Aug 14, 2025 02:31 UTC
  • Jumatano, Agosti 13, mwaka 2025

Leo ni Jumatano tarehe 19 Mfunguo Tano Safar 1447 Hijria sawa na tarehe 13 Agosti 2025.

Katika siku kama ya leo miaka 1276 iliyopita yaani tarehe 19 Safar mwaka 171 Hijria  alizaliwa Abu Ma'ashar Balkhi mmoja kati ya wanajimu na wasomi wakubwa wa elimu ya nujumu wa Kiirani.

Kutokana na hamu yake kubwa ya elimu ya nyota, Abu Ma'ashar alielekea Baghdad na kuanza kusoma elimu ya nujumu. Abu Ma'ashar Balkhi alitumia vyanzo vya lugha za Kiarabu, Kihindi, Kigiriki na Kisiriani kwa ajili ya kupata elimu ya nujumu na kuwa miongoni mwa wanajimu wakubwa katika zama zake.

Kazi zake katika taaluma hiyo zilitumiwa kwa karne kadhaa katika ulimwengu wa Kiislamu na Kimagharibi hata baada ya kufariki kwake dunia. Miongoni mwa vitabu mashuhuri vya msomi huyo wa Kiislamu ni al-Madkhal al-Kabir na al-Mawalidul al Saghirah.   

Siku kama ya leo miaka 162 iliyopita aliaga dunia Frederick Eugene Delacroix, mchoraji maarufu wa Ufaransa. Eugene Delacroix alirithi kipaji cha sanaa ya uchoraji kutoka kwa mama yake.

Baada ya kupoteza wazazi wake wawili akiwa kijana mdogo na kujikuta akiishi maisha magumu sana ya umasikini, aliamua kufanya juhudi kubwa katika kujiendeleza na fani yake uchoraji.

Baadaye alianza kufanya maonyesho ya sanaa hiyo katika ukumbi wa jiji la Paris. Katika kipindi hicho baadhi ya watu walikuwa wakimfanyia maskhara na kumkebehi, hata hivyo hakuvunjika moyo na hatimaye kazi zake zilikuwa na taathira. Alipata umashuhuri katika kipindi kifupi na kazi zake zikapokewa sana katika jamii.   ***

Siku kama ya leo miaka 126, yaani tarehe 13 Agosti miaka 115 iliyopita, alizaliwa Alfred Hitchcock mtengeneza filamu mashuhuri wa Kiingereza.

Alionesha kazi yake ya kwanza mwaka 1920 na baadaye akaanza kujihusisha na uongozaji filamu. Filamu zake za kuogopesha na za kusisimua zilikuwa mashuhuri mno katika zama hizo. Filamu hizo zilimfanya awe mashuhuri kwa jina la the Master of Suspense.

Miongoni mwa filamu zake ni The Man Who Knew Too Much na Young and Innocent. Alfred Hitchcock aliaga dunia tarehe 28 Aprili 1980.

Eugene Delacroix

Siku kama ya leo miaka 115 iliyopita, aliaga dunia Florence Nightingale, mwanzilishi wa uuguzi wa kisasa huko nchini Italia, akiwa na umri wa miaka 90.

Nightingale alizaliwa tarehe 12 Mei 1820 nchini Italia. Aliishi kipindi kirefu cha ujana wake nchini Uingereza. Akiwa kijana alifanya juhudi kubwa katika kuwasaidia watu, suala ambalo alilipa umuhimu mkubwa kuliko kitu kingine chochote na hatimaye alisabilia maisha yake kwa amjili ya kuuguza wagonjwa.

Bi, Florence Nightingale alikuwa muuguzi na mwanahesabati mashuhuri wa Uingereza. Alipewa lakabu ya ''Mwanamke Mwenye Taa Mkononi' kutokana na uvumilivu wake mkubwa na kujinyima usingizi kwa ajili ya kuwahudumia wagonjwa nyakati za usiku. Alifanya juhudi kubwa pia kwa ajili ya kuboresha huduma za afya katika hospitali nyingi nchini Uingereza. Kazi hiyo aliyoifanya kwa miaka mingi bila kuchoka ilimdhoofisha sana kimwili kwa kadiri kwamba alikuwa kipofu mwishoni mwa umri wake na hatimaye aliaga dunia tarehe 13 Agosti 1910. 

Florence Nightingale

Siku kama ya leo miaka 65 iliyopita, Jamhuri ya Afrika ya Kati ilipata uhuru kutoka kwa mkoloni Mfaransa.

Ilikuwa katikati ya karne ya 19 wakati nchi hiyo iliyokuwa ikijulikana hapo kabla kwa jina la Ubangi-Shari, ilipounganishwa na makoloni ya Ufaransa barani Afrika. Hata hivyo mwaka 1958, Jamhuri ya Afrika ya Kati ilijipatia mamlaka ya ndani na miaka miwili baadaye yaani mwaka 1960, ikajikomboa na kupata uhuru kamili.   ***