Jan 01, 2017 11:04 UTC

Sura ya Al-Qas’as’, aya ya 9-13 (Darsa ya 684)

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur'ani, Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu. Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur'ani. Hii ni darsa ya 684, na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 28 ya Al-Qas’as’. Tunaianza darsa yetu hii kwa aya ya 9 ambayo inasema:

وَقَالَتِ امْرَأَتُ فِرْعَوْنَ قُرَّتُ عَيْنٍ لِّي وَلَكَ لا تَقْتُلُوهُ عَسَى أَن يَنفَعَنَا أَوْ نَتَّخِذَهُ وَلَدًا وَهُمْ لا يَشْعُرُونَ

Na mkewe Firauni alisema: Atakuwa kiburudisho cha macho kwangu na kwako. Msimuuwe! Huenda akatufaa, au tumpange kuwa mwenetu. Na wala wao hawakutambua.

Katika darsa iliyopita tulisema kuwa Firauni na mkewe walikuwa wameketi kando ya kasri lao kwenye pwani ya Mto Nile, mara ghafla macho yao yakagongana na kisanduku kilichokuwa kikielea kwenye maji ya mto huo. Firauni akatoa amri kisanduku hicho kiopolewe kutoka majini. Kilipofunguliwa, akakutwa mtoto mchanga ndani yake. Kulingana na amri aliyotoa Firauni, kitoto hicho kichanga ambacho kilitokana na Bani Israil kilipasa kichinjwe. Kwa hivyo askari wa Firauni wakawa tayari kutekeleza agizo hilo, ndipo mke wa Firauni, Asia akamgeukia mumewe na kumwambia: kwa sababu gani unataka kumuua huyu mtoto! Mtoto huyu anaweza kutuletea bahati na baraka ndani ya nyumba yetu na atakuwa pia kitulizo cha macho kwetu. Sisi hatuna mtoto wa kiume, hivyo tunaweza kumfanya mwenetu kwa kumlea akakulia mikononi mwetu ili hapo baadaye aje kuwa mrithi wa taji na kiti cha enzi cha ukoo wako na utawala wako.

Maneno ya upole, mapenzi na ya kusisimua ya mke wa Firauni yalimfanya taghuti huyo aghairi kumuua mtoto huyo mchanga na badala yake akatoa amri awekwe na kutunzwa ndani ya kasri lake. Kwa hakika wao hawakujua taqdiri ya Allah SW, ambaye alipanga Firauni mwenyewe awe ndiye mlinzi wa maisha ya adui yake mwenyewe; na kwa njia hiyo kufeli na kuzimwa njama zote alizokuwa amezipanga za kuwaua watoto wachanga wa Bani Israil.

Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba mwanamke, anaweza kubadilisha mkondo wa historia na hatima ya umma mzima. Hatua ya mke wa Firauni ya kuzuia kuuliwa Nabii Musa iliwakomboa Bani Israil na madhila na kuwatoa utumwani mwa Mafirauni na kubadilisha mkondo mzima wa historia. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa nyoyo zote ziko kwenye mamlaka ya Mwenyezi Mungu. Atakapo yeye Mola huzilainisha hata nyoyo khabithi na zilizo ngumu kabisa; kama ambavyo moyo katili na khabithi wa Firauni ulilainika, na taghuti huyo akakubali kumlea mtu ambaye, kama ilivyokuwa kwa watoto wachanga wengine wote wa Bani Israil, yeye mwenyewe alikuwa ametoa amri ya kutaka auliwe.

Tunaiendeleza darsa yetu hii kwa aya ya 10 na 11 ambazo zinasema:

وَأَصْبَحَ فُؤَادُ أُمِّ مُوسَى فَارِغًا إِن كَادَتْ لَتُبْدِي بِهِ لَوْلا أَن رَّبَطْنَا عَلَى قَلْبِهَا لِتَكُونَ مِنَ الْمُؤْمِنِينَ

Na moyo wa mama yake Musa ukawa mtupu (kwa jengine ghairi ya kumfikiria mwanawe). Alikuwa karibu kufichua (siri hiyo), lau tusingeliuimarisha moyo wake ili awe miongoni mwa wenye imani (na ahadi ya Mwenyezi Mungu).

وَقَالَتْ لِأُخْتِهِ قُصِّيهِ فَبَصُرَتْ بِهِ عَن جُنُبٍ وَهُمْ لا يَشْعُرُونَ

Naye akamwambia dada yake Musa: Mfuatie. Basi naye akawa anamuangalia kwa mbali bila ya wao kujua.

Baada ya mama yake Nabii Musa kuyasabilia mwanawe mchanga mawimbi ya maji ya Mto Nile, moyo wake ulitibuka na kuhamanika kiasi cha kukosa shwari na utulivu. Alikaribia yeye mwenyewe kuchukua hatua ya kwenda kuliopoa sanduku mtoni na kumwokoa mwanawe. Lakini Allah Mwenyewe, aliyempa ilhamu ya kukitia kitoto chake kichanga sandukuni na kukitosa kwenye mawimbi ya maji ya Mto Nile, alimfanya awe na moyo thabiti, imara na tulivu kiimani, wa kuwa na hakika na ahadi ya Mola kwamba atamrejesha mwanawe mikononi mwake mwenyewe. Kwa hivyo badala ya kuchukua hatua waziwazi yeye mwenyewe, alimtuma dada yake Nabii Musa afuatilie kutokea mbali ili kujua kisanduku kile kinaelea kuelekea wapi na kitafikwa na hatima gani. Je, kuna mtu atakiopoa kutoka majini au kitaendelea kukata mawimbi na kuendelea kusonga mbele zaidi?

Naye dada yake Nabii Musa alitekeleza vizuri agizo alilopewa na mama yake, akawa anafuatilia mwendo na harakati ya kisanduku kile pasina kuonekana na askari wa kasri la Firauni. Hata wakati askari hao walipokiopoa kisanduku hicho kutoka majini, hawakuweza kumwona, la sivyo wangebaini kuwa kuna uhusiano baina yake na kitoto kichanga kilichokuwemo ndani ya kisanduku hicho na ndiyo maana amekuwa akikifuata nyumanyuma.

Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba kutunza siri ni moja ya sifa maalumu za watu waumini; na kufichua siri ni mojawapo ya alama za imani dhaifu; hususan suala hilo linapohusu maadui wa dini wanaotaka kugundua siri za mujahidina na wanamapambano ili kuweza kuwadhuru na kuwaangamiza. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, utulivu wa fikra na sakina na uthabiti wa moyo ni miongoni mwa athari za imani juu ya Allah, na ahadi zake Mola kwa waja waumini. Kadhalika tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba kutawakali kwa Mwenyezi Mungu maana yake si kufunga mikono na kutochukua hatua yoyote kuhusiana na mambo. Pamoja na mama yake Nabii Musa kutawakali na kumtegemea Allah, lakini alimtuma binti yake pia kufuatilia suala la mwanawe. Kuna msemo usemao “Mfunge ngamia wako kwanza, kisha tawakali kwa Mwenyezi Mungu”.

Darsa ya 684 ya Qur’ani, inahatimishwa na aya ya 12 na 13 ambazo zinasema:

وَحَرَّمْنَا عَلَيْهِ الْمَرَاضِعَ مِن قَبْلُ فَقَالَتْ هَلْ أَدُلُّكُمْ عَلَى أَهْلِ بَيْتٍ يَكْفُلُونَهُ لَكُمْ وَهُمْ لَهُ نَاصِحُونَ

Na tukamjaalia awakatae wanyonyeshaji wote tangu mwanzo, mpaka (dada yake) akasema: Je! Nikuonyesheni watu wa nyumba watakao mlea kwa ajili yenu, nao pia watakuwa wema kwake?

فَرَدَدْنَاهُ إِلَى أُمِّهِ كَيْ تَقَرَّ عَيْنُهَا وَلا تَحْزَنَ وَلِتَعْلَمَ أَنَّ وَعْدَ اللَّهِ حَقٌّ وَلَكِنَّ أَكْثَرَهُمْ لا يَعْلَمُونَ

Basi tukamrudisha kwa mama yake ili macho yake yaburudike, wala asihuzunike. Na ajue ya kwamba ahadi ya Mwenyezi Mungu ni ya kweli, lakini wengi wao hawajui.

Ni jambo la kimaumbile kwa mtoto mchanga ambaye ametengana na mama yake kwa masaa kadhaa kushikwa na njaa na kiu na kuanza kuchagiza kwa kilio. Kutokana na hali hiyo Firauni aliamuru akatafutwe mnyonyeshaji kwa ajili ya mtoto huyo. Lakini kwa irada ya Allah SW, kichanga hicho kilichokuwa na njaa kali hakikukubali kunyonya maziwa ya mnyonyeshaji yeyote. Askari wa Firauni walikuwa hoi taabani, wakawa hawajui wakifanye nini kitoto hicho kichanga kilichokuwa hakinyamaziki! Katika hali hiyo, dada wa Nabii Musa, akiwa na hadhari ya kutotamka kitu chochote kitakachowafanya askari wa Firauni wawe na shaka naye, alimtambulisha mama yake kuwa ni yaya na mnyonyeshaji mwenye huruma na mapenzi makubwa, na ambaye ataweza kumtunza vizuri mtoto huyo nyumbani kwake. Askari wa Firauni hawakuwa na la kufanya isipokuwa kulikubali shauri hilo; na bila ya wenyewe kujua wakamrejesha mtoto huyo mikononi mwa mama yake mzazi. Mtoto alipoa na kutulia; na wao pia wakafurahi na kufarajika kwa kuweza kuitekeleza kazi waliyopewa kama walivyotakiwa.

Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba inatakiwa tuwe wajanja tunapokabiliana na adui na kufanikisha lengo tulilokusudia bila ya yeye kujua. Dada yake Nabii Musa hakulitaja jina la mama yake, bali alimtambulisha kwa watu wa Firauni kama mtu asiyemjua. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa tuwe na imani kamili na ahadi ya Mwenyezi Mungu ya hapa duniani na ya huko akhera na wala tusiyapime mambo ya Allah kwa kutumia vigezo na vipimo vya kimaada vyenye kikomo na mipaka maalumu. Wa aidha tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba mtoto ni kitulizo cha roho na moyo wa mama. Akina mama wasiotaka kuzaa na kuwa na watoto kwa dhana kwamba kutokuwa na mtoto ndiko kutakowafanya wawe na raha, kwa kweli wanazinyima nafsi zao raha na utamu wa mazoea ya kuwa na mtoto. Wapenzi wasikilizaji darsa yetu ya leo imefikia tamati. Tunamwomba Allah atupe mema duniani, na akatupe mema akhera na atulinde na adhabu ya moto. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh…/