Aug 30, 2016 10:40 UTC
  • Maswali Yetu na Majibu ya Thaqalain (136)

Assalaama aleikum wapenzi wasikilizaji na karibuni kusikiliza sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Maswali Yetu na Majibu ya Thaqalain ambacho kinakujieni kupitia Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inayokutangazieni kutoka mjini Tehran.

Kipindi chetu cha juma hili kama tulivyosema katika kipindi kilichopita kitaendelea kujibu swali ambalo tumekuwa tukilijadili katika vipindi vitatu vilivyopita ambalo linasema: Je, ni kwa nini hadithi ya Thaqalain imebana wongofu na kuepuka mwanadamu upotevu katika vitu viwili ambavyo Waislamu wanapasa kushikamana navyo kwa pamoja bila ya kukizingatia kimoja na kukipuuza cha pili, vitu vyenyewe vikiwa ni Kitabu Kitakatifu cha Mwenyezi Mungu, Qur’ani Tukufu na Ahlul Beit Watoharifu wa Mtume (saw)?

Ilibainika katika kipindi kilichopita kwa kutegemea aya ya saba ya Surat  Aal Imran kwamba, hakika hadithi ya Thaqalain ni tafsiri ya Mtume Mtukufu (saw) ya aya hii kwa sababu inasema wazi kwamba katika Qur’ani Tukufu kuna aya zinazofahamika wazi na moja kwa moja bila kuhitajia ufafanuzi mkubwa na wa kina na nyingine za mifano ambazo kuna uwezekano wa kutolewa tafsiri zilizo na maana kadhaa, lakini pamoja na hayo maana halisi ya aya hizo za mifano hupatikana kwa kurejeshwa kwa aya madhubuti na zilizo wazi ambazo ndizo mama wa Kitabu. Licha ya hayo kuna watu waovu ambao huwa na maradhi na upotovu nyoyoni mwao ambao hufuatilia kwa makusudi aya hizo za mifano kwa ajili ya kutafuta fitina na kuwapotosha watu na kuwafanya wawafuate na kuwaabudu kinyume na matakwa ya Mwenyezi Mungu.

Kwa msingi huo tafsiri sahihi ya Qur’ani Tukufu ndio moyo wa siri za Mwenyezi Mungu zilizofichika ambazo kwazo milima hutembea, ardhi kuvukwa na maiti kuzungumziwa, kama inavyotwambia hilo aya ya 31 ya Surat Ra’d ambayo inaashiria nguvu kubwa ambayo huipata mwanadamu anapofanikiwa kuwa na uwezo wa kupata maarifa ya tafsiri sahihi ya Qur’ani. Kwa msingi huo Mwenyezi Mungu amewazui maimamu wa batili ambao wana upotovu kwenye nyoyo zao uwezo wa kuwa na maarifa sahihi ya kufasiri kitabu chake kitakatifu na kuwapa uwezo huo watu waliozama na kubobea kwenye elimu ambao ni maasumu ambao hutumia tafsiri sahihi ya kitabu hicho kuwaongoza waja wake kuelekea Muumba wao wa haki na Mtukufu. Hapa tunatambua kwamba ni katika rehema na neema kubwa ya Mwenyezi Mungu kwa waja wake kwamba alijaalia watu waliobobea kwenye elimu kuwa njia ya waja kunufaika na baraka za Qur’ani na kuwafundisha njia za kurejesha aya za mifano kwenye aya zilizo wazi, ili wapate kuepuka shari na upotoshaji wa maimamu wa upotovu. Jambo hilo huwawezesha wema waliobobea kwenye elimu kuwafikishia waja mambo ambayo yanaweza kuwanufaisha katika mafundisho sahihi ya Qur’ani ili kuwapa fursa ya kujikusanyia masurufu itakayowafaidi katika njia iliyo nyooka ya kuelekea kwa Muumba wao. Hakika hii ya Qur’ani Tukufu imeashiriwa na hadithi kadhaa ambapo tutaashiria baadhi katika katika kipindi hiki, hivyo endeleeni kuwa pamoja nasi.

 

Bwana wetu, Mlango wa Elimu ya Mtume Muhammad (saw) al-Imam Ali al-Murtadha (as) anasema katika sehemu moja ya hadithi iliyonukuliwa katika kitabu cha al-Ihtijaj kwamba Mwenyezi Mugu Mtukufu amegawa maneno yake katika makundi matatu. La kwanza ni la yale maneno yanayofahamika na wote, wasomi na majahili. Kundi hili ni lile la aya zilizo wazi ambazo ni bayana kwa kila mtu na wala hazina maana nyingine zaidi ya moja ambapo kila mtu huwa na uwezo wa kufahamu maana yazo. Kisha Imam aliashiria kundi la pili la maneno ya Mwenyezi Mungu ambayo yanajumuishwa kwenye aya za mifano ambazo ni za kina na kusema kuwa hakuna anayefahamu maana ya aya hizo isipokuwa wale watu ambao Mwenyezi Mungu amesafisha akili zao, kunyorosha hisia zao na kuweka sawa uchanganuzi wao katika wale ambao Mwenyezi Mungu amefungua vifua vyao kwa ajili ya Uislamu. Kisha Imam Ali (as) aliashiria kundi la tatu la maneno yake Mwenyezi Mungu ambalo ni la kufasiri na kufafanua maana halisi ya Qur’ani na kusema kuwa kundi hili la maneno halifahamiki isipokuwa na Mwenyezi Mungu mwenyewe na walinda amana wake waliobobea kwenye elimu.

Na tunaona hapa kwamba Imam Ali (as) ametumia neno ‘walinda amana’ kama ishara kwamba waliobobea kwenye elimu wamekingwa na kitendo cha wao kutumia ufafanuzi wa Qur’ani Tukufu katika kutafuta fitina na kuwafanya watu wawaabudu na kuwa watumwa wao. Hili ndilo jambo analolibainisha Imam Ali (as) anapobainisha maana ya Mwenyezi Mungu kugawa maeneo yake katika makundi tuliyoyataja kuhusu Qur’ani Tukufu. Anasema kuwa Mwenyezi Mungu aligawa maneneo yake katika makundi hayo ili kuepusha waovu walionyakua nafasi za uongozi wa umma wa Kiislamu kutumia vibaya nafasi ya ufafanuzi wa Qur’ani katika kupotosha, kunyanyasa na kuwafanya watu kuwa wafuasi na watumwa wao.

 

Imepokelewa katika kitabu cha Baswair ad-Darajaat kwamba Anas bin Malik alisema kuwa Mtume Mtukufu (saw) alimwambia Imam Ali (as): ‘Ewe Ali! Wewe utawafundisha watu yale wasiyoyajua katika maana ya Qur’ani. Imam Ali (as) akasema: ‘Nifikishe ujumbe upi katika ujumbe wako baada yako ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu? Mtume (saw) akasema: Wafahamishe watu mambo wasiyoyaelewa katika ufafanuzi wa Qur’ani.’ Na Imam Baqir (as) amenukuliwa katika vitabu vya al-Kafi na Baswair ad-Darajaat akifafanua kauli ya Mwenyezi Mungu inayosema,…..na wala hapana anayejua maana yake ila Mwenyezi Mungu na waliozama katika elimu, kwamba: ‘Mtume (saw) ndiye mmbora wa waliozama katika elimu. Mwenyezi Mungu alimfundisha mambo yote aliyomteremshia, ya ufunuo na maana zake. Hakumteremshia jambo ambalo hakumfundisha maana yake na mawasii wake pia baada yake waliyajua hayo yote……. Na Qur’ani ina mambo mahususi na ya jumla, ya wazi na ya mifano na yaliyofuta na yaliyofutwa na waliozama katika elimu wanayajua haya.’

Imam Jaffar (as) pia amenukuliwa na Thiqatul Islam al-Kuleini katika kitabu cha Raudhat al-Kafi akiwaambia masahaba zake watambue kwamba Mwenyezi Mungu hakumruhusu mtu yoyote kufafanua dini yake tukufu kwa kutumia matamanio, maoni binafsi au kukisia mambo na kwamba aliteremsha kitabu kitakatifu cha Qur’ani na kuwateu waja wake wema na watoharifu ambao aliwapa jukumu la kufafanau na kuwafahamisha wanadamu maana halisi ya maneno ya Yake yaliyotajwa kwenye kitabu hicho. Anasema kuwa wema hao ambao ni Mtume na Ahlul Beit wake watukufu ndio waja wema wanaokusudiwa na ambao Mwenyezi Mungu aliwajaalia kuwa viongozi na kuutaka umma wote wa Kiislamu kuwafauata katika kila jambo wanalowaamrisha kulifuata, katika yale wanayoyajua na wasiyoyajua. Hii ni kwa sababu wema hawa tayari wameongozwa na Mwenyezi Mungu mwenyewe na wala hawawezi kufanya kosa katika yale wanayowafundisha wafuasi wao kwa sababu tayari wapewa kinga tosha na Mwenyezi Mungu, kinga ambayo huwazuia kufanya kosa wala kufuata matamanio yao binafsi wanapotekeleza majukumu yao ya kuuongoza umma wa Kiislamu katika njia nyoofu ya kuulekea kwa Muumba wao.

Na kufikia hapa wapenzi wasikilizaji ndio tunahitimisha kipindi hiki cha Maswali Yetu na Majibu ya Thaqalain ambacho kimekujieni kupitia Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inayokutangazieni kutoka mjini Tehran. Basi hadi tutakapokutana tena juma lijalo panapo majaaliwa, tunakuageni nyote kwa kusema, Wassalaam Aleikum Warahmatullahi Wabarakatuh.