Alkhamisi, tarehe 28 Agosti, 2025
Leo ni Alkhamisi tarehe 4 Rabiul Awwal, mwaka 1447 Hijria, inayosadifiana na tarehe 28 Agosti mwaka 2025.
Miaka 275 iliyopita katika siku kama ya leo, yaani tarehe 28 Agosti 1749 alizaliwa Johann Wolfgang Von Goethe malenga na mwandishi mkubwa wa Kijerumani.
Von Goethe alisoma na kujifunza mambo mbalimbali kama uchoraji na kadhalika katika mji aliozaliwa wa Frankfurt nchini Ujerumani, huku akiendelea na masomo yake ya taaluma ya sheria.
Von Goethe ambaye anahesabiwa kuwa mmoja kati ya waenezaji wa fasihi ya lugha ya Kifarsi, alivutiwa mno na fasihi ya Kifarsi na hasa mashairi ya Hafidh, malenga na mshairi mashuhuri wa Kiirani.
Mwandishi huyo wa Kijerumani alikipenda sana Kitabu Kitakatifu cha Qur'ani pamoja na dini ya Kiislamu. Johann Wolfgang Von Goethe alifariki dunia mwaka 1832.

Katika siku kama ya leo miaka 261 iliyopita alifariki dunia huko Karbala, Iraq faqihi, mpokezi wa Hadithi, mhakiki na mwandishi maarufu wa Kiislamu katika karne ya 12 Hijria, Sheikh Yusuf Bahrani.
Alijifunza elimu ya msingi kwa baba yake na baadaye alielekea Bahrain na Makka kwa ajili ya kupata elimu ya juu. Baadaye alielekea katika mji wa Fasa kusini mwa Iran ambako alianza kufundisha na kuandika vitabu. Wakati huo alianza kuandika kitabu chake kikubwa zaidi cha fiqhi kinachoitwa "al Hadaiqun Nadhirah".
Mwanzuoni huyo ameandika vitabu 32 katika taaluma mbalimbali vikiwemo "Anisul Musafir" na "Jalisul Khawatwir.''

Miaka 105 iliyopita katika siku kama hii ya leo kwa mujibu wa kalenda ya Hijria, alifariki dunia Ayatullah Mirza Muhammad Taqi Hairi Shirazi, msomi mkubwa na mwanamapambano wa Iran.
Ayatullah Mirza Muhammad Taqi Hairi Shirazi ni mmoja wa maulama wakubwa wa Kishia na aliyepambika kwa elimu na uchaji-Mungu huko mjini Shirazi, moja ya miji ya Iran ya leo. Msomi huyo alipata umashuhuri kutokana na kuongoza mapambano ya Waislamu dhidi ya Uingereza.
Baada ya Ayatullah Mirza Muhammad Taqi Hairi Shirazi kugundua kuwa Uingereza ilikuwa na lengo la kudhibiti nchi za Kiislamu kupitia pendekezo la kutaka kukubaliwa mwakilishi wa Londoni nchini Iraq kuwa rais wa nchi hiyo, alitoa fatwa mashuhuri iliyohalalisha mapambano ya silaha ya wananchi wa Iraq dhidi ya mkoloni Mwingereza. Fatwa hiyo iliitia hofu Uingereza ambayo ililazimika kuachana na mpango huo wa kikoloni. Miongoni mwa vitabu vya amsomi huyo wa Kiislamu ni Al Qaswaidul Fakhirah Fii Madhil Itrati Atwahirah.

Siku kama ya leo miaka 68 iliyopita kombora la kwanza la kuvuka mabara lilirushwa hewani na wasomi wa Urusi ya zamani.
Siku nne baadaye yaani tarehe 4 Oktoba wasomi wa Urusi walirusha angani satalaiti ya kwanza dunia iliyopewa jina la Sputnik 1 kwa kutumia kombora hilo.
Hatua hiyo ilipongezwa kote dunia, na wasomi hao walitangaza kuwa watatuma mwanadamu angani katika kipindi cha chini ya miaka mitatu na kwamba watatuma chombo cha anga katika mwezi miaka mitano baadaye. Wasomi hao wa Urusi walitimiza hadi zao.

Katika siku kama hii ya leo miaka 62 iliyopita yaani Agosti 28, 1963, Martin Luther King mwanaharakati mkubwa wa kutetea haki za Wamarekani weusi nchini Marekani, alihutubia umati mkubwa wa watu waliofanya mgomo wa kutaka wapewe haki ya kijamii nchini humo.
Luther King ambaye ni Mmarekani mweusi alihutubia umati huo kwenye uwanja wa kumbukumbu wa Lincoln mjini Washington.
Kwenye mkutano huo, Martin Luther King alieleza ndoto yake ya kuwa huru Wamarekani weusi. ***