Aug 05, 2016 08:45 UTC
  • Maswali Yetu na Majibu ya Thaqalain (132)

Assalaam Aleikum wapenzi wasikilizaji na karibuni kutegea sikio sehemu ya 132 katika mfululizo huu wa vipindi vya Maswali Yetu na Majibu ya Thaqalain, ambavyo hukujieni kupitia Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kislamu ya Iran inayokutangazieni kutoka hapa mjini.

Katika kipindi cha leo tutamalizia kujibu swali ambalo tumekuwa tukilijadi katika vipindi viwili vilivyopita ambalo linasema: Je, aya inayozungumzia kukamilika dini na kutimizwa neema ya Mwenyezi Mungu kwa waja wake inathibitisha Uimamu wa Imam Ali (as) peke yake au pia inathibitisha Uimamu wa Maimamu wengine wote wa kizazi cha Nyumba ya Mtume (saw)?

Tulifahamu baada ya kuzingatia na kutafakari kwa kina maana ya aya ya 67 ya Surat al-Maida kwamba Mwenyezi Mungu alimuamuru Mtume wake (saw) katika Hija yake ya mwisho kuwafikishia Waislamu ujumbe ambao alikuwa amemteremshia, ujumbe ambao ulikuwa na umuhimu mkubwa  wa kukamilishwa dini na kuwa moja ya nguzo zake, kwa kadiri kwamba kama hangefikisha na kuwatangazia ujumbe huo basi ni kana kwamba hangekuwa amefikisha asili ya ujumbe uliotumwa nao na MwenyeziMungu kuwafikishia wanadamu, na hivyo kutokamilika dini tukufu ya Uislamu. Tangazo la ujumbe huo muhimu wa Mtume Muhammad (saw) lilitimia kupitia hadithi ya baia’ ya al-Ghadir ambayo imabeinishwa maana yake na zaidi ya masahaba 100 kwenye vitabu vya Ahlu Sunna pekee na Tabari kuthibitisha suala hilo katika kitabu chake mashuhuri cha al-Wilayat fi Twariq Hadith al-Ghadir ambapo anasema kuwa hadithi hii imepokelewa na kunukuliwa na wanazuoni wengi wa Kisuni wakiwemo as-Suyuti, al-Jazari, ad-Dhahabi, Ibn Kathir na wengine wengi.

Tuliona katika kipindi kilichopita kwamba hadithi ya Ghadir ilijumuisha kutangazwa kwa Uimamu na ukhalifa wa Imam Ali al-Murtadha (as) baada ya Mtume Mtukufu (saw). Hadithi hiyo ya Thaqalain ambayo ilijumuisha maneno ya Mtume (saw) yanayosema: ‘Yule ambaye mimi ni Maula wake basin a huyu Ali ni Maula wake, pia ilizungumzia Uimamu wa Maimamu wengine wotaharifu wa Nyumba ya Mtukufu Mtume (saw). Tulikunukulieni hadithi hiyo katika kipindi kilichopita kupitia vyanzo vya Ahlu Sunna ambapo katika kipindi cha leo tutazungumzia vyanzo vya madhehebu ya Watu wa Nyumba ya Mtume (saw) ambavyo vinazungumzia tukio na hadithi hiyo kwa uwazi zaidi. Endeleeni kuwa pamoja nasi

 

Ndugu wasikilizaji, tutakunukulieni hivi punde baadhi ya mambo yaliyonukuliwa kuhusiana na riwaya ya baia’ ya al-Ghadir ambayo imenukuliwa na mwandishi wa tafsiri ya Kanz ad-Daqaiq katika kufasiri maana ya aya ya kutangazwa amri na ujumbe alioamrishwa Mtume Mtukufu (saw) na Mwenyezi Mungu kuutangaza katika tukio la al-Ghadir, kutoka kwenye marejeo ya kuaminika ya madhehebu ya Ahlul Beit (as). Hadithi hii imepokelewa kutoka kwa Maimamu Al Baqir na as-Swadiq (as), na masahaba Ibn Abbas, Jabir al-Ansari na wengineo. Inasema: ‘Mtume (saw) aliporejea kutoka kwenye Hija yake ya Mwisho Malaika Jibril (as) alimteremshia aya ifuatayo kutoka kwa Mwenyezi Mungu: Ewe Mtume! Fikisha uliyoteremshiwa kutoka kwa Mola wako. Na kama hutafanya, basi hukufikisha ujumbe wake; na Mwenyezi Mungu atakulinda na watu. Hakika Mwenyezi Mungu hawaongozi watu makafiri. Na hilo lilitimia baada ya kuwa amefika katika eneo la Ghadir Khum. Aliamuru Waislamu waliokuwa wamemtangulia warejeshwe nyuma na kuwasubiri wale waliokuwa hawajafika mahala hapo bado ili awatangazie yale aliyokuwa ameteremshiwa na Mwenyezi Mungu. Kisha alisimamisha swala ya jamaa. Alipomaliza kuswalisha swala ya Adhuhuri alianza kuwahutubia hutuba ndefu ambapo aliwahafamisha kwamba Malaika Jibril alikuwa amemteremshia aya iliyonukuliwa. Aliwasomea aya hiyo na kubainisha sababu ya kuteremshwa kwake…. Pia aliwasomea aya inayosema: Hakika walii wenu hasa ni Mwenyezi Mungu na Mtume wake na wale walioamini, ambao husimamisha Swala na hutoa Zaka wakiwa wamerukuu, na nyingine inayosema: Mtiini Mwenyezi Mungu na mtiini Mtume na wenye mamlaka katika nyinyi, na nyingine ambazo Mwenyezi Mungu aliziteremsha kuhusiana na Ahlul Beit wa Mtume, ili kuwa utangulizi na ushahidi wa lile jambo Mwenyezi Mungu alimuamrisha awatangazie watu, kuhusiana na kuwekwa Wilaya na Uimamu katika kizazi chake kitoharifu (as) ambapo wa kwanza wao alikuwa ni Imam Ali al-Murtadha (as) ambaye Mtume aliwaamuru watu kumbai na kumpa mkono wa utiifu baada ya kumaliza kutoa  hotuba yake.’

Hili ndilo jambo alilolitangaza na kulibainisha kwa uwazi mkubwa kupitia hotuba yake hiyo iliyojaa ufasaha kama mnavyoshuhudia hilo katika kila sehemu ya hutuba hiyo tuliyokunukulieni na nyingine ambayo mtaisikiliza hivi punde, endeleeni kuwa pamoja nasi.

 

Kati ya yale aliyoyasema Mtume Mtukufu (saw) katika hotuba yake siku ya al-Ghadir ni haya yafuatayo: ‘Enyi Watu! Hii ni mara ya mwisho kwangu kusimama hapa. Basi sikilizeni, mtii na kufuata amri ya Mola wenu. Hakika Mweyezi Mungu ndiye Mola wenu, Walii wenu, na Mungu wenu kisha baada yake Muhammad ndiye Walii wenu, ambaye amesimama mbele yenu kuwahutubia. Kisha baada yangu Ali ndiye atakayekuwa Walii na Imamu wenu kwa amri ya Mwenyezi Mungu Mola wenu na kisha Uimamu katika kizazi changu utaendelea kupitia kizazi chake hadi Siku ya Kiama, siku ambayo mtakutana na Mwenyezi Mungu na Mtume wake….’

Baada ya hapo Mtume Mtukufu (saw) alibainisha na kufafanua sifa na fadhila za Wasii wake al- Murtadha kwa kusema: ‘Enyi watu! Mfadhilisheni (mtangulizeni) Ali kwa sababu yeye ndiye mbora wa watu baada yangu… Kwa ajili yetu riziki iliteremshwa na viumbe kubakia…. Tafakarini (zingatieni kwa kina) Qur’ani na kufahamu vyema aya zake. Tazameni aya zake zilizo wazi na wala msifuate zinazoshabihiana (zilizofichika maana zake). Wallahi! Hakua yeyote atakayekufafanulieni dhamira (maana) zake wala kukubainishieni tafsiri zake….isipokuwa huyu ambaye mimi nimeunyanyua mkono wake - yaani Ali -. Hakika yule ambaye mimi ni Maula wake (msimamizi wa mambo yake) basi na huyu Ali ni Maula wake…. Naye ni ndugu na Wasii wangu, na umaula wake unatoka kwa Mwenyezi Mungu ambao Mwenyezi Mungu ameniteremshia.’

Kisha Mtume Mtukufu (saw) alisema kuhusiana na Maimamu wengine wa kizazi chake kitoharifu: ‘Enyi Watu! Hakika Ali na wema wengine katika kizazi changu ni Kizito Kidogo na  Qur’ani ndicho Kizito Kikubwa. Kila kimoja kinatokana na kingine na kuafikiana nacho. Havitatengana hadi vitakaponifikia kwenye Hodhi. Viwili hivi ni amana ya Mwenyezi Mungu kwenye vimbe Vyake na ndivyo vinavyotawala katika ardhi Yake. Hakika nimetekeleza! Hakika nimefikisha ujumbe! Hakika nimewasilizisha! Hakika nimefafanua!’

Kisha Mtume (saw) alisema: ‘Hakika Mweyezi Mungu amesema na mimi ninasema kwa niaba yake (kwamba) hakika hakuna Amir Amir al-Mu’mineena (kiongozi wa waumini) isipokuwa ndugu yangu huyu na wala uongozi wa waumini hauwi halali kwa mtu mwingine yeyote baada yangu isipokuwa kwake…. Allahumma mimi ninakufanya wewe kuwa shahidi na inatosha kwamba Wewe ni shahidi kuwa nimefikisha ujumbe.’ Kisha akasema: Enyi watu! Hakika Mwenyezi Mungu amekukamilisheni dini kupitia Uimamu wake. Hivyo basi yoyote yule ambaye hatamzingatia yeye wala yule atakayesimama kwenye nafasi yake katika kizazi changu kutoka kwenye kizazi chake hadi Siku ya Kiama…. basi hao ndio walioharibikiwa mambo yao……. Enyi Watu! Mwaminini Mwenyezi Mungu, Mtume wake na nuru iliyoteremshwa pamoja naye…. Enyi watu! Nuru kutoka kwa Mwenyezi Mungu iko ndani yangu, kisha itafuatwa kwa Ali kisha kwa kizazi chake hadi itakapomfikia al-Mahdi (Imam Mahdi) ambaye atachukua haki ya Mwenyezi Mungu na kila haki ambayo ni yetu sisi….’

 

Mtume (saw) pia alisema: ‘Enyi watu! Ninakuachieni Uimamu baada yangu hadi Siku ya Kiama. Hakika nimefikisha ujumbe nilioamrishwa kuufikisha, ambayo ni hoja kwa kila mtu aliye hapa na asiyekuwepo na kwa kila mtu ambaye amezaliwa tayari na ambaye bado hajazaliwa. Hivyo basi aliye hapa na amfahamishe jambo hili asiyekuwepo hapa na mzazi amfahamishe mwanawe hadi Siku ya Kiama.’

Ndugu wasikilizaji kuna riwaya ngingine nyingi za kuaminika ambazo zimepokelewa kuhusiana na hotuba hii muhimu ya Mtume Mtuku (saw) ambayo aliitoa katika tukio la Ghadir Khum ambapo zote zina maana iliyo wazi kama hii tuliyokufafanulieni kuhusiana na Uimamu wa Watu wa Nyumba yake tukufu. Zote hizi zinathibitisha ukweli huu kwamba jambo alilowatangazia Mtume (saw) Waislamu siku ya Ghadir kwa amri ya Mwenyezi Mungu mwenyewe, lilijumuisha kutangazwa kwa Uimamu wa Maimamu wotoharifu (as) hadi Siku ya Kiama.

Na kufikia hapa tunafahamu vyema, kwa mujibu wa vyanzo vya kutegemewa vya Masuni na Mashia kwamba, aya ya kukamilishwa dini na kutimia neema ya Mwenyezi Mungu aliyoteremshiwa Mtume siku ya Ghadir, ilihusu kutangazwa Maimamu wanaotokana na kizazi cha Mtume ambao wataungoza Umma wa Muhammad (saw) hadi Siku ya Kiama.

Na kufikia hapa wapenzi wasikilizaji, kutoka Idhaa ya Kiswahili Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, hatuna la ziada ila kukutakieni usikilizaji mzuri wa vipindi vyetu vilivyosalia, kwaherini.