Jumatatu, 7 Novemba, 2016
Leo ni Jumatatu tarehe 7 Safari 1438 Hijria sawa na tarehe 7 Novemba 2016.
Siku kama ya leo miaka 1310 iliyopita alizaliwa Imam Mussa al-Kadhim (as) ambaye ni mmoja kati ya wajukuu watukufu wa Bwana wetu Muhammad (saw). Alilewa na baba yake Imam Ja'far Swadiq (as) na kupata elimu na maarifa ya Kiislamu kutoka kwa mtukufu huyo kwa kipindi cha miaka 20. Baada ya kuuawa shahidi baba yake, Imam Kadhim (as) alishika hatamu za Uimamu na uongozi wa Umma wa Kiislamu kwa kipindi cha miaka 35 na kukabiliana na mashaka mengi. Imam Kadhim (as) alipitisha kipindi kikubwa cha umri wake katika kuwazindua na kuwaelimisha Waislamu maarifa asili ya dini. Suala hili liliwatia hofu kubwa watawala wa Bani Abbas ambao walimkamata na kumfunga jela ili kumuweka mbali na Waislamu waliokuwa na kiu ya maarifa halisi ya dini yao. Imam Kadhim (as) alisifika kwa ukarimu mkubwa, uvumilivu na usamehevu. Tunatoa mkono wa baraka kwa Waislamu wote kwa mnasaba wa kuadhimisha siku hii muhimu ya kuzaliwa mtukufu huyo.
Siku kama ya leo miaka 149 iliyopita, Madam Escudo Doska ambaye baadaye alikuwa maarufu kwa jina la Marie Curie alizaliwa huko Warsaw mji mkuu wa Poland. Baba yake alikuwa profesa wa fizikia na baadaye Madam Curie pia alielekea Paris, Ufaransa kwa ajili ya kuendeleza masomo yake katika taaluma hiyo hiyo ya baba yake. Madam Curie alifunga ndoa na Pierre Curie mwanafikizikia wa Ufaransa wakati alipokuwa masomoni katika Chuo Kikuu cha Sorbonne. Hatimaye mwanamama huyo alifanikiwa kuvumbua mada ya radium baada ya utafiti miaka mingi. Ni vyema kuashiria hapa kuwa Madam Curie alitunukiwa tuzo ya Nobel mara mbili katika taaluma za fizikia na kemia na aliaga dunia mwaka 1934.
Katika siku kama ya leo miaka 60 iliyopita, vita vya mfereji wa Suez vilimalizika baada ya uingiliaji kati wa Umoja wa Mataifa. Vita hivyo vilianza baada ya wanajeshi wa utawala wa Kizayuni wa Israel kushambulia jangwa la Sinai na kufuatia mashambulizi ya askari wa miavuli wa Uingereza na Ufaransa katika eneo la kanali hiyo. Serikali hizo tatu zilizotajwa zilianzisha vita hivyo kufuatia hatua ya rais wa wakati huo wa Misri, Jamal Abdul-Nassir, kuutaifisha mfereji huo.
Siku kama ya leo miaka 27 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 7 Safar 1342 Hijria, alifariki dunia Ayatullahil Udhma Sayyid Shahabuddin Mar-ashi Najafi mmoja wa Marajii na viongozi wa juu wa Kiislamu hapa nchini, akiwa na umri wa miaka 96. Alimu huyo alisoma elimu za fiqihi, Usul Fiqihi, hadithi, tafsiri ya Qur'ani, teolojia na misingi ya kimaadili katika vyuo vikuu vya kidini katika miji ya Kadhmein na Najaf, Iraq. Moja ya athari kubwa zilizoachwa na Ayatullah Mar-ashi Najafi ni maktaba kubwa ya vitabu iliyoko mjini Qum, ambayo inahesabiwa kuwa ya aina yake. Mwanazuoni huyo pia daima alikuwa muungaji mkono wa Imam Khomeini na harakati ya Mapunduzi ya Kiislamu ya wananchi wa Iran.