Aug 08, 2025 03:41 UTC
  • Ijumaa, tarehe 8 Agosti, 2025

Leo ni Ijuamaa tarehe 14 Mfunguo Tano Safar 1447 Hijria inayosadifiana na tarehe 8 Agosti 2025.

Siku kama ya leo miaka 2358 iliyopita sawa na tarehe 8 Agosti 333 kabla ya kuzaliwa Nabii Issa Masih AS, ilianza kazi ya ujenzi wa mji wa Alexandria nchini Misri, ambao leo hii unahesabiwa kuwa moja kati ya bandari muhimu kusini mwa Bahari ya Mediterranean.

Ujenzi huo ulifanyika kwa amri ya Alexander Macedon huko kaskazini mwa Misri. 

Katika siku kama ya leo miaka 815 iliyopita sawa na tarehe 14 Safar mwaka 632 Hijria alifariki dunia Abul Mahasin Bahauddin mashuhuri kwa jina la Ibn Shidad, fakihi, kadhi na mwanahistoria wa Kiislamu.

Alizaliwa mwaka 539 huko Mosul, moja ya miji ya Iraq na alihifadhi Qur'ani akiwa bado mtoto na baadaye akajifunza hadithi, tafsiri na kusoma Qur'ani na kupata umahiri mkubwa katika taaluma hizo. Ibn Shidad alifanya safari katika nchi mbalimbali za Kiislamu kwa ajili ya kutafuta elimu.

Miongoni mwa vitabu vyake mashuhuri ni an Nawadir al Sultwaniya, Dalailul Ah-kam na al Aswaa kinachozungumzia maisha ya Nabii Musa A.S na mapambano yake dhidi ya Firauni.

Miaka 440 iliyopita katika siku kama hii ya leo alizaliwa Mulla Muhsin Faidh Kashani, aliyekuwa faqihi, mpokezi wa hadithi, mwanafalsafa na arifu mkubwa wa Kiislamu nchini Iran.

Faidh Kashani alipata elimu za fiqhi, hadithi, tafsiri na falsafa kwa wanazuoni wakubwa wa zama zake kama Muhammad Taqi Majlisi, Sheikh Bahai na Mulla Sadra.

Msomi huyo mkubwa ameandika vitabu vingi, mashuhuri zaidi vikiwa ni tafsiri ya Qur'ani ya al Swafi, Mafatiihu Sharaai', al Wafi na al Mahajjatul Baidhaa.   

ملا محسن فیض کاشانی

Siku kama ya leo miaka 33 iliyopita mwafaka na tarehe 17 Mordad 1371 Hijria Shamsia, alifariki dunia Ayatullahil Udhma Alhaj Sayyid Abul Qassim al Mussawi al Khoui, faqihi na marjaa mkubwa wa Kiislamu duniani, akiwa na umri wa miaka 96.

Mwanachuoni huyo mashuhuri alizaliwa katika mji wa Khoui ulioko kaskazini magharibi mwa Iran na akiwa katika umri wa ubarobaro, alifuatana na baba yake mjini Najaf nchini Iraq kwa ajili ya kujiendeleza kielimu. Katika zama za umarjaa wake, Ayatullahil Udhma al Khoui alitoa fatwa inayosisitiza udharura wa kuilinda Palestina na kuikomboa Quds Tukufu kutoka mikononi mwa Wazayuni maghasibu.

Alimu huyo mkubwa ameacha vitabu vingi vikiwemo 'Jawaahirul Usuul', 'Muntakhabu Rasaail', 'al Bayaan Fii Tafsiiril Qurani' na "Misbahul Faqaha". 

Ayatullahil Udhma Alhaj Sayyid Abul Qassim al Mussawi al Khoui

Miaka 27 iliyopita katika siku kama ya leo inayosadifiana na tarehe 8 Agosti 1998, wanamgambo wa kundi la Taliban nchini Afghanistan waliuteka na kuukalia kwa mabavu mji wa Mazar Sharif ulioko kaskazini mwa nchi hiyo.

Baada ya kukaliwa kwa mabavu mji huo, wanamgambo wa Taleban waliushambulia ubalozi mdogo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika mji huo na kuwauwa shahidi wanadiplomasia 8 wa Kiirani na mwandishi mmoja wa habari.

Kundi la Taliban liliasisiwa mwaka 1994 kwa ufadhili na usaidizi wa Marekani na Pakistan na kufanikiwa kuikalia sehemu kubwa ya ardhi ya Afghanistan.