Jan 25, 2026 04:01 UTC
  • Jumapili, 25 Januari, 2026

Leo ni Jumapili 5 Shaaban 1447 Hijria awa na 25 Januari 2026 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 1409 iliyopita alizaliwa Imam Ali bin Hussein (AS) maarufu kwa laqabu ya Zainul Abidin katika mji mtakatifu wa Madina. Mtukufu huyo ni mwana wa Imam Hussein bin Ali Bin Abi Twalib, mjukuu wa Bwana wetu Muhammad (SAW). Alikuwa kinara wa elimu, uchamungu, ukarimu na upendo. Miongoni mwa sifa kuu za Imam Zainul Abidin ni kufanya ibada na kusali Swala za usiku. Alikuwa mwingi wa ibada na alipewa laqabu ya Sajjad kwa maana ya mwenye kusujudu sana na Zainul Abidin kwa maana ya 'Pambo la Wafanya Ibada' kutokana na sijda zake ndefu katika Swala. Imam Zainul Abidin alichukua jukumu la kuendeleza ujumbe wa mapambano ya Imam Hussein ya kupambana na ufisadi na dhulma ya watawala wa Bani Umayyah baada ya kuuawa baba yake katika medani ya Karbala. Aliishi miaka 35 baada ya tukio hilo chungu na aliuawa shahidi na mtawala wa Bani Ummayah Hisham bin Abdul Malik. Athari maarufu zaidi ya mtukufu huyo ni kitabu cha dua na miongozo ya Kiislamu cha al Sahifa as Sajjadiyya. 

 

Miaka 1134 iliyopita katika siku kama ya leo alifariki dunia tabibu na mwanakemia mtajika wa ulimwengu wa Kiislamu na mvumbuzi wa alkoholi kwa jina la Muhammad bin Zakaria Razi. Tabibu Razi alizaliwa mwaka 251 Hijria katika mji wa Rei kusini mwa Tehran ya leo. Mwanakemia huyo mkubwa alianza kujishughulisha na kazi ya usonara na baadaye kemia. Tabibu na mkemia Muhammad bin Zakaria Razi alijifunza pia elimu nyingine kama vile tiba, mantiki na falsafa. Baadae Razi alifanikiwa kutengeneza asidi ya Sulfuriki kwa kustafidi na mada asilia. Mwanasayansi huyu Muislamu wa Iran alikuwa mtu wa kwanza kugundua alkoholi.

 

Katika siku kama ya leo miaka 570 iliyopita, kazi ya uchapishaji vitabu ilianza na kitabu cha kwanza kabisa kikachapishwa kwa kutumia mashine iliyogunduliwa na Mjerumani, Johannes Gutenberg.  Mashine hiyo ya uchapishaji ilikuwa hatua muhimu katika njia ya uchapishaji na uenezaji wa elimu na maarifa kati ya wanadamu. Katika zama zake, Johannes Gutenberg pia alichapisha kitabu cha Biblia maarufu kwa jina la' Gutenberg Bible.'  Hii leo kurasa kadhaa zilizobakia za kitabu hicho zinahifadhiwa katika majumba ya makumbusho. 

 

Tarehe 5 Bahman miaka 47 iliyopita matabaka mbalimbali ya wananchi wa Iran waliendeleza maandamano makubwa katika miji mbalimbali dhidi ya utawala kibaraka wa Shah licha ya mamluki wa mfalme huyo kutumia mbinu zote za ukatili na ukandamizaji. Siku hiyo wananchi Waislamu wa Iran walipuuza marufuku iliyokuwa imetangazwa ya kuzuia mikusanyiko ya zaidi ya watu mawili katika miji mbalimbali ya Iran. Ukandamizaji mkubwa wa maajenti wa utawala wa Shah ulipelekea kuuawa shahidi idadi kubwa ya raia. Siku hiyo hiyo idadi kubwa ya maafisa wa Jeshi la Anga la Iran ilijiunga na harakati ya mapambano ya wananchi katika mitaa ya jiji la Tehran na kufanya maandamano dhidi ya utawala wa Shah. Askari hao walitangaza utiifu wao kwa Imam Ruhullah Khomeini na harakati ya Mapinduzi ya Kiislamu. 

 

Siku kama ya leo miaka 20 iliyopita Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS ilipata ushindi mkubwa katika uchaguzi wa Bunge ikiwa ni mara ya kwanza kwa harakati hiyo kushiriki kwenye zoezi hilo.  Katika uchaguzi huo uliosimamiwa na waangalizi wa kigeni, Hamas ilifanikiwa kupata viti 76 kati ya jumla viti 132 vya Bunge la Palestina licha ya propaganda chafu zilizokuwa zikifanywa na vyombo vya habari vya nchi za Magharibi. Kwa utaratibu huo Hamas ilimuarifisha Ismail Hania kama Waziri Mkuu na kutangaza kwamba itaunda serikali ya umoja wa kitaifa.  Hata hivyo nchi za Magharibi zikiongozwa na Marekani na muitifaki wake Israel, zilikataa kutambua rasmi serikali hiyo iliyochaguliwa kidemokrasia na wananchi wa Palestina.