Jumatatu, 17 Novemba, 2025
Leo ni Jumatatu 26 Mfunguo Nane Jamad al-Awwal 1447 Hijria mwafaka na 17 Novemba 2025.
Siku kama ya leo miaka 1167 iliyopita, sawa na tarehe 26 Jamadil Awwal 280 Hijria, alifariki dunia Ibn Tayfur, mwandishi na malenga wa Kiarabu.
Ibn Tayfur alizaliwa mwaka 204 Hijiria. Baada ya kuhitimu masomo yake ya awali, alijishughulisha na uandishi wa vitabu mjini Baghdad. Katika kipindi hicho Ibn Tayfur alifahamiana na maulama na wasomi mashuhuri wa mji wa Baghdad. Ni baada ya hapo ndipo Ibn Tayfur akawa mashuhuri katika uwanja wa mashairi.
Mbali na uwanja huo, msomi huyo alijulikana sana kwa uandishi wa vitabu mbalimbali ambavyo hii leo vinapatikana katika maktaba za mji wa Baghdad, Iraq.

Siku kama ya leo miaka 308 iliyopita, Jean le Rond d'Alembert mwanahisabati wa Kifaransa alizaliwa katika mji wa Paris huko Ufaransa. Baba na mama yake walimtelekeza kando ya kanisa moja mjini Paris akiwa mtoto mchanga.
Aliokotwa na kulelewa na mwanamke na mwanaume mmoja waliokuwa wauza vioo.
Jean le Rond d'Alembert alisoma kwa bidii na baada ya kuhitimu masomo ya kati alianza kusoma taaluma ya tiba na sheria. Hata hivyo baada ya muda aliondokea kuipenda mno taaluma ya hisabati ambapo alifanya utafiti mkubwa katika uwanja huo. Alipotimiza umri wa miaka 22 d'Alembert alizindua makala kuhusiana na hesabu, makala ambayo yalimpatia umashuhuri mkubwa.
Ameacha athari mbalimbali ambazo zipo katika maktaba za Ufaransa. Jean le Rond d'Alembert alifariki dunia tarehe 29 Oktoba 1783 akiwa na umri wa miaka 66.

Siku kama ya leo miaka 229 iliyopita, Catherine The Great malkia mashuhuri wa Russia aliaga dunia.
Alizaliwa Mei Pili 1729 na akiwa na umri wa miaka 15 aliolewa na Peter III. Hata hivyo Peter III mfalme wa wakati huo wa Russia hakuwa akimpenda mkewe huyo na alikuwa akimvunjia heshima na kumdhalilisha mbele za watu. Mwaka 1762 wakati Peter III alipokuwa ametoka nje ya mji, Catherine the Great alijitangaza kuwa malkia wa Russia.
Peter III ambaye alishtushwa na kupata pigo kwa hatua hiyo alilazimika kujiuzulu pasina ya mapambano na baada ya siku chache akaaga dunia.

Siku kama ya leo miaka 167 iliyopita, Robert Owen mpigania mageuzi ya kisoshalisti wa Wales na mmoja wa waasisi wa Harakati ya Usoshalisti aliaga dunia.
Alianza harakati zake tangu akiwa na umri wa miaka 18 sambamba na kujenga kiwanda cha ufumaji.
Katika kiwanda chake hicho kwa mara ya kwanza alianza kuboresha hali ya afya na ustawi wa wafanyakazi barani Ulaya kwa kupunguza masaa ya kazi kutoka masaa 14 kufikia masaa 10.

Katika siku kama ya leo miaka 156 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 17 Novemba mwaka 1869, Mfereji wa Suez unaounganisha Bahari ya Mediterania na Bahari Nyekundu ulifunguliwa.
Uchimbaji wa mfereji huo ulisimamiwa na mhandisi wa Kifaransa Ferdinand de Lesseps katika kipindi cha miaka 10 huku ukiwa na urefu wa kilomita 168 na upana wa mita 120 hadi 200. Karne kadhaa kabla yake, Mfalme Daryush wa Iran na baadhi ya wafalme wa Misri walichukua hatua kadhaa za kuanzisha mfereji baina ya bahari hizo mbili, suala ambalo linaonyesha umuhimu wa Mfereji wa Suez unaopunguza kwa kiasi kikubwa masafa ya kutoka Asia kuelekea Ulaya, safari ambayo zamani ilikuwa ikifanyika kupitia kusini mwa bara Afrika.

Miaka 91 iliyopita katika siku kama ya leo alifariki dunia Ayatullah Allamah Mirza Muhammad Hussein Naini, marjaa na faqihi mkubwa na mmoja wa wahakiki wa elimu ya usulu fiq’h.
Allamah Naini alizaliwa mwaka 1276 Hijiria Qamaria mkoani Nain, ambao ni moja ya mikoa ya katikati mwa Iran katika familia ya kidini. Allamah Naini alisoma na kuhitimu masomo yake ya awali nyumbani kwao na kuendelea na masomo ya juu huko mjini Najaf, Iraq.
Akiwa mjini hapo, alipata kusoma kwa wasomi wakubwa wa zama hizo kama vile Allamah Mirza Shirazi na kufikia daraja ya juu ya elimu za hesabu, falsafa ya sayansi, falsafa, irfan na fiq’hi.
Miongoni mwa athari za Allamah Naini ni pamoja na vitabu vya “Wasilatun-Najjat” na “Tanbihul-Ummah wa Tanzihul-Millah” kitabu ambacho kilitoa mchango mkubwa katika kuathiri mapambano dhidi ya viongozi dhalimu wa zama hizo.

Siku kama ya leo miaka 46 iliyopita ulianzishwa tena uhusiano wa Iran na Libya. Uhusiano huo ulikatwa kabla ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu hapa nchini.
Sababu ya kukatwa uhusiano huo ni msimamo wa kiongozi wa zamani wa Libya Kanali Muammar Gaddafi aliyeitambua serikali ya Shah nchini Iran kuwa ilikuwa tegemezi kwa ubeberu wa Marekani na kwamba ilitanguliza mbele maslahi ya nchi za Magharibi na utawala ghasibu wa Israel kuliko maslahi ya nchi za Kiarabu na Wapalestina.

Miaka 45 iliyopita katika siku kama leo mji wa mpakani wa Susangerd huko kusini magharibi mwa Iran ulishuhudia mapambano kati ya wapiganaji wa Kiislamu na wanajeshi vamizi wa utawala wa zamani wa Iraq.
Oparesheni hiyo ya kujihami ilifanywa na wapiganaji shupavu 200 wa Iran waliojumuisha wanajeshi wa ulinzi, wanamgambo wa kujitolea na idadi ya kadhaa ya wenyeji wa mji huo waliokuwa wakitumia silaha nyepesi dhidi ya jeshi vamizi la Saddam.
Katika operesheni hiyo wapiganaji shupavu wa Iran chini ya uongozi wa shahidi Dakta Mustafa Chamran, walipambana vikali na kufanikiwa kuukomboa mji wa Susangerd.
