Alkhamisi, Julai 10, 2025
Leo ni Alkhamisi tarehe 14 Mfunguo Nne Muharram 1447 Hijria sawa na tarehe 10 Julai 2025.
Siku kama ya leo miaka 1151 iliyopita, wavuvi wa Norway walivumbua kisiwa cha Iceland kilichopo kaskazini mwa bara la Ulaya na karibu na ncha ya kaskazini.
Kisiwa hicho kiliingia katika udhibiti wa Norway mwaka 1261 Miladia na karne moja baadaye, Denmark ikazidhibiti nchi mbili zote yaani, Iceland na Norway. Hatimaye mwaka 1944 Iceland ilifanikiwa kupata uhuru kamili kutoka kwa mkoloni Mdenmark.

Miaka 284 iliyopita katika siku kama hii ya leo ardhi ya Alaska iligunduliwa na mvumbuzi wa Kidenmark kwa jina la Vitus Bering.
Mvumbuzi huyo aligundua ardhi ya Alaska inayopatikana kaskazini magharibi mwa Canada akiwa katika safari yake kuelekea Urusi. Hadi kufikia mwaka 1867 eneo tajiri kwa mafuta la Alaska lilikuwa sehemu ya mamlaka ya Urusi ya Kitezari.
Hata hivyo mwaka huo Urusi iliiuzia Marekani ardhi ya Alaska kwa kiasi cha dola milioni saba, eneo ambalo leo hii linahesabiwa kuwa jimbo la 49 la Marekani.

Siku kama ya leo miaka 85 iliyopita, Italia ilijiunga rasmi na Ujerumani katika Vita vya Pili vya Dunia.
Kipindi hicho Waziri Mkuu wa Italia alikuwa ni Benito Mussolini ambaye pia alikuwa kiongozi wa chama cha Ufashisti nchini humo. Kuingia Italia katika vita hivyo hakukumsaidia chochote Hitler, licha ya kwamba kulikuwa na taathira kubwa ya ongezeko la uharibifu.
Hadi kipindi cha miaka mitatu, Italia ilikuwa imepata hasara kubwa katika sekta tofauti, huku Benito Mussolini akiuzuliwa madarakani na mfalme wa wakati huo wa Italia mwezi Disemba mwaka 1943, kufuatia kudhibitiwa na waitifaki ardhi ya kusini mwa nchi hiyo.

Siku kama ya leo, miaka 84 iliyopita, Jemedari Henri Petain Waziri Mkuu wa muda na afisa wa ngazi za juu wa jeshi la Ufaransa, alichukua uongozi baada ya Ufaransa kushindwa na Wanazi wa Ujerumani katika Vita vya Pili vya Dunia.
Kwa mujibu wa mkataba wa vita uliosainiwa na nchi mbili hizo tarehe 22 Juni 1940, eneo la kaskazini mwa Ufaransa, ukiwemo mji wa Paris lilibaki chini ya himaya ya jeshi la Manazi wa Ujerumani.

Katika siku kama ya leo miaka 51 iliyopita, visiwa vya Bahamas huko Amerika ya Kati vilipata uhuru kutoka Uingereza na siku kama ya leo hufahamika visiwani humo kama siku ya taifa. Visiwa vya Bahamas viligunduliwa mwaka 1492 na mvumbuzi wa Ulaya Christopher Columbus na kuwa chini ya himaya ya Uhispania. Visiwa vya Bahamas vilipata uhuru mwaka 1973 na kuwa mwanachama wa Umoja wa Mataifa. Visiwa hivyo viko kaskazini mwa Cuba na kusini mashariki mwa Marekani.
