Mar 01, 2016 12:00 UTC
  • Uislamu Chaguo Langu (93)

Hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni kujiunga nami katika makala hii inayoangazia watu ambao baada ya kufanya utafiti wa kina huamua kufuata njia ya haki na iliyojaa nuru katika maisha ya hapa duniani na kesho Akhera yaani Uislamu. Katika makala yetu ya leo tutamuangazia Mromania aliyesilumu Lucian Cojocaru. Karibuni kujiunga nami hadi mwisho.

Bw. Lucian Cojocaru anasema hivi kuhusu namna alivyosilimu: "Mimi na mama yangu kwa kawaida tulikuwa tukienda katika kanisa la Orthodox na tulikuwa tunajitahidi kujikurubisha kwa Mwenyezi Mungu SWT hasa kwa kuzingatia kuwa tulikuwa na matatizo mengi wakati huo. Pamoja na hayo mazingira ya pale kanisani hayakuridhisha lakini kutokana na kuwa tulihitajia dini tulilazimika kuvumilia hali ya mambo. Hatua kwa hatua kadiri muda ulivyosonga mbele tuliamua kufanya uchunguzi na utafiti kuhusu dini nyinginezo. Nilipoingia chuo kikuu niliweza kujifunza machache kuhusu Uislamu lakini kutokana na ufahamu duni kuhusu dini hii sikuweza kuifuata wakati huo. Hivyo niliamua kuendeleza utafiti wa kina zaidi na niliweza kupata mitandao kadhaa ya intaneti kuhusu Uislamu kwa lugha ya Kiingereza na Kiromania. Nilivutiwa na kushangazwa sana na mafundisho ya Uislamu. Niliweza kukijua kitabu kitukufu cha Waislamu yaani Qur'ani. Baada ya hapo nilipata hamu zaidi ya kuijua dini hii tukufu," anasema Mromania huyu aliyesilimu.
Qur'ani Tukufu ni Wahyi na ufunuo kutoka kwa Mwenyezi Mungu SWT kwa ajili ya wanaadamu wote ili wapata mwongozo na saada pamoja na ufanisi. Mafundisho ya kitabu hiki kitukufu yanaweza kumuongoza mwanaadamu na kukidhi mahitaji yake yote ya kisheria katika sekta zote za maisha. Iwapo mwanaadamu atatumia hekima na uwezo wake wa kiakili sambamba na utakasifu wa dhati katika moyo wake ili kutafuta ukweli, basi kwa yakini ataweza kudiriki na kutambua ukweli kuhusu njia inayoweza kumuelekeza katika saada na ufanisi. Ni kwa sababu hii ndiyo maana tunashuhudia namna Qur'ani Tukufu, kama alivyoadhidi Mwenyezi Mungu, imevyoweza kuhifadhika na sasa imeweza kuangazia nyoyo zaidi za wanaadamu. Bw. Cojocaru aliendeleza utafiti wake wa Qur'ani. Anafafanua zaidi kwa kusema: "Kutokana na kuendeleza utafiti wangu kuhusu Qur'ani katika intaneti niliweza kuijua zaidi dini tukufu ya Kiislamu. Tarjama ya Qur'ani Tukufu na vitabu nilivyopokea kutoka Idhaa ya Kiingereza ya Radio Tehran vilinisaidia sana kupata ufahamu bora kuhusu Uislamu. Bw. Cojocaru anaendelea kusimulia kwamba: Nilikuwa na hamu kubwa ya kuisoma na kuielewa Qur'ani kabla sijasilimu. Nilivutiwa sana na Aya za Qur'ani na Hadithi za Mtume SAW na nilizosoma kwa makini ili niweze kufahamu ni kwa nini baadhi ya watu wana uadui mkubwa sana dhidi ya Uislamu. Niliathiriwa pakubwa kutokana na kusoma kwa makini Qur'ani Tukufu na nilipata utulivu mkubwa wa kiroho kutokana na kumjua Mwenyezi Mungu na Mtume wake Mtukufu.
Katika kipindi cha utafuti wangu anaendelea kusema Mromania huyo, niliweza kutambua kuwa katika Qur'ani Tukufu imetumia lugha sahali na yenye kufahamika. Hiki ni kiabu ambacho tokea kuteremshwa kwake hakijaweza kupotoshwa au kubadilishwa hata kidogo na hilo ni kinyume cha kile kilicho katika Bibilia. Mromania huyu aliyesilimu anaongeza kuwa: "Kwa kweli nilifurahi sana kutokana na kuwa Qur'ani ina thamani nyingi ambazo zinapaswa kuzingatiwa na kuheshimiwa katika maisha. Aidha kitabu hiki kitukufu kimezingatia maisha ya hapa duniani na pia kesho Akhera. Kwa hakika Qur'ani Tukufu ni mwongozo kamili kwa ajili ya harakati sahihi katika jamii. Kitabu hiki kitukufu kimesisitiza kuhusu sheria za kijamii na kiuchumi katika jamii. Aidha Qur'ani Tukufu inaenda sambamba na maisha pamoja na sayansi za kisasa. Kitabu hiki ambacho kiliteremshwa zaidi ya miaka 1,400 iliyopita kinaashiria mambo ambayo yamevumbuliwa na wanasayansi miaka mingi baadaye. Kwa hakika Qur'ani Tukufu ni muujiza katika taaluma kama vile tiba, jiografia, nujumu n.k. na hiyo ni miongoni mwa ushahidi kuwa kitabu hiki ni neno la Mwenyezi Mungu. Aidha Qur'ani Tukufu imewataja Mitume wa Mwenyezi Mungu bila kubagua wakiwemo Manabii Issa na Mussa...Amani ya Mwenyezi Mungu iwe juu yao."
@@@
Mtume Mtukufu wa Uislamu ndie shakhsia wa juu zaidi katika historia ya mwanaadamu. Kuwaongoza wanaadamu kuelekea katika ufanisi na saada ni wadhifa mzito ambao Mwenyezi Mungu aliuweka katika mabega ya mwanaadamu mwenye hadhi ya juu; mtukufu huyo naye alitekeleza wadhifa wake ipasavyo. Mtume Muhammad SAW kwa mafundisho yake sahihi, aliweza kuiongoza dunia kuelekea katika nuru. Mromania aliyesilimu anasema alivutiwa sana na sira na maisha ya Mtume SAW. Anafafanua zaidi kwa kusema: "Nilisoma vitabu kadhaa kuhusu Uislamu na maisha ya Mtume SAW. Baada ya kuisoma sira ya maisha ya Mtume Mtukufu nilifikia natija kuwa yeye ni kigezo cha kipekee kwa wanaadamu wote. Maisha yake yaliyojaa nuru yalikuwa maisha ya utakasifu, yaliyojaa ukarimu, ushujaa na imani thabiti kwa Mwenyezi Mungu SWT. Kwa hakika yeye ni kigezo bora zaidi kwa wanadamu wote. Hayo yote yalinibainikia baada ya kusoma vitabu kuhusu shakhsia yake adhimu. Nilivutiwa sana na mfumo wa maisha, tabia na mwenendo wa Mtume SAW kwani alikuwa akizingatia sekta zote za maisha hata mavazi yake binafsi na aliendelea kuwa matakasifu na mcha Mungu hadi lahadha za mawisho za maisha yake."
Mromania huyu aliyesilimu anataja sababu nyingine iliyomfanya asilimu na kusema: "Suala jingine lililonivutia kuelekea katika Uislamu ni mafundisho ya Kiislamu kuhusu namna mwanaadamu anavyoweza kuishi maisha bora zaidi. Kabla ya kusilimu nilikuwa nafahamu kuwa maisha ya kifamilia ya Waislamu yamejengeka katika misingi ya Kiislamu. Mfano wa hayo ni sistizo kuhusu kufunga ndoa, kuunda familia, kuwaheshimu wazazi, kuwa na maadili mema n.k. Hayo ni mafunzo ambayo yakifuatwa ipasavyo yanaweza kuwa chimbuko la kuwepo maisha bora kwa mtu binafsi na jamii nzima. Uislamu hata umetilia mkazo suala la usalama wa kimwili na kiroho sambamba na kuwataka watu wajizuie na tabia mbaya zinazoweza kuwadhuru wao binafsi na jamii kwa ujumla.
Bw. Cojocaru hatimaye alifanya uchunguzi wa kina kuhusu dini mbalimbali na hatimaye akafikia natija kuwa Uislamu ndio dini ya haki na hivyo yeye akiwa na mama yake kwa pamoja waliamua kusilimu. Walisilimu wakiwa Stockholm mji mkuu wa Sweden. Anafafanua zaidi kwa kusema: "Kutokana na kuongezeka utafiti wangu katika intaneti na kusoma kwa kina Qur'ani Tukufu nilianza kutafuta misikiti ya mjini Stockholm na hatimaye niliweza kuupata msikiti uliokuwa katika mtaa wenye wakazi wengi Waarabu. Siku iliyoahidiwa ilifika na mnamo tarehe 4 Machi mwaka 2011, baada ya Sala ya Ijumaa mimi na mama yangu tuliingia katika ofisi ya Imamu wa msikiti na kumfahamisha kuwa tunataka kusilimu. Alituuliza maswali kuhusu kiwango cha ujuzi wetu kuhusu Uislamu na kisha akatuarifisha kwa waumini waliokuwepo ndani ya msikiti. Nilikuwa na msisimko mkubwa. Walitukaribisha sote kwa ukarimu mkubwa. Kabla ya hapo nilikuwa sijawahi kuamiliana na Waislamu. Baada ya kusilimu Waislamu walinifunza mengi zaidi na niliweza kujifunza hasa kuswali na kuisoma Qur'ani." Mromania huyu aliyesilimu anasema daima anamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kumrahisishia njia ya kuukubali Uislamu maishani. Anasema kila siku anajitajidi kuwa Mwislamu bora kwani Uislamu ni zawadi aliyoipata kutoka kwa Mwenyezi Mungu na hivyo katika njia ya kushukuru neema na fursa aliyopata anajitahidi kuwa Mwislamu mwenye kutii mafundisho ya Qur'ani Tukufu.