Dec 06, 2016 10:08 UTC
  • Maswali Yetu na Majibu ya Thaqalain (146)

Assalaam Aleikum wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inayokutangazieni kutoka hapa mjini Tehran.

Ni furaha yetu kwamba tumepata wasaa mwingine wa kujumuika nanyi katika kipindi hiki cha itikadi kwa mujibu wa mafundisho ya dini tukufu ya Kiislamu. Katika kipindi hiki tutaedelea kuzungumzia suala ambalo tumelizungumzia katika vipindi viwili vilivyopita kuhusiana na majukumu tuliyonayo sisi Waislamu kwa Maimamu wetu watukufu (as) ambao ndio waliorithi nafasi ya Mtume Mtukufu (saw) baada ya kuondoka kwake humu duniani. Katika vipindi hivyo maandiko matakatifu yalituongoza na kutuwezesha kujua majukumu mawili kati ya majukumu hayo muhimu, la kwanza likiwa ni la kuwatii moja kwa muja na bila ya masharti yoyote, ambapo kufanya hivyo ni sawa na kumtii Mweyezi Mungu na Mtume wake (saw). Utiifu huu unatulazimu kuwafauata watukufu hao katika kila jambo wanalotuamrisha kulifanya au kuliacha, na kufuata mifano ya matendo na tabia zao katika maisha yetu ya kila siku.

Wajibu wa pili ni kuwarejea wao katika kila hitilafu na ugomvi unaotokea miongoni mwetu ili wapate kutusuluhisha kwa msingi wa mafundisho ya Qur’ani Tukufu kwa sababu wao ndio wajuzi zaidi wa hukumu za kitabu hicho cha mbinguni na ambacho kinabainisha kila jambo, liwe dogo au kubwa. Ni wazi kuwa kufanya hivyo na kuwafuata katika kila jambo hutuepusha na hitilafu na ufuataji wa njia za shetani muovu. Baada ya kujua wajibu hizo mbili, tunauliza wajibu wa tatu ni upi? Karibuni tutafute kwa pamoja wajibu huu kutoka kwenye maandiko matakatifu.

 

Ndugu wapendwa, wajibu wa tatu ambao tunapata kuufahamu kutokana na maandiko matakatifu ni wajibu wa kuwapenda Ahlul Beit, yaani Watu wa Nyumba na Bwana Mtume (as). Jambo hili limebainishwa wazi na aya ya 23 katika Surat as-Shura ambapo Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema:

ذَلِكَ الَّذِي يُبَشِّرُ اللَّهُ عِبَادَهُ الَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ قُل لّا أَسْأَلُكُمْ عَلَيْهِ أَجْرًا إِلاَّ الْمَوَدَّةَ فِي الْقُرْبَى وَمَن يَقْتَرِفْ حَسَنَةً نَّزِدْ لَهُ فِيهَا حُسْنًا إِنَّ اللَّهَ غَفُورٌ شَكُورٌ

Hayo ndiyo aliyowabashiria Mwenyezi Mungu waja wake walioamini na wakatenda mema. Sema: Kwa haya sikuombeni malipo yoyote kwenu ila mapenzi katika ndugu (watu wa karibu). Na anayefanya wema tutamzidishia wema. Hakika Mwenyezi Mungu ni Msamehevu Mwenye shukrani.

Kwa hivyo utekelezwaji wa jukumu na wajibu huu, kama inavyosisitiza aya hii ndio wema ambao Mwenyezi Mungu anamzidishia mwenye kuutekeleza, wema mwingine na kumzidishia baraka Zake. Na hii ndio njia ya kujikurubisha kwa Mweyezi Mungu Mtukufu kama inavyosisitiza hilo aya ya 57 ya Surat al-Furqan inayosema:

قُلْ مَا أَسْأَلُكُمْ عَلَيْهِ مِنْ أَجْرٍ إِلاَّ مَن شَاء أَن يَتَّخِذَ إِلَى رَبِّهِ سَبِيلا

Sema: Sikukuombeni ujira juu yake; ila atakaye na ashike njia iendayo kwa Mola wake Mlezi.

Hii ina maana kwamba matunda na faida ya kuwa na mapenzi ya aina hii kwa Watu wa Nyumba ya Mtume (saw) na kufanya juhudi za kuyaimarisha na kuyakitisha mizizi kwenye moyo, humrejea mtu anayetekeleza wajibu huu mwenyewe, sawa kabisa na kama anavyonufaika na faida zinazotokana na utekelezaji wa majukumu mengine yote yaliyoamrishwa na MwenyezI Mungu.

Na hili ni jambo ambalo linabainishwa wazi na aya ya 47 ya Surat Saba kuhusiana na mapenzi haya ya lazima na wajibu, ambapo Mwenyezi Mungu anasema:

قُلْ مَا سَأَلْتُكُم مِّنْ أَجْرٍ فَهُوَ لَكُمْ إِنْ أَجْرِيَ إِلاَّ عَلَى اللَّهِ وَهُوَ عَلَى كُلِّ شَيْءٍ شَهِيدٌ

Sema: Ujira niliokuombeni ni wenu nyinyi. Sina ujira ila kwa Mwenyezi Mungu. Naye ni Shahidi juu ya kila kitu.

Ama kuhusiana na makusudio ya ndugu au kwa ibara nyingine watu wa karibu waliokusudiwa katika aya ya kwanza na ambao Mwenyezi Mungu amewajibisha mapenzi kwao, imethibiti kwamba ni wale walioashiriwa katika aya ya Tat’hir, yaani utakaso, ambao Mtume Mtukufu (saw) alikuwa tayari kuapishana na Wakristo wa Najran kwa majina yao katika mjadala uliozuka baina ya pande hizo. Watukufu hao ni wale ambao isma, yaani kutotenda dhambi na utakaso wao umethibiti na hivyo mapenzi kwao kufanywa kuwa zawadi kwa ujumbe wa Mtume Muhammad (saw).

 

Ndugu wasikilizaji, maulamaa na wanazuoni wengi wemethibitisha katika tafiti zao za kuaminika ubatili wa kauli nyinginezo zisizo na msingi ambapo baadhi ya watu wanaojaribu kufasiri Qur’ani Tukufu kwa matamanio na maslahi yao binafsi ya kutaka kuzua fitina baina ya Waislamu na hivyo kuwafanya wasiwapende Maimamu wa Nyumba ya Mtukufu Mtume (saw), wameifasiri aya ya Tat’hir kinyume kabisa na maana yake ya wazi na ya moja kwa moja.

Sisi hapa tutatosheka tu kwa kutaja hadithi moja muhimu na kamilifu ambayo imenukuliwa na mmoja wa wanazuoni wakubwa wa Kisuni ambaye si mwingie bali ni Jarullah az-Zamakhshari katika juzuu ya pili katika Tafsiri yake ya al-Kashif. Katika hadithi hiyo kuna ufafanuzi wa kuvutia wa Mtume Mtukufu kuhusiana na faida na baraka za kutekeleza wajibu huu muhimu wa kupeda na kuwafuata Maimamu wa nyumba yake. Az-Zamakhshari anasema hivi kuhusiana na sababu ya kuteremshwa aya ya mapenzi kwa Watu wa Nyumba ya Mtume (saw): ‘Washirikina walikusanyika katika moja ya vikao vyao na kusema: ‘Je, si mnaona Muhammad anataka apewe ujira wa yale anayoyatekeleza - yaani mashaka anayoyapitia katika kufikisha ujumbe wa Mwenyezi Mungu?’ Hapo ndipo aya hiyo ilipoteremka….. Aliendelea na mazungumzo yake na pakatamkwa: ‘Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu! Ni nani hawa watu wa karibu yako ambao inatuwajibikia sisi kuwapenda?’ Hapo Mtume (saw) alijibu kwa kusema: ‘Ni Ali na Fatumah na wana wao wawili. Pepo imeharamishwa kwa yule anayedhulumu Aali zangu na kuniudhi kuhusiana nao….’ Kisha akasema (saw) – katika hadithi nyingine kamilifu kuhusiana na athari za kutekeleza wajibu wa kuwapenda Ahlul Beit (as): ‘Hakika mtu anayekufa hali ya kuwa anawapenda Aali wa Muhammad, huwa amekufa shahidi, hakika mtu anayekufa hali ya kuwa anawapeda Aali wa Muhammad huwa amekufa hali ya kuwa amesamehewa dhambi zake, hakika mtu anayeaga dunia hali ya kuwa anawapenda Aali wa Muhammad huwa ameaga hali ya kuwa ametubu dhambi zake, hakika mtu anayaga dunia hali ya kuwa anawapenda Aali wa Muhammad huwa ameaga hali ya kuwa ni muumini aliyekamilisha imani yake, hakika mtu anayeaga dunia hali ya kuwa anawapeda Aali wa Muhammad hubashiriwa Pepo na Malakul Maut, kisha na Munkir na Nakir….’ Kisha Mtume (saw) aliendelea kwa kusema: ‘Hakika Mtu anayekufa hali ya kuwa anawapenda Aaali wa Muhammad husindikizwa kwa furaha kuelekea kwenye Pepo kama anavyosindikizwa bibi harusi kuelekea nyumba ya mumewe, hakika mtu anayeaga dunia hali ya kuwa anawapenda Aali wa Muhammad hufunguliwa milango miwili kwenye kaburi lake kuelekea Pepo, hakika mtu anayeaga dunia hali ya kuwa anawapenda Aali wa Muhammad Mweyezi Mungu hujaalia kaburi lake kuwa sehemu inayotembelewa na Malaika…..’

Sehemu ya pili ya hadithi hii muhimu na kamilifu ya Bwana Mtume (saw) inaashiria matokeo mabaya na machungu ya kupuuza na kutotekeleza wajibu huu wa kuwapenda Watu wa Nyumba ya Mtume (saw), ambapo Mtume mwenyewe anasema: ‘Hakika mtu anayeaga dunia hali ya kuwa anawachukia Aali wa Muhammad, siku ya Kiama atadhihiri hali ya kuwa pameandikwa machoni pake, ‘aliyekata tamaa na rejema ya Mwenyezi Mungu’, hakika anayekufa hali ya kuwa anawachukia Aali wa Muhammad huwa amekufa hali ya kuwa ni kafiri, hakika mtu anayekufa hali ya kuwa anawachukia Aali wa Muhammad hataonja harufu ya Peponi.’

 

Nukta mbili muhimu ambazo zinapasa kuashiriwa zinajitokeza hapa mpenzi msikilizaji ambapo ya kwanza ni kwamba mapenzi na mahaba kwa Watu wa Nyumba ya Mtume (saw) ambayo hukita moyoni yanatokana na maarifa, na dhihirisho la kivitendo la kutekelezwa wajibu wa mapenzi kwa watukufu hao ni kuwanusuru na kuwatetea ipaswavyo (as) wakati wa haja. Nukta ya pili ni kwamba makusudio ya aya ya Mahaba ni wale watukufu ambao wamezungumziwa katika aya za Tat’hir na Mubahala na kuenezwa makusudio ya aya mbili hizi kwa Maimamu wote 12 maasumu waliosalia katika Nyumba ya Mtume Muhammad kwa kutegemea dalili nyingi za kuaminika ambazo zinasisitiza wazi kwamba wao wote ni Aali wa Muhammad al-Mustafa (SAW) na ni watu wa karibu yake kama ilivyopokelewa katika hadithi za Maimamu kumi na wawili kupitia madhehebu yote mawili ya Shia na Suni.

Tunaongeza juu ya hayo hadithi zilizopokelewa kutoka kwa Maimamu wenyewe ambao Waislamu wote wanaafikiana juu ya ukweli na elimu yao ya juu na kamilifu kuhusiana na Kitabu cha Mwenyezi Mungu. Wote hao wameafikiana kwamba watukufu hao ndio kusudio la aya hii. Kwa mfano imepokelewa katika kitabu cha Mahasin kutoka kwa Imam Swadiq (as) kwamba amesema kuwa Mwenyezi Mungu alijaalia mahaba kwa Ahlul Beit (as) kuwa wajibu, na kisha akasoma aya ya ‘Mahaba’ kuthibitisha suala hilo. Na katika kitabu cha al-Kafi, Imam Baqir (as) ananukuliwa akisema kuhusiana na aya hiyo kwamba waliokusudiwa ni Maimamu (as). Kuna hadithi nyingine nyingi kama hizi ambazo zimepokelewa kutoka kwa Maimamu Zeinul Abideen, ar-Ridha na al-Mahdi (as) hadithi ambazo zinatosha na kumkinaisha kila mwenye kuzingatia.

 

Wapenzi wasikilizaji, natija tunayoipata kutokana na yale tuliyosoma kwenye kipindi hiki ni kuwa wajibu wa tatu tulionao kwa Maimamu watukufu wa Nyumba ya Mtume (as) ni kuwapenda wote kwa nyoyo zetu na kisha kuwanusuru kivitendo wakati wa haja.

Na kufikia hapa wapenzi wasikilizaji ndio tunafikia mwisho wa kipindi chetu cha juma hili cha Maswali Yetu na Majibu ya Thaqalain ambacho kama kawaida kimekujieni kupitia Idhaa ya Kiswahili Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inayokutangazieni kutoka mjini Tehran. Basi hadi tutakapojaliwa kukutana tena juma lijalo, tunakuageni nyote wapenzi wasikilizaji kwa kusema, Wassalaam Aleikum Warahmatullahi Wabarakatuh.