Sep 21, 2016 07:01 UTC
  • Usekulari Katika Mizani ya Uislamu (23)

Ni matumaini yangu kuwa hamjambo wapenzi wasikilizaji popote pale mlipo. Karibuni kusikiliza kipindi hiki, ambacho lengo lake ni kuuchambua Usekulari kwa kutumia mizani ya mafundisho ya Uislamu ili kuweza kuelewa kasoro, dosari na udhaifu wa fikra na nadharia hiyo ambayo chimbuko lake ni Ulimwengu wa Magharibi. Ni mategemeo yangu kuwa mtanufaika na kuelimika na yale mtakayoyasikia katika kipindi hiki. Endeleeni kuwa pamoja nami basi kuitegea sikio sehemu hii ya 23 ya mfululizo huu.

Katika vipindi kadhaa vilivyopita tumeanza kuzungumzia maudhui ya haki za binadamu na Usekulari; na tukasema kuwa Tangazo la Dunia la Umoja wa Mataifa la Haki za Binadamu limepitishwa kwa kufuata misingi ya Usekulari na Umwanadamu, na limekosolewa na wengi si katika Ulimwengu wa Kiislamu pekee bali hata wanafikra wa Magharibi pia. Aidha tukaashiria kwamba chanzo cha hitilafu nyingi za mitazamo katika maudhui ya haki za binadamu ni kutofautiana katika mtazamo juu ya ulimwengu na kumtambua mwanadamu; na tukasema haiyumkiniki kutoa maoni kuhusiana na mahitaji na haki za mwanadamu bila ya kuitambua kwanza hakika halisi ya kiumbe huyo. Moja ya nukta za msingi katika fikra ya Usekulari ni kupuuza uhusiano wa mtu na asili na marejeo yake; na ni kutokana na msingi huu wa haki za binadamu za Usekulari kiumbe mwanadamu anazingatiwa kuanzia wakati wa kuzaliwa hadi kufa kwake tu. Lakini dini ya Uislamu inamtambulisha mwanadamu kuwa ni kiumbe chenye hali na pande mbili za kimaada na kimaanawi, akiwa na roho itokayo kwa Mungu na ya kubakia milele. Kwa mtazamo wa Uislamu ustahiki alionao mtu kutokana na fitra, yaani upande wa kiroho aliojaaliwa na Mwenyezi Mungu ndio asili na msingi wa haki za binadamu. Ni kinyume na nadharia ya Usekulari ambayo imeyafanya matashi na matamanio ya binafsi na ya kimaada ya mtu kuwa asili ya haki za binadamu. Ili kumtambua mwanadamu na thamani zake, Usekulari unatumia njia ya jarabati na akili ya kiuwenzo ya mwanadamu, ambavyo ni vitu vinavyoweza kufanya makosa na vina mpaka wa kiuwezo. Lakini wanafikra wa Kiislamu wanaitakidi kuwa wahyi, kama ilivyo akili ni aina mojawapo ya wenzo wa maarifa na utambuzi ambao chimbuko lake ni Muumba wa ulimwengu na ambao hauna uwezekano wowote wa kukosea na kufanya makosa. Wahyi unajumuisha pia masuala ya upeo wa juu zaidi ya uwezo wa akili na wa kijarabati wa mwanadamu. Ndiyo kusema kuwa katika kumtambua mwanadamu na haki zake, haki za binadamu za Usekulari zimejikosesha chanzo na marejeo ya uhakika zaidi ya maarifa na utambuzi, yaani "wahyi". Lakini Uislamu unanufaika na chanzo hicho.

 

Baada ya kuelezea muhtasari wa yale tuliyoyazungumza katika vipindi kadhaa vilivyopita, katika kipindi chetu cha leo tutaendelea kutaja tofauti nyengine zilizopo kati ya haki za binadamu za Usekulari na haki za binadamu za Kiislamu. Haki za binadamu za Kimagharibi zimepuuza thamani na tunu za kimaadili na kuamua kuzitenganisha haki za mtu na uga wa thamani za kiutu. Kulingana na fikra ya Usekulari anuai za ufisadi na ufuska ni mambo yanayoruhusika; na maana ya uhuru wa mtu binafsi inaelezwa kuwa ni kutojali kitu na kujivua na vizuizi vya kiakhlaqi na kidini. "Uhuru wa binafsi" ni thamani na tunu mutlaki inayozitangulia thamani nyengine za kiutu kama usawa, uadilifu, imani na sifa tukufu za kiakhlaqi. Maana na madhumuni ya utangulizwaji huu ni kwamba haikubaliki na haiwezekani kuubana uhuru binafsi wa watu kwa kisingizio cha kulinda yoyote ile kati ya thamani hizo. Ni kwa sababu hiyo uteteaji uhuru binafsi wa mtu kwa sura ya kufurutu mpaka na vilevile ukanaji wajibu na majukumu ndio muelekeo unaoshuhudiwa kwenye takribani vipengee vyote vya Tangazo la Dunia la Haki za Binadamu. Mtakumbuka kuwa katika kuzungumzia uhuru wa mtu binafsi tulidokeza kwamba kwa mujibu wa mafundisho ya Uislamu, uhuru huo kwa mtu sio lengo bali ni wenzo wa kufikia ghaya na lengo stahiki kwa mwanadamu. Katika jicho la Uislamu, kukidhi matashi na matamanio ya nafsi sio lengo kwa mwanadamu, lakini ustahiki wa kiumbe huyo ni kufikia ukamilifu wa kiutu na saada ya milele. Kwa hivyo uhuru wa mtu binafsi ni utangulizi wa ukamilifu wa mwandamu si ukamilifu wenyewe. Uislamu unautafsiri uhuru wa mtu binafsi unaoendana na lengo hili. Na ndiyo kusema kuwa haki bora na ya juu kabisa ya mtu ni ya kuhakikisha hakuna kitu chochote kinachozuia irada ya uhuru wake binafsi kwa ajili ya kufikia "ukamilifu stahiki wa kiutu". Ufuataji mutlaki wa matamanio ya kinafsi, kusahau asili na marejeo ya mwanadamu na kutomjali Muumba wa ulimwengu ndivyo vizuizi vikuu vinavyomfanya mwanadamu aporomoke kutoka kwenye hadhi na daraja yake ya utu. Kwa hivyo kuufanya uhuru mutlaki wa mtu binafsi katika kukidhi na kuridhisha matamanio yake ya nafsi kuwa ndio haki ya msingi zaidi ya binadamu na kuzifanya thamani na sifa za kiutu kuwa kitu kisicho na hadhi wala nafasi yoyote, ni mambo ambayo hayakubaliki kwa mtazamo wa Uislamu. Kwa mtazamo wa Uislamu kufikia ukamilifu mtu ndicho kipimo kinachoainisha yenye maslaha na madhara kwake; na ili kujua ni ukamilifu upi anaostahiki mwanadamu na pia ili kuweza kutambua njia za kufikia na vizuizi vinavyokwamisha kuufikia ukamilifu huo, mbali na akili ya mtu, kuna ulazima pia wa kuwa na wahyi wa Mwenyezi Mungu. Wahyi utokao kwa Allah ni dira inayomuongoza na kumuonesha mtu njia sahihi za kufikia ukamilifu na vilevile katika harakati ya kuelekea kwenye ukamilifu huo unamwekea maagizo ya kufuata katika sura ya maamrisho na makatazo ya kimatendo. Maamrisho hayo ya kutekelezwa na makatazo hayo ya kujiepusha nayo, kidhahiri yanamwekea mipaka mtu, lakini ukweli ni kwamba yanamkomboa na kumweka huru na utumwa wa kutii hawaa na matamanio ya nafsi au kuwa mtumwa wa matakwa ya watu wengine. Kwa hiyo katika mtazamo wa fikra ya Kiislamu kulinda thamani na sifa za kikhlaqi za kiutu ni haki ya mwanadamu; kinyume na fikra ya Usekulari ambayo kutokana na kukana utukufu mutlaki wa thamani za kiutu na badala yake kuyafanya matakwa ya mwanadamu kuwa ndio msingi wa kila kitu, umefikia hadi ya kutetea vitendo vichafu kabisa ya kiakhlaqi yakiwemo maingiliano ya kimwili ya watu wa jinsia moja na kuyachukulia kuwa miongoni mwa haki za wazi kabisa na kimaumbile za mwanadamu.

 

Mtazamo wa kisekulari wapenzi wasikilizaji, ni wa kukwepa wajibu na uwajibikaji na unachojali ni mtu kuwa na “haki” tu basi. Lakini hakika ya mambo ni kuwa “haki” na “wajibu” ni watoto pacha au ni pande mbili za sarafu moja. Kwa mtazamo wa Uislamu mwanadamu ana wajibu na mas-ulia mbele ya Mwenyezi Mungu, mbele ya wanadamu wenzake na hata mbele ya ulimwengu wa maumbile na neema kadha wa kadha alizopewa na Mola. Tunapomchukulia mtu kuwa na haki fulani, maana yake ni kwamba tumembebesha mtu mwengine mzigo wa wajibu kwa mtu huyo. Mathalani, tunapozungumzia haki ya mtoto ya kupata elimu, huwa wakati huohuo tunazungumzia wajibu wa wazazi na jamii wa kumpatia elimu mtoto huyo. Kama tulivyotangulia kusema, katika haki za binadamu za Usekulari hakujazungumzwa chochote kuhusu ‘wajibu’. Kulingana na mtazamo huu, haki na wajibu ni vitu vinavyogongana; kwa hivyo tunapompangia mtu wajibu wa kufanya, maana yake ni kukiuka haki zake na uhuru wake wa binafsi.  Wapenzi wasikilizaji, sehemu ya 23 ya kipindi cha Usekulari Katika Mizani ya Uislamu imefikia tamati. Katika sehemu ijayo ya 24 ya kipindi hiki tutakuja kuangalia mtazamo wa Uislamu juu ya maudhui hii ya haki na wajibu. Msiache kujiunga nami wiki ijayo inshallah katika siku na saa kama ya leo.

Tags