Jumamosi, 22 Oktoba, 2016
Leo ni Jumamosi tarehe 20 Mfunguo Nne Muharram 1438 Hijria mwafaka na tarehe 22 Oktoba mwaka 2016 Miladia.
Siku kama ya leo miaka 170 iliyopita, Mirza Taqi Khan Amir Kabir aliuzuliwa cheo cha Kansela. Alikuwa mmoja wa wanasiasa wa Iran katika kipindi cha utawala wa Qajar. Kipindi fulani alikuwa Kansela wa Naser al-Din Shah mfalme wa wakati huo wa Iran. Amir Kabir alikuwa mtu huru, mwenye imani, muenezaji wa elimu na mwenye kupenda utamaduni na anahesabiwa kuwa mmoja wa waasisi wa marekebisho na waenezaji wa fikra bora katika uwanja wa ufundishaji, malezi na utamaduni nchini Iran. Amir Kabir alifanya juhudi kubwa katika njia ya mafanikio ya wananchi wa Iran na katika kipindi alichokuwa Kansela alitoa huduma na kufanya marekebisho mengi. Aidha alifanya juhudi kubwa za kuzuia uingiliaji wa madola ya kigeni katika masuala ya ndani ya Iran. ***

Katika siku kama ya leo miaka 110 iliyopita, Paul Cezanne mchoraji maarufu wa Kifaransa aliaga dunia akiwa na umri wa miaka 67. Alikuwa na shauku na mapenzi makubwa na fani ya uchoraji tangu akiwa mdogo, lakini kutokana na msisitizo wa baba yake aliingia Chuo Kikuu na kusoma taaluma ya sharia. Hatimaye akiwa na umri wa miaka 24, baba yake alimruhusu kuendelea na masomo katika fani ya uchoraji. Mwanzoni mabango ya uchoraji ya Paul Cezanne hayakupata wafuasi wengi na athari zake za uchoraji zilikabiliwa na ukosoaji mkubwa. Mwenendo huo uliendelea hadi alipofikisha umri wa miaka 50 ambapo hatua kwa hatua alianza kupata umashuhuri kutokana na kuuza mabango yake ya uchoraji. ***

Miaka 67 iliyopita katika siku kama ya leo yaani tarehe Mosi Aban 1328 Hijria Shamsia chama cha The National Front cha Iran kiliasisiwa na Dakta Mohammad Mosaddegh. Tarehe 18 Aban 1328, wanasiasa 19 akiwemo Dakta Mosaddegh walikusanyika ndani ya makao ya utawala kulalamikia uchaguzi wa duru ya 16 ya Bunge la Taifa la Iran. Natija ya msimamo wao huo, ilikuwa ni kubatilishwa matokeo ya uchaguzi wa Bunge mjini Tehran na viunga vyake. Baada ya chama cha The National Front kuingia Bungeni kilichukua usukani wa vita dhidi ya ukoloni kwa taifa la Iran kikipata himaya na uungaji mkono wa Maulama na wananchi. Hatua muhimu iliyofikiwa katika kipindi hicho kwa kuwa mstari wa mbele chama hicho ni kutaifishwa sekta ya mafuta hapa nchini na kufanywa kuwa mali ya taifa. ***

Siku kama ya leo miaka 41 iliyopita, aliaga dunia Arnold Joseph Toynbee mwanahistoria mtajika wa Uingereza. Alizaliwa mwaka 1889. Toynbee alikuwa akifundisha taaluma ya Historia ya Kimataifa katika Chuo Kikuu cha London. Msomi huyo ameandika vitabu vingi katika uga wa historian a baadhi ya vitabu vyake ni A Study of History, Change and Habit, Choose Life na Civilization on Trial. ***

Na miaka 39 iliyopita Ayatullah Sayyid Mustafa Khomeini, mtoto mkubwa wa Imam Khomeini muasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran aliauawa shahidi nyumbani kwake huko Najaf Iraq kwa njama za maafisa usalama wa utawala wa Shah. Mustafa Khomeini alizaliwa mjini Qum mwaka 1930 na baada ya kumaliza masomo ya awali, alianza kusoma masomo ya dini katika Chuo Kikuu cha Kidini mjini humo. Kutokana na ufahamu na upeo mkubwa wa masomo aliokuwa nao alizikwea haraka mno daraja za kielimu. Mustafa Khomeini alifikia daraja ya Ijtihadi akiwa na umri wa miaka 27. Alikuwa mwalimu katika Chuo Kikuu cha Kidini mjini Najaf Iraq kwa muada wa miaka 10. Katika kipindi kigumu cha mapambano Mustafa Khomeini alikuwa kando ya baba yake hadi alipouawa shahidi katika siku kama ya leo na vibaraka wa utawala wa Shah. ***
