Jumapili, 28 Agosti, 2016
Leo ni Jumapili tarehe 25 Dhil-Qaadah mwaka 1437 Hijria sawa na tarehe 28 Agosti 2016 Miladia.
Siku kama ya leo miaka 1427 iliyopita Mtukufu Mtume Muhammad (saw) akiwa na zaidi ya Waislamu laki moja na wafuasi wake, alitoka mjini Madina kwa nia ya kwenda kuzuru Nyumba ya Mwenyezi Mungu ya al-Kaabah. Inafaa kuashiria kuwa, tangu mtukufu huyo alipohajiri mjini Madina alifanya safari mara tatu kwenda mjini Makkah, hata hivyo alifanikiwa kutekeleza ibada ya Hijjah mara mbili pekee. Katika safari yake ya mwisho na wakati wa kutekeleza ibada ya Hijjah, aliwafundisha Waislamu namna ya kutekeleza kwa usahihi ibada hiyo. Na akiwa anarejea mjini na kabla ya Waislamu hawajasambaa kuelekea makwao katika bonde la Ghadir aliteremshiwa wahyi kutoka mbinguni akitakiwa amtangaze kiongozi wa Waislamu baada yake. Katika tukio hilo, Nabii wa Allah alimshika mkono Imam Ali (as) binamu na mkwe wake na kumtangaza kwa Waislamu kuwa khalifa baada yake. Hijja hiyo ilifahamika katika Uislamu kwa jina la Hijjatul-Wida’a, yaani Hijja ya kuaga.
Siku kama ya leo miaka 267 iliyopita, yaani Tarehe 28 Agosti 1749 alizaliwa Johann Wolfgang Von Goethe malenga na mwandishi mkubwa wa Kijerumani. Von Goethe alisoma na kujifunza mambo mbalimbali kama uchoraji na kadhalika katika mji aliozaliwa wa Frankfurt nchini Ujerumani, huku akiendelea na masomo yake ya taaluma ya sheria. Von Goethe ambaye anahesabiwa kuwa mmoja kati ya waenezaji wa fasihi ya lugha ya Kifarsi, alivutiwa mno na fasihi ya Kifarsi na hasa mashairi ya Hafidh, malenga na mshairi mashuhuri wa Kiirani. Mwandishi huyo wa Kijerumani alikipenda sana Kitabu Kitakatifu cha Qur'ani pamoja na dini ya Kiislamu. Johann Wolfgang Von Goethe alifariki dunia mwaka 1832.
Siku kama ya leo miaka 64 iliyopita, alifariki dunia Ayatollahil udhma Sayyid Muhammad Taqi Khonsari mmoja wa Marjaa taqlidi wakubwa. Ayatollah Khonsari alizaliwa mwaka 1267 Hijria Shamsia huko Khonsari moja kati ya miji ya katikati mwa Iran. Msomi huyo alipata elimu katika fani za fiqih, usul-fiqih na falsafa kutoka kwa maustadhi mashuhuri wa hauza ya kielimu ya mji mtakatifu wa Najaf huko Iraq. Akiwa nchini humo, Sayyid Muhammad Taqi Khonsari alishirikiana na wananchi katika vita vilivyopiganwa kati yao na wanajeshi wa Uingereza, hata hivyo Ayatollah Khonsari alikamatwa mateka na vikosi hivyo na kubaidishwa nchini Singapore. Baada ya miaka minne ya kubaidishwa hatimaye alirejea nchini Iran na kuanza kujishughulisha na kazi ya kufundisha katika hawza ya kielimu ya mjini Qum na muda mfupi baadaye akafikia daraja ya umarjaa wa Waislamu.
Siku kama ya leo miaka 59 iliyopita kombora la kwanza la kuvuka mabara lilirushwa hewani na wasomi wa Urusi ya zamani. Siku nne baadaye yaani tarehe 4 Oktoba wasomi wa Urusi walirusha angani satalaiti ya kwanza dunia iliyopewa jina la Sputnik 1 kwa kutumia kombora hilo. Hatua hiyo ilipongezwa kote duniani na wasomi hao kutangaza kuwa wangetatuma mwanadamu angani katika kipindi cha chini ya miaka mitatu na kwamba wangetuma chombo cha anga miaka mitano baadaye, ahadi ambazo walizitimiza kama walivyoahidi.
Siku kama ya leo miaka 47 iliyopita, alifariki dunia Sayyid Zia'eddin Tabatabai, mwanasiasa wa Iran. Tabatabai alizaliwa mwaka 1268 Hijiria huko mjini Shirazi, kusini mwa Iran na kuanza kusoma elimu ya msingi na dini. Kadhalika aliweza kujifunza lugha ya Kingereza, Kifaransa na Kirusi. Katika kipindi cha mapinduzi ya katiba, alikuwa miongoni mwa wanaharakati wa mapinduzi hayo ambapo pia aliweza kuchapisha magazeti kadhaa katika uwanja huo. Aidha Sayyid Zia'eddin Tabatabai aliendeleza harakati za kisiasa katika umri wake wote. Katika kipindi cha utawala wa Kipahlavi, Tabatabai alikuwa upande wa Uingereza huku akijitenga na kushughulikia maslahi ya taifa lake.
Na siku kama ya leo miaka 53 iliyopita yaani Agosti 28, 1963, Martin Luther King mwanaharakati mkubwa wa kutetea haki za Wamarekani weusi nchini Marekani, alihutubia umati mkubwa wa watu waliofanya mgomo wa kutaka wapewe haki za kijamii nchini humo. Luther King ambaye ni Mmarekani mweusi alihutubia umati huo kwenye uwanja wa kumbukumbu wa Lincoln mjini Washington. Kwenye mkutano huo, Martin Luther King alieleza ndoto yake ya kuwa huru Wamarekani weusi.