Aug 23, 2016 06:20 UTC
  • Maswali Yetu na Majibu ya Thaqalain (134)

Assalaama Aleikum wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inayokutangazieni kutoka mjini Tehran. Kama ilivyokuwa katika vipindi vilivyopita kipindi cha juma hili cha Maswali Yetu na Majibu ya Thaqalain.

Kipindi chetu cha leo kitaendelea kujibu swali linalosema kwamba je, ni kwa nini Mtume Mtukufu (saw) alisisitiza katika hadithi ya Thaqalain ambayo imepokelewa kwa wingi katika madhehebu zote mbili za Shia na Suni kwamba kuepuka upotovu hakutimii ila kwa kushikamana kimamilifu na kwa pamoja na Vizito Viwili yaani Qur’ani Tukufu na Ahlul Beit wake watoharifu (as), na ni kwa nini haitoshi kushikama na Qur’ani peke yake? Katika kipindi kilichopita tuliashiria dalili ya Qur’ani kuhusiana na suala hili ambapo tulinukuu aya mbili za 43 na 44 za Surat an- Nahl ambapo Mwenyezi Mungu anasema: Nasi hatukutuma kabla yako ila wanaume tuliowapa Wahyi (Ufunuo). Basi waulizeni wenye ukumbusho kama nyinyi hamjui. Kwa hoja zilizo wazi na Vitabu. Nasi tumekuteremshia wewe Ukumbusho ili uwabainishie watu waliyoteremshiwa, wapate kufikiri.

Tulifahamu katika kipindi hicho baada ya kutadabari na kuchunguza kwa makini dhahiri ya aya hizo kwamba kanuni na desturi ya Mwenyezi Mungu kwa waja wake imesimama katika msingi wa kuwafanya Manabii na Mitume katika hatua ya kwanza na ya asili, na kisha mawasii na warithi wao katika hatua ya pili kuwa ndio wabainishaji wa hakika na makusudio ya Wahyi Wake, yakiwemo maandiko matakatifu ya Qur’ani Tukufu. Ni wazi kuwa hii ni katika rehema kubwa ya Mwenyezi Mungu kwa waja wake ambapo aliwajaalia watu wema na wasiotenda dhambi wala makosa fursa ya kuwabainishia makusudio ya maandiko na mafundisho Yake kiasi cha kufanya nyoyo zao zitulie na yale wanayoambiwa na kufafanuliwa na watukufu hao, na hivyo ufafanuzi huo kuwa hoja tosha na kamilifu katika kufahamu maneno ya Mwenyezi Mungu kwa njia sahihi na salama iliyo mbali na makosa, uelewa mbaya na upotoshaji unaoweza kufanywa na maimamu wa upotovu kuhusiama na makusudio ya maneno hayo.

Na aya tulizotangulia kusoma zinabainisha wazi kwamba Mtume Mtukufu (saw) ndiye marejeo ya kwanza ya ufafanuzi wa wahyi na maneneo ya Mwenyezi Mungu aliyoyateremshia wanadamu kupitia Qur’ni Tukufu. Wakati huohuo Hadithi ya Thaqalaini na hadithi nyinginezo sahihi ambazo zimepokelewa kwa wingi wa wapokezi wake katika madhehebu zote mbili zinasema wazi kwamba Ahlul Beit wa Mtume (saw) ni warithi wa elimu hiyo ya Mtume ya kufafanua na kubainisha makusudio ya aya za Qur’ani Tukufu. Kwa msingi huo ubainishaji na ufafanuzi wao kuhusiana na aya hizo ni hoja tosha na isiyo na makoso kwa waumini kwa sababu wao ni warithi wa elimu ya Mtume (saw) na milango ya mji wa elimu ya Mtume (saw). Isitoshe, wanazuoni wengi wa Kishia na Kisuni wamepokea hadithi za kuaminika zinazosema kwamba watu walio na ukumbusho ambao Mwenyezi Mungu aliamuru kuulizwa ufafanuzi wa aya za Qur’ani Tukufu tulizotangulia kusoma kuhusiana na hoja zilizo wazi na vitabu ni Ahlul Beit wa Mtume Muhammad (saw). Tunakunukulieni hapa baadhi ya hadithi hizo, endeleeni kuwa pamoja nasi.

 

Imam Tabari ambaye ni mmoja wa wanazuoni mashuhuri wa Kisuni anasema katika tafsiri yake ya Tabari na vilevile Qurtubi katika tafsiri yake ya Qurtubi wakimnukuu Jabir al-Ju’fi kwamba alisema: ‘Aya inayosema; Basi waulizeni wenye ukumbusho kama nyinyi hamjui, ilipoteremshwa Ali bin Abi Talib alisema: ‘Sisi ndio wenye ukumbusho.’

Al-Hakim al-Hasakani as-Shafi’ anasema katika kitabu chake cha Shawahid at-Tanzil kutoka kwa as-Sadiyy kutoka kwa Harith kwamba alisema: ‘Nilimuuliza Ali kuhusu aya hii, Basi waulizeni wenye ukumbusho akasema: ‘Wallahi sisi ndio wenye ukumbusho, na sisi ndio wenye elimu, na sisi ndio kitivo cha ufafanuzi na uteremkaji. Hakika nilimsikia Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) akisema: Mimi ni mji wa elimu na Ali ni mlango wake, hivyo basi anayetafuta elimu na apitie mlango wake.’

Al-Hakim al-Hasakani pia amenukuu hadithi nyingine saba katika kitabu hichohicho ambazo madhumuni yazo ni hiihii tuliyoifafanua. Maana hii pia imenukuliwa na at-Tha’labi katika Tafisiri yake kuhusiana na hadithi ya Jabir kama ilivyonukuliwa pia na Tabari, Qurtubi na wengineo.

Al-Hafidh Muhammad bin Mu’min as-Shirazi ambaye ni katika wanazuoni wa Kisuni pia amenukuu hadithi kutoka kwa Ibn Abbas ambayo imenukuliwa katika tafsiri nyingine mashuhuri 12 za Ahlu Suna ambazo ni za Abi Yusuf Ya’qub bin Suleiman, Maqatil bin Suleiman, Ibn Hajar, Jureih, Waki’ bin Jarrah, Qatada, Yusuf al-Qatan, Harb at-Tai, Sadiyy, Mujahid, Abu Swalih na Sufyan at-Thauri.

Ibn Abbas anasema katika riwaya hii ya wenye ukumbusho kwamba:

‘Wao ni Muhammad, Ali, Fatumah, al-Hassan na al-Hussein. Wao ndio wenye ukumbusho, elimu, akili na hoja zilizo wazi na wao ndio Watu wa Nyumba ya Mtume, chimbuko la ujumbe na sehemu wanayoteremkia na kupaa Malaika.’

Qur'ani, Kitabu pekee kisicho na makosa ndani yake

 

Na Hafidh al-Qunduzi al-Hanafi amesema katika kitabu chake cha Yanabi al-Mawadda akinukuu Kitabu cha al-Manaqib ambapo Abdul Hamid bin Abi Duweilim mmoja wa wanazuoni wa Kisuni anamnukuu Imam Ja’ffar as-Swadiq (as) akisema: ‘Ukumbusho una maana mili; Qur’ani na Muhammad (saw) na sisi ndio wenye ukumbusho kwa maana zote mbili. Ama maana ya Qur’ani inathibitishwa na kauli ya Mwenyezi Mungu inayosema: Nasi tumekuteremshia wewe Ukumbusho ili uwabainishie watu waliyoteremshiwa, ama maana ya Muhammad (saw) inathibitishwa na aya ya Surat at-Talaaq.’

Ndugu wasikilizaji aya anayoiashiria Imam Swadiq (as) ni kauli yake Mweyezi Mungu katika aya mbili za 10 a 11 katika Surat at-Talaaq zinazosema: ……….Hakika Mwenyezi Mungu amekuteremshieni Ukumbusho. Mtume anayekusomeeni Aya za Mwenyezi Mungu zinazobainisha, ili kuwatoa walioamini na wakatenda mema kutoka gizani kuwapeleka kwenye nuru………

Kuna hadithi nyingi mno ambazo zimepokelewa katika vitabu vya kuaminika vya Shia kuhusiana na maana hii ambapo tutatosheka kwa kutaja hadithi mbili tu kati ya hizo. Hadithi ya kwanza ni ile iliyonukuliwa na as-Swaduq katika kitabu cha Uyun Akhbar ar-Ridhwa ambayo inazungumzia maneno aliyoyatamka Imam Ridha (as) katika kikao cha Ma’mun ambapo wanazuoni waliokuwa hapo walimuuliza maswali kuhusiana na aya zinazozungumzia kuteuliwa na kufadhilishwa Ahlul Beit (as) juu ya watu wengine. Miongoni mwa maneno aliyosema Imam Ridha (as) katika kuthibitisha ustahiki wao wa kuongoza Umma wa Kiislamu ni haya: ‘…… Sisi ndio watu wenye ukumbusho ambao Mwenyezi Mungu anawazungumzia kwa kusema: Basi waulizeni wenye ukumbusho kama nyinyi hamjui. Wanazuoni wakasema; Mwenyezi Mungu alikusudia Mayahudi na Wakristo….. Imam Ridha (as) akajibu: Mwenyezi Mungu ametukuka na hilo! Je, hilo linajuzu? Kwa hivyo wanatuita kwenye dini yao wakisema: Ni bora kuliko dini ya Uislamu?!’

Hadithi ya pili ni ile iliyonukuliwa na Thiqatul Islam al-Kuleini katika kitabu cha Raudhat al-Kafi ambapo ananukuu barua ndefu ambayo Imam Swadiq (as) aliwaandikia masahaba zake kwa kusema katika sehemu moja ya barua hiyo: ‘Fahamuni kwamba si katika elimu ya Mwenyezi Mungu wala katika amri yake kwa mtu yoyote katika viumbe Vyake kufuata dini Yake kwa msingi wa matamanio, rai (maoni binafsi) wala kiasi (kukisia/kulinganisha). Hakika Mwenyezi Mungu ameteremsha Qur’ani na kujaalia humo ufafanuzi wa kila jambo na kuwateua watu wanaofaa kwa ajili ya Qur’ani na mafundisho yake…….Nao ni wenye ukumbusho ambao Mwenyezi Mungu ameuamuru Umma huu uwaulize (maswali na ufafanuzi)…Mtu anayewafuata humuongoza na kumpa katika elimu ya Qur’ani mambo yanayomuelekeza kwa Mwenyezi Mungu kwa idhini Yake….’

**********

Ndugu wasikilizaji katika kipindi kijacho cha Maswali Yetu na Majibu ya Thaqalain, Inshallah tutajadili aya ya saba ya Surat Aal Imran ambayo inazungumzia udharura wa kushikamana kwa pamoja na Vizito Viwili ili kunusurika kutokana na upotovu unaomwangamiza mwanadamu. Hivyo basi tunakuombeni mjiunge nasi katika kipidi hicho ili tupate kunufaika kwa pamoja na yake tutakayoyajadili katika kipindi hicho Inshallah. Kama kawaida kutoka Idhaa ya Kiswahili Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inayokutangazieni kutoka mjini Tehran hatuna la ziada isipokuwa kukutakieni kila la heri katika mambo yote mema mnayoyafanya. Basi hadi juma lijalo tunakuageni nyote kwa kusema, Wassalaam Aleikum Warhmatullahi Wabarakatuh.