Jan 01, 2017 10:59 UTC

Sura ya Al-Qas’as’, aya ya 5-8 (Darsa ya 683)

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur'ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu. Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur'ani. Hii ni darsa ya 683, na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 28 ya Al-Qas’as’. Tunaianza darsa yetu hii kwa aya ya 5 na ya 6 za sura hiyo ambazo zinasema:

وَنُرِيدُ أَن نَّمُنَّ عَلَى الَّذِينَ اسْتُضْعِفُوا فِي الأَرْضِ وَنَجْعَلَهُمْ أَئِمَّةً وَنَجْعَلَهُمُ الْوَارِثِينَ

Na tukataka kuwafadhili walio dhoofishwa katika ardhi na kuwafanya wawe ni viongozi (wa watu) na kuwafanya ni warithi (wa ardhi).

وَنُمَكِّنَ لَهُمْ فِي الأَرْضِ وَنُرِي فِرْعَوْنَ وَهَامَانَ وَجُنُودَهُمَا مِنْهُم مَّا كَانُوا يَحْذَرُونَ

Na kuwapa nguvu na kuwamakinisha katika ardhi, na kumuonyesha Firauni na Hamana na majeshi yao yale waliyo kuwa wakiyahadhari kwao.

Katika darsa iliyopita tulisema kuwa Nabii Musa (AS) aliamriwa na Allah SW amuendee Firauni na kumtaka aache dhulma na uonevu anaoifanyia kaumu ya Bani Israil. Kwa sababu Firauni alikuwa akiwafanyia madhila na kuwafanya watumwa watu wa kaumu hiyo; na kwa kutumia visingizio tofauti akawa anawachinja wanaume wa Bani Israil na kuwafanya wajakazi wanawake wa kaumu hiyo.

Aya tulizosoma zinaeleza kuwa Firauni alikuwa akidhani kwamba ataendelea daima dawamu kuwa na hatamu za madaraka na utawala na ataweza kufanya kila analolitaka. Hakuwa akijua kwamba irada ya Allah imehukumu kwamba waistikbari na wenye kutakabari watadhalilishwa papa hapa duniani, na wale waliokuwa wakionekana kuwa wanyonge na madhalili watashikishwa hatamu za madaraka na kuwatawala watu hao. Kwa kuchelea na kuhofia Bani Israil wasije wakaanzisha uasi na mapambano na kuuangusha utawala wake, Firauni pamoja na waziri wake Haman walikuwa wakiwahilikisha kwa adhabu na mateso makubwa na kuwaua vijana wa kaumu hiyo waliokuwa na moyo na hamasa kubwa za kimapinduzi. Hata hivyo kile kile ambacho Firauni na wasaidizi wake walikuwa wakikihofia kilikuja kuwapata kwa qudra na irada ya Allah; na kwa uongozi wa Nabii Musa (AS) Bani Israil waliwashinda Mafirauni hao na kurithi makasri pamoja na utajiri na mali zao chungu nzima. Tab'an irada ya Allah SW haiji vivi hivi bila ya sababu wala mantiki. Kwa sababu, ikiwa watu wa kaumu au taifa lolote lile watataka kujikomboa na kukata pingu na minyororo ya dhulma za madhalimu na wao wenyewe wakachukua hatua za kivitendo za kulifikia lengo hilo, Mola Mwenyezi huwapa auni na msaada wake na kuwawezesha kuwashinda madhalimu hao. Hii ni kaida ya uhakika na utaratibu usiobadilika wa Allah SW katika zama zote za historia, kwamba hatima na majaaliwa ya kila umma yanafungamana na amali na matendo ya umma huo; na kwa hivyo kama watu wenyewe wa umma hizo hawatoazimia kivitendo kuleta mabadiliko, hakuna chochote kitakachobadilika katika hatima na majaaliwa yao. Kwa mujibu wa hadithi, katika zama za mwisho wa dunia, yaani aakhiruz-zamaan atadhihiri Imam Mahdi (AS) anayetoka kwenye kizazi cha Bwana Mtume Muhammad SAW, ambaye atapambana na kuwashinda madhalimu na mataghuti wa zama hizo na kuwawezesha wanyonge na waliodhulumiwa kushika hatamu na hivyo kuifanya haki na uadilifu utawale pande zote za mashariki na magharibi ya dunia. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba taqdiri na irada ya Allah ni ya kutaka tawala za madhalimu na mataghuti zing'olewe; na hatamu za madaraka kushikwa na wanyonge na waliodhulumiwa. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa tawala zenye ubinafsi na za kinyonyaji huwadhoofisha na kuwanyongesha watu muhimu na wenye ufanisi katika jamii ili kuweza kuwadhibiti na kuwatawala kirahisi kabisa watu wa jamii hizo. Kadhalika tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba katika zama zijazo, hatamu za uongozi wa dunia zitakuwa mikononi mwa wanyonge na waliodhulumiwa; na hii ni bishara itokayo kwa Allah kwa watu hao ili waendelee kufanya jitihada za kulifikia lengo hilo huku wakiwa na matumaini juu ya mustakabali wao. Wa aidha tunajielimisha kutokana na aya hizi kuwa mbali na adhabu ya akhera, hapa duniani pia tawala na watawala mataghuti na madhalimu hawatosalimika na adhabu ya Mola, ya watu hao kuishia kwenye unyonge na udhalili mbele ya waumini.

Darsa ya 683 ya Qur'ani inahatimishwa na aya za 7 na 8 ambazo zinasema:

وَأَوْحَيْنَا إِلَى أُمِّ مُوسَى أَنْ أَرْضِعِيهِ فَإِذَا خِفْتِ عَلَيْهِ فَأَلْقِيهِ فِي الْيَمِّ وَلا تَخَافِي وَلا تَحْزَنِي إِنَّا رَادُّوهُ إِلَيْكِ وَجَاعِلُوهُ مِنَ الْمُرْسَلِينَ

Na tulimpa ilhamu mama yake Musa kuwa: Mnyonyeshe. Na utakapo mkhofia basi mtie mtoni, na usikhofu wala usihuzunike. Hakika Sisi tutamrudisha kwako na tutamfanya miongoni mwa Mitume.

فَالْتَقَطَهُ آلُ فِرْعَوْنَ لِيَكُونَ لَهُمْ عَدُوًّا وَحَزَنًا إِنَّ فِرْعَوْنَ وَهَامَانَ وَجُنُودَهُمَا كَانُوا خَاطِئِينَ

Basi wakamwokota watu wa Firauni, aje kuwa adui kwao na huzuni. Hakika Firauni na Hamana na majeshi yao walikuwa wenye makosa.

Aya hizi ambazo zinasimulia yaliyojiri baada ya kuzaliwa Nabii Musa (AS) na matukio ya baada yake ni mfano wa kaida na utaratibu usiobadilika wa Allah SW ulioashiriwa katika aya zilizotangulia wa ushindi wa wanyonge dhidi ya waistikbari.

Makuhani wa Firauni walikuwa wamempa habari taghuti huyo kwamba mwaka huu atazaliwa mtoto katika kaumu ya Bani Israil, ambaye katika siku za usoni atakuja kuung'oa na kuuondoa utawala wako. Kutokana na kupewa habari hiyo, Firauni akatoa amri kwamba mtoto yeyote wa kiume atakayezaliwa katika Bani Israil auliwe na wala asihurumiwe wala kusamehewa mtu yeyote yule. Wakati Nabii Musa alipozaliwa, Mwenyezi Mungu SW alimpa ilhamu mama yake kwamba amnyonyeshe mwanawe, kisha amweke kwenye sanduku na kulitia kwenye mto Nile na Yeye Mola ndiye atakayemhifadhi na kumlinda mtoto huyo. Mama wa Musa (AS) alifanya kama alivyoamriwa na Allah; akakichukua kitoto chake kichanga na kukitia sandukuni na kuliacha sanduku hilo lielee kwenye maji ya Mto Nile. Pamoja na hayo alibaki kuwa na majonzi na wasiwasi juu ya hatima ya mwanawe. Katika upande mwengine, Firauni na mkewe, ambao walikuwa wameketi kwenye pwani ya Mto Nile kandokando ya kasri la utawala wake, mara aliliona sanduku linaelea kwenye maji ya mto huo. Firauni alitoa amri sanduku lile liopolewe kutoka majini. Wakati lilipofunguliwa macho yao yaligongana na kitoto kichanga kizuri ambacho hawakujua wakifanyeje. Kwa upande mmoja, Firauni alikuwa ameamuru watoto wachanga wa kiume wa Bani Israil wauliwe; na ni wazi kwamba kitoto hicho kilikuwa ni cha Bani Israil kilichotiwa majini ili kukiokoa na kifo. Na kwa upande mwengine Firauni alikuwa hana mtoto; na mkewe Asia alikuwa akitaka kukifanya kitoto hicho mwanawe wa kulea. Lakini kubwa zaidi ya yote hayo ilikuwa ni irada na taqdiri ya Allah SW, ambaye alimfanya mama yake Nabii Musa aridhie kumtosa majini mwanawe mchanga, na akatia mapenzi pia ya mtoto huyo moyoni mwa mke wa Firauni yaliyomkinga na kumnusuru na kifo. Na kwa njia hiyo akalelewa ndani ya nyumba ya adui yake mkuu Firauni katika hali na mazingira salama kabisa na yasiyo na hatari yoyote ili hapo baadaye aje kuung'oa na kuutokomeza utawala wake wa kidhalimu na wa kitaghuti. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba katika hali ya mkwamo, Mwenyezi Mungu Mtukufu ndiye mlinzi na mwongozaji bora wa waumini, ambaye huwaonyesha na kuwaelekeza kwenye njia ya kujivua na masaibu na matatizo. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa kushukiwa na msaada wa ghaibu hakuna mgongano na utumiaji suhula na nyenzo za kimaada. Tunapaswa kutekeleza wajibu wetu kwa kuzingatia suhula tulizonazo, na vile vile tunapaswa kutawakali na kumtegemea Allah; kama ambavyo mama yake Nabii Musa alimnyonyesha mwanawe, kisha akamtia kwenye sanduku na kutawakali kwa Mwenyezi Mungu. Kadhalika aya hizi zinatuelimisha kuwa japokuwa hatujui hekima na falsafa ya maamrisho mengi ya Allah lakini tusizembee wala kufanya ajizi katika kutekeleza maamrisho hayo, kwa sababu ni hakika isiyo na shaka kwamba kuna siri zimefichika ndani ya maamrisho ya Mola, na hakuna amri au hukumu yake yoyote isiyo na hekima ndani yake. Ni kama ile amri ya Allah kwa mama yake Nabii Musa ya kumtaka amtie mwanawe kwenye maji ya Mto Nile, ambapo muda si muda ilidhihirika hekima yake. Wapenzi wasikilizaji, darsa yetu ya leo ya Qur'ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah aupe izza Uislamu na Waislamu, na aidhalilishe shirki na washirikina. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh…/