya jeshi la Uingereza nchini Misri.

Thomas Edward Lawrence alichangia pakubwa kuingia madarakani kwa wafalme Fadhil huko Syria, Abdallah nchini Jordan na Mfalme Abdulaziz huko Saudi Arabia.

Thomas Edward Lawrence

Siku kama ya leo miaka 89 iliyopita, rada ilivumbuliwa na Robert Watson Watt mvumbuzi wa Kiingereza.

Kifaa hicho ambacho ni muhimu kinachotumiwa katika ugunduzi na utambuzi kwenye oparesheni mbalimbali za kijeshi na kiraia, kwa mara ya kwanza kilitumika katika mojawapo ya viwanja vya ndege vya Uingereza.

Rada ilihesabiwa kama chombo muhimu cha kutoa tahadhari katika Vita vya Pili vya Dunia na hivi sasa kinatumika katika masuala mbalimbali.

Robert Watson Watt