Jumatatu, 7 Julai, 2025
Leo ni Jumatatu tarehe 11 Mfunguo Nne Muharram 1447 Hijria sawa na 07 Julai mwaka 2025.
iku kama ya leo, miaka 1386 iliyopita, yaani tarehe 11 Muharram mwaka 61 Hijiria, msafara wa mateka wa familia ya Bwana Mtume Muhammad (swa), ulianza kuelekea Sham, yalikokuwa makao makuu ya utawala wa kidhalimu wa Yazidi bin Muawiya baada ya tukio chungu la mauaji ya siku ya Ashura.
Baada ya majeshi ya Yazidi yaliyokuwa yakiongozwa na Omar bin Sa’ad kumuua shahidi Imam Hussein bin Ali bin Abi Twalib (as) na masahaba wake, majeshi hayo ambayo hayakuwa na chembe yoyote ya ubinaadamu moyoni, yalianza kupora vitu vya thamani vya msafara wa watu wa familia ya Mtume (swa). Askari hao sanjari na kuchoma moto hema za Imam Hussein (as) na watu wake, waliwanyang’anya pia wanawake mapambo yao, huku wakiwaacha bila stara wanawake. Hatimaye jioni ya siku kama ya leo msafara wa familia ya Imam Hussein uliokuwa ukiongozwa na Imam Sajjad (as) na Bibi Zainab (as), uliendelea na safari kutoka mjini Kufa, Iraq kuelekea Sham, baada ya watukufu hao kuamsha hamasa ya kimapinduzi dhidi ya madhalimu, kuwalaumu watu wa mji huo kwa kumsaliti Imam Hussein (as) na kufichua maovu ya watawala wa Bani Umayyah.

Miaka 218 iliyopita mwafaka na siku kama hii ya leo, ulitiwa saini mkataba wa kihistoria wa Tilsit katika mji wenye jina hilo huko Russia kati ya Alexander wa Kwanza, mfalme wa Russia na Napoleon Bonaparte wa Ufaransa.
Kwa mujibu wa mkataba huo Urusi na Ufaransa zilikubaliana kuwa, ikiwa nchi yoyote ingeishambulia nchi moja wapo kati ya hizo, zingesaidiana kumpiga adui. Mkataba huo wa urafiki, uliendelea hadi mwaka 1810.

Katika siku kama ya leo miaka 47 iliyopita, visiwa vya Solomon vilivyoko kaskazini mashariki mwa Australia katika bahari ya Pacific vilipata uhuru.
Visiwa hivyo viligunduliwa na watu kutoka Ulaya mwaka 1567. Mwaka 1885 Ujerumani ilidai umiliki wa visiwa vya kaskazini mwa Solomon na ndiyo maana ikachukua hatua ya kuvishambulia na kisha kuvikalia kwa mabavu.
Muongo mmoja baadaye, Uingereza ilivishambulia visiwa hivyo na kuvidhibiti. Harakati ya kupigania uhuru ilianzishwa katika visiwa hivyo baada ya Vita Vikuu vya Pili vya Dunia na kuzaa matunda katika tarehe kama ya leo ambapo visiwa hivyo vilipata uhuru.

Tarehe 7 Julai mwaka 2005 kulitokea mlipuko katika basi na milipuko mingine katika vituo vitatu vya treni ya chini ya ardhi katikati mwa mji mkuu wa Uingereza, London na kusababisha vifo vya watu 50 na wengine wapatao 700 kujeruhiwa.
Mashambulio hayo yalifanywa sambamba na kikao cha Viongozi wa Nchi Tajiri Kiviwanda Duniani G8 huko nchini Scotland kaskazini kwa Uingereza. Mashambulio hayo ya mabomu yalitekelezwa ili kupinga ushirikiano wa London na Washington katika kuikalia kwa mabavu Afghanistran na Iraq na kuuawa kiholela wananchi wa nchi hizo.
Serikali ya Uingereza ilidai kwamba, Waislamu walihusika na tukio hilo, na kwa muktadha huo mashinikizo dhidi ya Waislamu wa Uingereza yaliyoanza baada ya mashambulio ya Septemba 11, 2001 yakashadidi zaidi.
