Dec 06, 2016 11:18 UTC
  • Familia Salama (19)

Hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni kujiunga nasi katika mfululizo huu wa makala kuhusu Familia salama. Makala hizi huangazia masuala mbali mbali ya afya ya familia kama vile lishe, mazoezi, madhara ya matumizi ya mihadarati, umuhimu wa mahaba katika familia n.k. Katika makala ya leo tutaangazia kuhusu kipindi cha kustaafu baada ya kuajiriwa. Karibuni kujiunga nasi hadi mwisho.

Katika makala yetu iliyopita tuliangazia maudhui ya zama za kustaafu na tukasema kuwa, kipindi hicho kina umuhimu mkubwa sawa na zama zingine katika maisha ya mwanadamu na kwa msingi huo, iwapo hakutakuwepo na mpango wa kimsingi kwa ajili ya kipindi hicho basi yamkini mwenye kustaafu akakumbwa na matatizo ya kiuchumi, kijamii na kiutamaduni. Iwapo mwenye kustaafu atakumbwa na matatizo jambo hilo litamuathiri vibaya yeye pamoja na familia, jamii na nchi nzima kwa ujumla. Tulimaliza kwa kusema kuwa kustaafu si mwisho wa njia bali ni mwanzo mpya katika maisha.

Kuingia katika kipindi hiki kipya katika maisha kwa kawaida huambatana na wasiwasi mkubwa. Kwa kawaida mabadiliko katika maisha yawe ni mazuri au mabaya huambatana na msongo wa mawazo au stress na mfadhaiko au depression.

Kipindi cha kustaafu kinatoa mwanya wa kuwa karibu zaidi na familia

 

Moja ya matukio katika maisha ambayo yamkini yakamsababishia matatizo mhusika yeyote ni kustaafu baada ya kuishia maisha ya kuajiriwa. Iwapo mhusika hatakuwa amejitayarisha kukabiliana ipasavyo na kipindi hiki maishani, basi atakumbwa na huzuni, majonzi, asiye na motisha wala furaha na asiyeridhika na hali yake mpya. Aidha atakuwa ni mwenye kutoa visingizio kwa matatizo yanayomkumba. Iwapo mhusika atasalimu amri mbele ya hali hiyo atakuwa hajali tena wakati wa kulala au kuamka na wala hatalipatia umuhimu suala la dhahiri yake. Kwa taratibu mtu kama huyu yamkini akapoteza marafiki zake.

Kinyume cha hali hiyo, kipindi cha kustaafu kikisimamiwa ipasavyo kinaweza kuwa kipindi cha mwanzo mpya katika maisha.  Inaweza kuwa ni dunia yenye siku zilizojaa fursa na furaha kwa mtu binafsi na walio karibu nayo. Mwenye kustaafu ambaye aghalabu huwa amefikia umri wa juu anaweza kuwa mwenye manufaa katika jamii kwa kukubali majukumu mbali mbali yanayoenda sambamba na umri wake. Hii ni kwa sababu mwenye kustaafu baada ya kufanya kazi kwa muda mrefu huwa amepata uzoefu muhimu na wenye manufaa katika jamii.

Wataalamu wa masuala ya jamii wanatoa ushauri kuwa, ili mwenye kustaafu asiwe na mfadhaiko wa nafasi au msongo wa mawazo, anaweza kutafuta jambo la kumshughulisha kifikra.

Hii ni kwa sababu iwapo mtu atashinda usiku kucha pasina kufanya lolote baada ya kuwa amehudumu kazini kwa miaka mingi, yamkini akakumbwa na matatizo ya kimawazo. Kwa hivyo wataalamu wanashauri kuwa mwenye kustaafu atafute jambo la kufanya katika siku hata kama hatalazimika kufika katika sehemu ya kufanyia kazi kwa wakati maalumu. Kwa mfano mwenye kustaafu anaweza kujishughulisha na kazi zisizo na malipo za kusaidia jamii kama vile mashirika ya kutoa misaada au katika maeneo ya ibada n.k.

 

Kwa mujibu wa uchunguzi uliofanywa na Chuo Kikuu cha Michigan nchini Marekani, raia wa Marekani ambao wanajishughulisha na kazi za kujitolea zisizo na malipo kwa lengo la kuwasaidia watu wasiojiweza katika jamii, huwa na umri mrefu kwa kiwango cha asilimia 60 ikilinganishwa na wenzao waliostaafu wasijishughulisha na chochote.

*********

Wapenzi wasikilizaji, shughuli nyingine ambayo waliostaafu wanaweza kufanya ni kukubali kuchukua nafasi ya kusaidia kuwalea wajukuu katika familia. Katika shughuli hii, waliostaafu wanaweza kuwa ni wenye kuwafunza wajukuu kuhusu mila, desturi na utamaduni pamoja na thamani za kimaadili. Tab'aan hilo litawezekana tu iwapo wenye kustaafu ni watu wenye maadili mema na ambao wanaweza kuwa mfano mzuri wa kuigwa na wajukuu.

Iwapo mwenye kustaafu atapuuza shughuli kama hiyo ya kulea wajukuu au kazi ya kujitolea katika jamii na mashirika ya misaada basi huenda akawa mpweke na mwenye kujitenga na kuhisi asiye na faida na jambo hilo litamsababishia msongo wa mawazo na mfadhaiko wa nafasi na yamkini akakumbwa na maradhi hatari kama vile Alzheimer. Ugonjwa huu ni miongoni mwa magonjwa ya ubongo yanayoathiri zaidi wazee au watu wa umri wa makamo. dalili za kawaida zinazotambuliwa ni kukosa uwezo wa kupata kumbukumbu mpya, kama vile matatizo ya kukumbuka mambo yaliyofanyika hivi karibuni. Ugonjwa unapoendelea, dalili huwa ni pamoja na kuchanganyikiwa, kukerwa na uchokozi, mabadiliko ya hali ya moyo, kutatizika kwa lugha, kupoteza kumbukumbu ya muda mrefu, na mgonjwa kujitenga sana kadiri hisia zake zinavyoendelea kupungua. Hatua kwa hatua, kazi za kimwili hupotea, na hatimaye kusababisha kifo.

Kwa hivyo, mbali na kujishughulisha na kazi mbali mbali za kujitolea na zisizo na shinikizo, jambo jingine ambalo mtu aliyestaafu anaweza kulifanya ili kuepuka ugonjwa wa Alzeima ni kuwa ni mwenye kufanya mazoezi ya kimwili na michezo.  Kufanya mazoezi sahali kama vile kutembea kwa kasi ya kilomita tano kwa saa kwa muda wa dakika 20 kila siku ni aina nzuri na sahali zaidi ya mazoezi ambayo huboresha mzunguko wa damiu mwilini na hivyo kuimarisha seluli za ubongo. Mazoezi kama hayo pia hupunguza mfadhaiko wa nafasi na wasiwasi. Hii ni kwa sababu wasi wasi na hofu huwa na athari mbaya ambazo huzeesha homoni kwa kasi.

 

Shughuli nyingine ambayo mwenye kustaafu anaweza  kujishguhulisha nayo ni kuwaalika na kuwatembelea jamaa na marafiki na kujuliana hali pamoja na kujadili masuala mbali mbali kadiri inavyowezekana. Hali hii ya kutembeleana na kujuliana hali humpa mwenye kustaafu motisha na bashasha.

Zaidi  ya hayo yote, wataalamu katika suala la kustaafu wanashauri kuwa, mwenye kustaafu ajihusishe na ibada pamona na kusoma dua na kutembelea mara kwa mara maeneo matakatifu na ya ibada kwani jambo hilo huimarisha mwili na roho na kumkinga mwanadamu na maradhi mengi ya kimwili na kiakili.

 

Tunamaliza kwa kauli ya Mtume Muhammad SAW aliyesema:

'Kila mzee katika kaumu yake ni kama mtume katika umma wake