Nov 19, 2016 02:36 UTC
  • Jumamosi, Novemba 19, 2016

Leo ni Jumamosi tarehe 19 Mfunguo Tano Safar 1438 Hijria inayosadifiana na tarehe 19 Novemba 2016 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 1267 iliyopita yaani tarehe 19 Safar mwaka 171 Hijria  alizaliwa Abu Ma'ashar Balkhi mmoja kati ya wanajimu na wasomi wakubwa wa elimu ya nujumu wa Kiirani. Kutokana na mapenzi makubwa aliyokuwa nayo ya elimu ya nujumu alielekea Baghdad na kuanza kusoma elimu hiyo. Abu Ma'ashar Balkhi alitumia vyanzo vya lugha za Kiarabu, Kihindi, Kigiriki na Kisiriani kwa ajili ya kupata elimu ya nujumu na mnajimu mashuhuri zaidi katika zama zake. Kazi zake katika taaluma hiyo zilitumiwa kwa karne kadhaa katika ulimwengu wa Kiislamu na Kimagharibi hata baada ya kufariki kwake dunia. Miongoni mwa vitabu mashuhuri vya msomi huyo wa Kiislamu ni al-Madkhal al-Kabir na al-Mawalidul al Saghirah.***

Unajimu

Katika siku kama ya leo miaka 108 iliyopita, Sayyid Jamaluddeen Waidh Isfahani mtoa waadhi mashuhuri wa Kiirani aliuawa. Alizaliwa mjini Hamedan. Akiwa na lengo la kujiendeleza kielimu alielekea Isfahan akiwa na umri wa miaka 20 na baadaye kachagua makazi yake kuwa mjini Tehran.  Sayyid Jamaluddeen Waidh Isfahani alikuwa akitoa hotuba na mihadhara katika miji ya Isfahan, Mash'had, Shiraz na Tehran. Kutokana na mwaidha yake kuleta mwamko baina ya watu, Muhammad Ali Shah alitoa amri ya kutiwa mbaroni alimu huyo. Baada ya kushikiliwa jela kwa miezi kadhaa hatimaye mwaka 1326 Hijria aliuawa akiwa na umri wa miaka 45. ***

Katika siku kama ya leo miaka 55 iliyopita Ayatullahj Sayyid Murtadha Langeroodi mmoja wa wanazoni na walimu wakubwa wa Kiislamu alifariki dunia. Alizaliwa mwaka 1306 Hijria Shamsia katika viunga vya mji wa Langarud moja ya miji ya kasakzini mwa Iran. Alielekea katika mji wa Qazvin akiwa katika rika la ujana kwa ajili ya masomo. Ayatullah Langeroodi baadaye alisoma elimu mbalimbali kwa walimu mashuhuri wa zama hizo mjini Tehran.  Baadaye alielekea mjini Najaf Iraq. Hatimaye alipata daraja ya Ijtihadi na kuwa miongoni mwa walimu na Ulamaa watajika katika Chuo Kikuu cha Kidini mjini Najaf. Kipindi fulani alikuwa akifundisha pia katika Chuo Kikuu cha Kidini mjini Qum. Ayatullah Sayyid Murtadha Langeroodi ameacha vitabu vingi alivyoviandika katika maudhui mbalimba. ***  

Indira Ghandhi

Miaka 99 iliyopita katika siku kama ya leo, alizaliwa huko Allah Abadi nchini India, Bi Indira Gandhi binti pekee wa Jawaharlal Nehru. Mwaka 1947 baada ya India kupata uhuru kutoka kwa mkoloni Mwingereza na baba yake kuwa Waziri Mkuu wa India, Indira Gandhi alikuwa na nafasi muhimu kando ya baba yake. Mwaka 1964 baada ya kufariki dunia baba yake, Indira Gandhi aliteuliwa katika serikali ya Lal Bahadur Shastri kuwa Waziri wa Habari, Radio na Televisheni. Bi Indira Gandhi alikuwa Waziri Mkuu wa India kuanzia mwaka 1966 hadi 1984 alipouawa. ***

Miaka 39 iliyopita katika siku kama ya leo, Anwar Sadat Rais wa wakati huo wa Misri alifanya safari katika Baitul Muqaddas huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu. Hiyo ilikuwa safari ya kwanza kufanywa na Rais wa nchi ya Kiarabu katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu. Safari hiyo ilifanyika katika fremu ya kujikurubisha Misri kwa utawala haramu wa Israel. Safari ya Anwar Sadat iliwakasirisha mno Waislamu hasa wananchi wa Palestina. Licha ya hali hiyo mwaka 1978 Anwar Sadat alitiliana saini mkataba wa Camp David na utawala huo ghasibu kwa usimamizi wa Marekani. Nchi nyingi za Kiarabu na baadhi ya nchi za Kiislamu zilikata uhusiano na serikali ya Misri zikionyesha kuchukizwa na hatua hiyo ya Sadat ambayo pia ilizusha machafuko na ghasia nchini Misri kwenyewe. Hatimaye mwaka 1981 Khalid Islambuli aliyekuwa afisa katika jeshi la Misri alimpiga risasi na kumuua Sadat akipinga hatua yake ya kutia saini mkataba muovu wa Camp David. ***

NATO

Na katika siku kama ya leo miaka 26 iliyopita, viongozi wa Jumuiya za Kujihami ya Nchi za Magharibi (NATO) na Warsaw walitiliana saini maafikiano ya usalama mjini Paris, Ufaransa. Mkataba huo ulihitimisha vita baridi baina ya kambi mbili za Magharibi na Mashariki. Viongozi wa kambi hizo pia walikubaliana kumaliza vita vya propaganda kati yao na kupunguza silaha za jumuiya mbili hizo za kijeshi.

 

Tags